WAKURUGENZI WATAKIWA KUTENGA FEDHA KUTEKELEZA AFUA ZA LISHE
Na Annastazia Paul, Simiyu
MKUU wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Nawanda amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya kutekeleza afua za lishe na fedha hizo zitumike kama ilivyopangwa.
Dkt Nawanda ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye kikao cha kamati ya lishe na mipango ya awali ya bajeti 2023/24 kilichofanyika wilayani Bariadi mkoani hapo ambapo ameeleza kuwa suala la lishe linapaswa kuchukuliwa kwa umuhimu mkubwa na fedha zinazotengwa kutekeleza afua za lishe zitumike ipasavyo.
"Wakurugenzi wa Halmashauri zote ndani ya mkoa huu niwatake sasa afua zote zile na suala la lishe linakuwa ni suala muhimu sana kwenu, likija kwenye meza, mhakikishe mnatenga fedha na zinatumika ipasavyo kutokana na afua inavyotaka.
"Hilo ni jambo muhimu sana na haya yote ni maagizo ambayo wakati mwingine tutakapokuja kuyazungumza yatakuwa kama maazimio yetu ya kikao, kwahiyo fedha zitengwe lakini pia mkishatenga hiyo fedha ikatumike vizuri kutokana na zile afua." Amesema Dkt. Nawanda.
Amesisitiza suala la wanafunzi kupatiwa uji shuleni na ikiwezekana mwakani waanze kupewa chakula kwani kwa kufanya hivyo afya za watoto zitaimalika.
"Ajenda yetu ya kuhakikisha watoto wanakula chakula tumekubaliana mwakani watoto wetu katika shule zote nataka zianze kupata chakula asubuhi na mchana, tukianza na watoto wa awali wapate uji na shule za sekondari pia, huko mbeleni chakula cha mchana tuanze kutoa.
"Tukifanya hivyo basi tutaimarisha afya za watoto na mwisho wa siku afua zitakuwa tumezitekeleza kwa asilimia 100 na mkoa wetu tutang'ara, Simiyu hatuna jambo dogo kila jambo sisi ni jambo kubwa." amesema Dkt Nawanda.
Afisa Lishe wa mkoa wa Simiyu Dkt Chacha Magige amesema karibia asilimia 99 ya watoto mkoani humo wananyonyeshwa maziwa ya mama, huku akitaja kuwepo kwa changamoto ya matumizi ya chumvi isiyo na madini joto.
"Bahati nzuri tuliyonayo kama mkoa ni kwamba angalau watoto karibia asilimia 99 wananyonya maziwa ya mama ingawaje hawafuati utaratibu ambao unakubalika, lakini changamoto tuliyonayo ni matumizi ya chumvi iliyotiwa madini joto.
" Takwimu za mwaka 2018 ni asilimia 23 ndizo zinatumia chumvi yenye madini joto, na hii inatokana na kwamba sisi mkoa wa Simiyu ni moja ya mikoa ambayo inazalisha chumvi kwahiyo chumvi hiyo tunayozalisha ni rahisi mtu anaweza kuchukua kiasi kikubwa kwa gharama ndogo halafu akahifadhi akawa anatumia hata kwa mwaka mzima." amesema Dkt Magige.
Post a Comment