HEADER AD

HEADER AD

UKUSANYAJI MAPATO WATIA SHAKA TARIME DC


>Madiwani wadai fedha za makusanyo zinaliwa

>Hifadhi ya Serengeti yadaiwa kukwepa CSR

>Kamti ya fedha yatakiwa kupitia vyanzo

Na Dinna Maningo, Tarime

MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya Tarime mkoa wa Mara wamesema hawaridhishwi na makusayo ya fedha katika vyanzo mbalimbali vya mapato ya ndani huku wakiitaka Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango kuvipitia upya vyanzo vyote vya mapato.

Madiwani wameitaka Halmashauri kuibua na kubaini vyanzo vipya vya mapato ikiwa ni pamoja na kufuatilia fedha za mapato ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwakuwa hifadhi hiyo imepita pia wilaya ya Tarime katika Halmashauri lakini hailipi kodi na siyo kutegemea tu chanzo cha Mgodi wa North Mara.

Hayo yamebainika katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya kwanza katika mwaka wa fedha 2022/2023 kilichofanyika Novemba, 8,2022 ukumbi wa shule ya Sekondari JK Nyerere katika Kijiji cha Nyamwaga kata ya Nyamwaga .

Madiwani wamesema mapato yanayokusanywa ni kidogo kwani wao wanaamini kuna vyanzo vingi vya mapato lakini pesa zinazokusanywa ni kidogo haziendani na vyanzo halisi vilivyopo na kwamba huwenda fedha zingine zinaishia kwenye mifuko ya watu.

Diwani wa Kata ya Nyanungu Richard Tiboche amesema uhai wa Halmashauri ni ukusanyaji wa mapato hivyo haiwezekani Halmashauri hiyo ikakusanya mapato ya ndani Tsh Bilioni 7 kwa mwaka hili hali vyanzo vya mapato ni vingi, hivyo huwenda fedha zingine zinaliwa na wajanja.


          Diwani Richard Tiboche

" Halmashauri haipaswi kukusanya Bilioni 7 mapato ya ndani , kuna mapungufu katika makusayo na hii ni mara ya 6 au 8 nalalamikia hili jambo,kamati ya fedha pitieni vyanzo vyote vya mapato, zipo hoteli kwenye Halmashauri hii lakini hazilipi mapato, mf. kuna magogo 200 yalisafirishwa lakini mtu akaandikiwa magogo 30 je mengine fedha ilikwenda wapi kamati ya fedha ifuatilie" amesema Tiboche.

Tiboche ameongeza kuwa Kata yake imepakana na Hifadhi ya Serengeti msimu wa mwezi Mei hadi Septemba kuna makampuni ya kitalii wanaoweka kambi ndani ya hifadhi hiyo eneo la Tarime katika shughuli zao za utalii lakini hawalipi fedha za CSR.

"Kule Hifadhini kuna hoteli za muda mfupi zinawekeza kule ndani upande wa Tarime lakini sijawahi kuelezwa hapa ni utaratibu upi unaotumika kupata fedha , na inaonekana makampuni hayo hayalipi fedha kwenye Halmashauri.

" Barabara ya Gibaso inapitisha magari makubwa wale watu wanapitisha vifaa  lakini hawalipi mapato, tunapoenda kwenye mpango wa Bajeti 2023/2024 tubadilike fedha za Halmashauri zinateketea ,zilitengwa fedha kujenga kichomea taka tangu 2018 lakini bado, vyanzo vipitiwe tujue utaratibu zinavyokusanywa na kutumika " amesema Tiboche.

Diwani wa Kata ya Kwihancha Ragita Mato amesema " Kata yangu imepakana na Hifadhi ya Serengeti lakini hawawajibiki kuchangia maendeleo kwa jamii inayoizunguka kama huduma ya maji, afya, mbona mgodi unalipa CSR kwanini hifadhi haitoi wakati imepita hadi wilaya ya Tarime ? Alihoji Ragita.

                     Madiwani

Madiwani wamesema Baraza hilo lilitenga fedha kununua mitambo ya kutengeneza barabara lakini haipo na kutaka kujua kwanini mitambo hiyo haijanunuliwa.

Diwani wa Kata ya Regicheri John Bosco amesema stendi ya mabasi iliyojengwa kwenye kata yake mapato yanapotea kwakuwa gari haziingii ndani ya stendi kubeba abiria.

"Mapato Regicheri yanapotea ukienda stendi ya mabasi na malori hayaonekani ndani hawapeleki kweye eneo linalotakiwa tunakosa mapato ,kuna gari zinasafirisha mazao, miti kupeleka nje sidhani mapato hayo yanakusanywa vilivyo sijui nani anawahakiki, kuna vyanzo vya mapato havikusanywi kama Loko fundi" amesema John.

Diwani wa Viti Maalumu Mariam Mkono amesema kamati ya fedha ndiyo inasimamia fedha na vyanzo vyote vya mapato kwenye Halmshauri hivyo akaiomba kamati hiyo ipitie vyanzo vyote ikiwemo minada kujua ukusanyaji wake .

        Diwani Mariam Mkono

" Kamati ya fedha pitieni upya vyanzo vyote yawezekana havikusanywi vizuri pengine hatuweki mkazo kwasababu tunajua tuna Mgodi wa North Mara unatupatia fedha tujue kesho na kesho kutwa utaondoka " amesema Mariam.

Diwani wa Kata ya Sirari Amos Sagara amesema wachimbaji wadogo wa dhahabu hukatwa tozo ya huduma lakini hana hakika kama Halmshauri inapata fedha na iwapo zinakusanywa aelezwe zimekusanywa kiasi gani cha fedha.

" Kuna wachimbaji wadogo wa dhahabu  kuna mapato huwa yanakatwa je fedha kwenye planti hizo zinaonekana ? kama tunaona zinakusanywa kwa kiasi gani ?, leseni za bucha, maduka ya nguo zimepanda kiholela watu wanatozwa kodi laki moja kodi zinapanda bila kupitishwa kwenye vikao, Madiwani hatujawahi kujadili wala kupitisha viwango hivyo vya tozo,kwanini Sirari kodi yake ni tofauti na maeneo mengine?amehoji Sagara.

            
                Diwani Amos Sagara

Diwani Kata ya Binagi Marwa Marigiri alitaka kujua ni lini ukumbi wa kufanyia vikao vya Baraza la Madiwani utajengwa ili waache kuendelea kutumia ukumbi wa shule ya Sekondari JK Nyerere.

Akijibu malalamiko ya Madiwani Mweka Hazina wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime Andrew Ndaba alikili kutengwa fedha za kununua mitambo ya barabara na kusema fedha hizo zipo kwenye akaunti .

" Ili ununue mpaka upate kibali ofisi ya Waziri mkuu tulishaomba na tumeendelea kufuatilia kwa muda mrefu lakini tukakwama ila imepita wiki moja tumeelekezwa namna ya kufuatilia kibali kwa sasa wamehamishia ofisi ya Rais kupitia Katibu mkuu kiongozi kwahiyo tunaandaa barua kibali kikitolewa mitambo itanunuliwa " amesema Andrew.

Kuhusu ukusanyaji hafifu wa fedha za makusanyo vyanzo vya ndani vya mapato amekirini ni kweli Halamashauri inatakiwa kukusanya fedha nyingi, kuhusu kodi za wachimbaji wadogo wa migodi amesema;


           Mweka Hazina Andrew Ndaba

" Masoko ya dhahabu yanasimamiwa na watu wa madini ambao ndio wanaojua makusanyo kisha wanatupatia taarifa tunapata mapato yetu, kwa soko la dhahabu Nyamongo tumekusanya Tsh Milioni 9 kwa kipindi cha wiki mbili na tumejipanga kuona namna gani tukague mialo na uchenjuaji" amesema.

Akizungumzia chanzo cha mapato cha Hifadhi ya Serengeti amesema kamati ya fedha ilishakwenda Hifadhini na kukutana na uongozi na kwamba kulikuwa na tatizo la kisheria ambalo limeshatatuliwa hivyo kodi imeanza kulipwa Halmashauri.


" Tatizo kampuni nyingi zimesajiliwa nje ya wilaya ya Tarime kwahiyo kodi ya huduma walikuwa wanalipa kule walikosajilia biashara yao, ila sheria ya fedha imefanyiwa mabadiliko sasa watatakiwa kulipa kwenye maeneo wanayozalisha na wameanza kulipa." amesema.

Akieleza kodi za leseni za biashara kupanda kiholela amesema kodi za leseni hazipangwi na Halmashauri zinabebwa na sheria na zimepangwa kingazi ambapo viwango vyake vinatambulika.

Ameongeza kuwa stendi iliyopo kata ya Regicheri mazingira yake siyo rafiki kwakuwa madhari yake hayavutii kibiashara " Eneo hilo siyo sahihi tunaogopa kuwafurumusha kuwaleta kwenye eneo ambalo siyo rafiki tunaangalia namna gani kupaboresha.

Ukumbi wa vikao amesema," Bado ujenzi wa Halmashauri unaendelea unajengwa kwa fedha kutoka serikali kuu na fedha hizo hutolewa kwa awamu, fedha zikiletwa zote ujenzi utakamilika na madiwani watafanya vikao vyao kweye ukumbi wa Halmashauri " amesema Andrew.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mwema Petro Kurate amesema wamepokea ushauri wa Madiwani na wanaandaa ratiba ya kutembelea vyanzo vyote vya mapato.


       Diwani Petro Kurate

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime Solomon Shati amesema ni kweli kuna sababu ya kuweka mipango ambayo itaongeza mapato kwani hawawezi kutegemea mgodi na kwamba Bajeti ijayo wataona namna yakuongeza fedha kwenye miradi kama stendi ili ziweze kuwaongezea mapato pamoja na kubaini vyanzo vingine vya mapato.


     Mkurugenzi Solomon Shati

>>>Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo cha Februari 2021 kilipitisha Bajeti ya Tsh Milioni 535 kwa ajili ya kununua mitambo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

>>>Januari, 2021 katika kikao cha Baraza, Madiwani walitoa muda wa miezi sita kwa Halmashauri hiyo kukamilisha ujenzi wa ukumbi wa kufanyia vikao ambapo walisema hawawezi kuendelea kufanya vikao katika ukumbi wa chakula wa shule na kukalia viti vya wanafunzi.


No comments