HEADER AD

HEADER AD

TALIRI : WAFUGAJI PANDENI MALISHO,MBEGU BORA ZILIZOFANYIWA UTAFITI


Na Dinna Maningo, Tarime

WANANCHI wilayani Tarime mkoa wa Mara wakiwemo wafugaji wanaeleza umuhimu wa nyasi za asili kwa jamii huku wakisisitiza nyasi hizo ziendelee kudumishwa ili ziwe endelevu kizazi na kizazi kwa faida ya jamii na mifugo.

Mwita Mkami mkazi wa Kijiji cha Nkerege kata ya Kiore anasema nyasi za asili ni muhimu kwa mahitaji ya mifugo, hutumiwa na wananchi hususani wa Vijijini katika ujenzi, usafi wa mazingira, kuzuia mmomonyoko wa udongo pamoja na kutunza uoto wa asili.

" Kuna nyasi zinaitwa Tutu hii inaliwa na mifugo lakini ni nzuri zaidi kwa kuezeka nyumba za asili zilizojengwa kwa kuezekwa na nyasi, zinatumika kuezekea maghala ya kuhifadhi mazao, ukifyatua matofari wakati wa kuzichoma lazima juu ufunike kwa nyasi," anasema.

Judith Wambura ni mfanyabiashara wa nyanya anasema nyasi zina umuhimu kwakuwa wanazitumia kufunika matenga ya nyanya zinaposafirishwa ili zisiharibike na kuharibiwa na jua.


Bhoke Mwikwabe mkazi wa kijiji cha Murito anasema zamani kijiji hicho kiliaminika kwa biashara ya kuuza maziwa kutokana na kuwepo kwa nyasi nyingi za asili zilizowezesha mifugo kupata chakula cha kutosha na hivyo uzalishaji wa mifugo kuongezeka.

Anasema kadri siku zinavyokwenda maziwa yanazidi kupungua kutokana na kuzidi kupotea nyasi za asili zisizotosheleza mahitaji ya mifugo.

"Ng'ombe asiposhiba hatoi maziwa mengi, mwaka 2016 ulikuwa ukikamua ng'ombe mmoja unapata maziwa yanajaa kasuku ya lita mbili, lakini kwa sasa kuna ng'ombe ukikamua hupati hata nusu lita ya Maziwa ," anasema.

Eliasi Musa anasema ," Serikali imekuwa ikijitahidi kupeleka fedha za miradi kwa wananchi kama afya, elimu, maji, pembejeo za kilimo, lakini hatujaona ikisaidia upande wa mifugo kama dawa za mifugo, malisho ya bei nafuu yaliyofanyiwa utafiti ili yawafikie wafugaji wengi kama zinavyotolewa huduma zingine za kijamii.

Anaiomba serikali kuzitambua na kuzifanyia utafiti nyasi za asili kisha maeneo yatengwe kwa ajili ya kuzalisha nyasi za asili na yale maeneo yenye nyasi yadumishwe ili ziwe endelevu na maeneo hayo yasitumike kwa shughuli zozote za kibinadamu isipokuwa tu kwa ajili ya malisho ya mifugo.

Kitini kilichoandaliwa na Idara ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kinaeleza kuwa malisho ni chakula cha msingi cha mifugo kinachojumlisha aina mbalimbali za nyasi na mikunde.


Inaelezwa kuwa utunzaji wa malisho ni muhimu ili kuhakikisha mifugo inapata chakula bora na cha kutosha wakati wote . Ukuaji na ustawi wa aina za malisho hutofautiana kutegemea hali ya hewa na mazingira mbalimbali.

Kitini hicho kinaeleza faida ya kupanda malisho, hurahisisha upatikanaji wa chakula cha mifugo chenye viini - lishe kama wanga, protini, madini na vitamini ,hurutubisha ardhi hasa malisho aina ya mikunde, huzuia mmomonyoko wa ardhi. Miti malisho kama lukina,Sesbania na Grilicidia hutumika kama kuni na Kinga ya upepo.

Mtafiti wa Malisho afunguka

Patrick Rukiko ni Mtafiti katika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Ziwa kituo cha Mabuki kilichopo wilaya ya Misungwi mkoa wa Mwanza, anasema Tanzania ni nchi ya tatu kuwa na mifugo wengi barani Afrika = 30.5 milioni (Tanzania Livestock master plan,2018), inachangia kutoa ajira na usalama wa chakula, wanyama hutumika katika shughuli za kijamii.

Patrick anasema uzalishaji wa wanyama umekuwa ni mdogo kutokana na changamoto mbalimbali katika uzalishaji mifugo unaochangiwa na ukosefu/uhaba wa malisho, hupatikana kwa vipindi, ubora mdogo ambapo upatikanaji ni asilimia 26 ya mahitaji yote.

Patrick anasema kuwa malisho ni chakula kikuu cha wanyama wanaocheua wakiwemo, mbuzi, ng'ombe,kondoo na wanyama wa porini wenye sifa kama hiyo, malisho huchukua zaidi ya asilimia 60 ya mahitaji yote ya chakula.


"Malisho huchukua asilimia 70 ya gharama zote za ufugaji wa ng'ombe wa maziwa, ni chanzo cha mapato kwa wauzaji na wazalishaji na hutunza ardhi/kuzuia mmomonyoko.

Mtafiti huyo anasema kama hakuna malisho bora kwa wanyama, uzalishaji utapungua, mifugo na bidhaa zake bei kuongezeka, pato la mwananchi na Taifa kushuka,vifo, ukosefu wa bidhaa bora, kupotea kwa ajira, migogoro ya wafugaji na wakulima. shughuli za utafiti kwenye malisho.

Anasema Teknolojia za uzalishaji na matumizi ya malisho inakua kwa kasi kutokana na wafugaji kuhamasika, inachagiwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi na kupungua kwa maeneo ya malisho.

Patrick anasema kituo cha Utafiti wa Mifugo Tanzania  TALIRI -Mabuki kinaibua, kinasambaza Teknolojia na kufanya tafiti mbalimbali za ufugaji bora ikiwemo Teknolojia ya uzalishaji wa malisho bora.

Anasema kutokana na tafiti zilizofanyika kwa miaka mingi, aina za malisho ambazo zimesambazwa kwa wafugaji zinahusisha malisho jamii ya nyasi na mikunde.

Anasema TALIRI imefanya utafiti wa malisho ya majani ya asili ya Tanzania kitaalamu yanaitwa Brachiaria ambayo yamethibitika kutoa nyasi nyingi zenye ubora na yanaongeza maziwa kwa asilimia 15- 40 na nyama, yanavumilia ukame na yanastahimili maeneo yenye rutuba ndogo.


             Watafiti wa Malisho kutoka TALIRI wakiwa kwenye nyasi aina ya Brachiaria zilizofanyiwa utafiti

" Majina ya Brachiaria yana uwezo wa kuongeza rutuba kwenye ardhi, unaweza kuyatumia kuzuia mmomonyoko wa udongo, yanafaa kwa kukata kulisha au kuchunga na kuyahifadhi ,bei ya kuagiza ni ghali 45-50 kwa dolla" anasema Patrick.

Anasema lengo ni kuchangia kwa ongezeko la uzalishaji wa mifugo Tanzania kupitia uendelezaji wa majani yaliyoboreshwa aina ya Brachiaria, ukusanyaji wa majani hayo asilia kutoka maeneo yasiyo rasmi nchini, kutathmini utofauti wake, kuchagua majani yaliyo bora kwa ajili ya uendelezaji.

Anasema Taasisi hiyo ya utafiti ilikusanya sampuli za Nyasi katika mikoa mbalimba nchini ambapo kwa Kanda ya Ziwa ni Mwanza, Mara, Simiyu, Shinyanga, Geita na Kagera na jumla ya sampuli 90 za nyasi zilikusanywa. Kanda ya Magharibi ni Kigoma, Rukwa,Katavi na Tabora jumla ya sampuli 90 zilikusanywa.

Kanda ya Kati ni Dodoma na Singida zilikusanywa sampuli 27, Kanda ya Kaskazini ni Manyara, Arusha na Kilimajaro kulikokusanywa sampuli 40 ,Kanda ya Mashariki ni Tanga, Morogoro na Pwani jumla ya sampuli 45 zilikusanywa na Kanda ya Kusini ni mkoa wa Mtwara  na Lindi zilikusanywa sampuli 30 ambapo jumla ya sampuli zote katika Mikoa hiyo ni 289.

Anasema katika matokeo ya awali aina kumi zilizofanya vizuri zilichaguliwa na zimetawanywa katika vituo vingine kwa ajili ya majaribio ya hali ya hewa ,na kwamba kwa wilaya ya Tarime sampuli za Nyasi za asili zilichukuliwa kutoka mtaa wa Gamasara, Bomani, Kijiji Cha Gwitiryo pamoja na Mika wilayani Rorya.


Patrick anasema "  Matokeo tarajiwa ya muda mfupi ni kuwa na taarifa za aina za majani aina ya Brachiaria, kufanyika uchambuzi wa aina bora kwa ajili ya uendelezaji na matokeo ya muda mrefu ni kuwa na taarifa za uzalishaji (breeding) na program ya utunzaji na uendelezaji wa malisho vitakuwepo.

Pia kuimalisha mahusiano ya mashirikiano ya kitafiti kati ya TALIRI Tanzania na BecA - ILRI Hub Nairobi, kuongezeka kwa mazao ya mifugo kwa ajili ya upatikanaji wa malisho bora.

Mtafiti huyo anawashauri wafugaji nchini kubadili mtazamo wao wa kutegemea malisho ya asili, wafugaji na wadau wengine waanze kuzalisha malisho na mbegu Bora zilizofanyiwa utafiti wa kina kutapunguza migogoro ya wakulima na wafugaji.

Anaongeza kwa kusema kuwa Rasilimali fedha bado ni kidogo katika utafiti wa mifugo hivyo Serikali inatakiwa kuwekeza zaidi.


Ilani ya CCM kwa Serikali

Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM ) 2020-2025, Ibara ya 38 inaeleza kuwa sekta ya mifugo ni miongoni mwa sekta muhimu katika ukuaji wa uchumi,kutokana na umuhimu huo ni dhahiri kuwa ipo haja kuendelea kuimarisha ufugaji wa kisasa na kuchakata bidhaa za mifugo kwa ajili ya mahitaji ya ndani,ikiwemo ya lishe bora,na usafirishaji nje ya nchi.
 
      Rais Samia Suluhu akiwa na Ilani ya CCM

Ilani inaeleza mafanikio yaliyopatikana katika ilani ya uchaguzi ya 2015-2020 katika sekta ya ufugaji ni pamoja na kuongezwa kwa maeneo ya ufugaji kutoka Hekta milioni 1.4 mwaka 2015 hadi  Hekta milioni 5.0 mwaka 2020, hadi 2020 vijiji 1,852 vimeandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi kati ya vijiji 12,545 vilivyopo nchini ambapo maeneo ya malisho Hekta 2,788,901.17 yametengwa kwa ajili ya ufugaji katika mikoa 22.

Ibara ya 40 ya Ilani hiyo katika kipindi cha miaka mitano CCM itaielekeza Serikali kuendelea kuleta mabadiliko makubwa na ya kisayansi katika ufugaji kwa kuhimiza ufugaji wa kisasa wenye kuzingatia kinga,tiba na utafiti wa mifugo ili kuzalisha ajira nyingi zaidi hasa kwa vijana na kuinua mchango wa sekta katika pato la Taifa na kuleta ustawi wa wananchi.

Serikali itatakiwa kushughulikia kwa nguvu zaidi migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi ili kufikia azma hiyo,CCM itaielekeza Serikali kujikita katika kuboresha maeneo ya kimatokeo,ikiwa ni pamoja na kuanzisha Mashamba darasa na mashamba ya mfano ya malisho katika vijiji, halmashauri za wilaya na miji nchini. 

Kuimarisha utambuzi na usajili wa mifugo nchini ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wafugaji na mifugo yao,kurekebisha maeneo ya wafugaji kwa kuyapatia huduma muhimu.

Huduma hizo ni maji,afya na elimu kwa ajili ya kusaidia jamii kutulia sehemu moja na hivyo kuepuka kuhamahama kufuata huduma hizo na kuimarisha huduma za maji,malisho na vyakula  vya mifugo ikiwa ni pamoja na kubaini na kutenga maeneo ya ufugaji kwa kuyatambua,kuyapima,kuyasajili na kuyamilikisha ili kuongeza maeneo yaliyotengwa kutoka Hekta 2,788,901.17 hadi Hekta 6,000,000.










No comments