HEADER AD

HEADER AD

WANANCHI WATISHIA KUJENGA ZAHANATI ENEO LA STEND ILIYOTELEKEZWA

Na Dinna Maningo, Tarime

WANANCHI wa Kijiji cha Ng'ereng'ere Kata ya Regicheri wameitaka Halmashauri ya wilaya ya Tarime mkoa wa Mara, kujenga miundombinu rafiki ya stendi ili itoe huduma baada ya kuitelekeza kwa miaka sita hali ambayo imesababisha mabasi, gari ndogi na malori kutoingia ndani ya stendi.

Wamesema Kijiji hicho kilitoa eneo bure na kuipatia Halmashauri kujenga stendi lakini imeitelekeza na kushindwa kuiendeleza na kwamba endapo haitakarabati, kuboresha miundombinu na kuhakikisha gari zinaingia stendi, eneo hilo watalibadili matumizi na kujenga zahanati kwakuwa kata hiyo haina huduma ya afya.

Wakizungumza na DIMA Online, Calvin Ghati Mwenyekiti wa Kitongoji cha Buhemba Kijiji cha Ng'ereng'ere amesema fedha za Serikali zimetumika kujenga stendi anashangaa kuona haiendelezwi ili huduma za usafirishaji ziendelee.

              Mwenyekiti wa Kitongoji

"Serikali imeweka fedha lakini imeshindwa kuendeleza , sababu ya kujenga stendi hapa kijijini ni baada ya kuona pale Sirari yalikokuwa yanapaki mabasi yanayotoka Mwanza- Sirari hapakuwa na eneo la kujenga stendi tukaombwa tuwape eneo tukawapa bure lakini wamelitelekeza, kama hawaendelezi waseme ili tujenge zahanati.

"Serikali inashindwaje kusisitiza gari zije stendi mbona stendi ya Bweri-Musoma mwanzoni ilikuwa na changamoto wakati huo hata nyumba hazikuwepo lakini Halmashauri ya Musoma ilisimamia magari yakaenda Bweri.

Anaongeza " Hata kule Nyashimo stendi ni ya kawaida sana lakini mabasi yakifika yanaingia stendi ya Nyashimo, vivyohivyo stendi ya Misungwi lakini kwa Tarime imekuwa ngumu kuhamia" anasema Calvin.

Chacha Marwa ameongeza "  Tulitoa hili eneo ili Kijiji kipate maendeleo na mzunguko wa fedha kutokana miingiliano watu wapate ajira lakini stendi ipoipo tu, kama Halmashauri imeshindwa kuhakikisha magari yanaingia stendi waturejeshee eneo letu tujenge zahanati watu wapate huduma ya afya" amesema Chacha.

Hamis Marwa mkazi wa Kijiji hicho amesema wananchi walitozwa gharama Tsh 30,000 kwa kila mmoja aliyeomba kupewa eneo la kujenga kibanda ambapo zaidi ya watu 300 walilipa fedha ili wapewe vibanda lakini wameshindwa kujenga kwakuwa stendi hiyo haieleweki.
              Stendi ya Ng'ereng'ere

" Ili upewe eneo ulikuwa unapewa fomu unailipia elfu 30,000 kama malipo ya kupimiwa viwanja vya kujenga vibanda vya biashara, kama hawaendelezi stendi waturudishie fedha zetu tulizowalipa vinginevyo siku wanakijiji tukiamua watakuta msingi wa zahanati kisha tutaenda huko Halmshauri kudai fedha zetu," amesema Hamis.

Catherine Pozeo ameiomba Halmashauri kuendeleza eneo hilo litoe huduma " Stendi ikifanya kazi sisi wanawake tutaanzisha biashara mbalimbali , tutaanzisha migahawa , tutauza togwa, maandazi na chai tutapata fedha zitakazotusaidia kutimiza mahitaji ya familia" amesema.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Tawi la  Ng'ereng'ere Boniface Mwita amesema kilio cha wananchi wa Ng'ereng'ere wanahitaji stendi ifanye kazi na isipotoa huduma chama hicho kitapakwa matope kwa kushindwa kuisimamia serikali kuhakikisha inatekekeza miradi ya wananchi.

Amesema Halmashauri kutojenga miundombinu rafiki ya stendi ni kukichonganisha Chama cha CCM na wananchi hivyo anaielekeza Serikali kuhakikisha stendi inatoa huduma kama ilivyokusudiwa.

Katika kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya wilaya ya Tarime Novemba, 8, 2022, Diwani wa Kata ya Regicheri kupitia Chama cha Mapinduzi John Bosco, alisema kutofanya kazi kwa stendi hiyo kunaikosesha Halmashauri mapato ya ndani kwakuwa gari haziingii ndani ya stendi kubeba abiria.

           Diwani Kata ya Regicheri John Bisco

"Mapato Regicheri yanapotea ukienda stendi mabasi, gari ndogo na malori hayaonekani ndani hawapeleki kweye eneo linalotakiwa gari zinaunga moja kwa moja kwenda Sirari na mjini Tarime bila kuingia stendi tunakosa mapato" amesema John.

Mweka Hazina wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime Andrew Ndaba katika kikao cha Baraza la Madiwani alikiri stendi hiyo kuwa na mazingira yasiyo na mvuto ," Stendi iliyopo kata ya Regicheri mazingira yake siyo rafiki kwakuwa madhari yake hayavutii kibiashara, eneo hilo siyo sahihi tunaogopa kuwafurumusha kuwaleta kwenye eneo ambalo siyo rafiki tunaangalia namna gani kupaboresha," amesema.

               Andrew Ndaba

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime Solomon Shati aliahidi kuwa Bajeti ijayo wataona namna yakuongeza fedha kwenye miradi kama stendi ya Ng'ereng'ere, Nyamwaga ili ziweze kuwaongezea mapato pamoja na kubaini vyanzo vingine vya mapato.

          Solomon Shati

>>>Stendi ya Ng'ereng'ere ilifunguliwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime Glorious Luoga tarehe 1, Agasti, 2016 ambapo vilijengwa vyumba viwili vya mfano kituo cha polisi na ofisi ya mkuu wa soko.

                Glorious Luoga





No comments