UKATILI WA KIJINSIA BADO NI CHANGAMOTO BARIADI
Na Annastazia Paul, Simiyu.
UKATILI wa Kijinsia umetajwa kuwa bado ni changamoto kubwa ndani ya Jamii wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, huku ikielezwa kuwa jitihada zaidi zinahitajika kuhakikisha matukio hayo yanaripotiwa na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria ili kukomesha vitendo hivyo.
Hayo yamesemwa kwenye mkutano wa kutoa elimu ya kupinga ukatili ngazi ya jamii na Mratibu mradi wa kampeni ya kuimarisha usawa wa kijinsia mkoa wa Simiyu Frank Kasamwa, mkutano uliofanyika kata ya Dutwa.
Frank amesema mradi huo unatekelezwa kupitia asasi ya kiraia ya Mass Media na jitihada mbalimbali zinafanyika ikiwemo kutoa elimu ili kuhakikisha vitendo vya ukatili vinaripotiwa na wahusika kuchukuliwa hatua.
"Suala la ukatili kwenye jamii yetu limeshamili kwa hiyo tunapokuja kuimarisha usawa wa kijinsia lazima tuangalie makundi yote hasahasa mtoto, kuna mawakala wa mabadiliko ya tabia ngazi ya jamii hawa watatusaidia kuhakikisha wanawafundisha wazazi/ jamii kujua ukatili unaofanywa dhidi ya watoto.
"Ukatili upo wa aina tofauti tofauti mbali na kuwapatia watoto mimba kuna ukatili pia wa kuwakatisha watoto masomo yao na kuwalazimisha kwenda kuchunga mifugo". amesema Frank.
Ameongeza kusema"Ukitembelea mahotelini ,stendi na mitaani utakuta watoto wanajihusisha na biashara ndogondogo mfano kuuza karanga, mayai badala ya kusoma, ukatili mwingine ni kubakwa na kulawitiwa, tunataka tuwafundishe watoto mbinu za kuripoti matukio ya ukatili ili wapate ujasiri na tunatengeneza channel kwa maana ya daraja kuanzia kwa walimu, viongozi wa serikali ya kijiji mpaka polisi Kata.
Amesema wanakwenda kutengeneza daraja klabu za kupinga ukatili shuleni kwani wanaamini watoto wakianza kuripoti vitendo vya ukatili hatua zitachukuliwa na hivyo kulindwa.
Katibu Tawala wa wilaya ya Bariadi Nicodemus Shirima amewataka wananchi kuachana na vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani kwa watoto na badala yake wawe mabalozi wazuri wa kupinga vitendo hivyo ndani ya jamii na kwa kufanya hivyo vitapungua kwa kiasi kikubwa na hatimaye kutokomezwa.
" Ndugu zangu sisi ndio wa kwanza mradi huu umeanzia kwetu, na sisi tutakuwa mabalozi kwa wenzetu kwasababu tumeambiwa kuna ukatili wa aina nyingi, hata wazazi kutokuchangia chakula cha watoto wao shuleni ni ukatili.
" We fikiria mtoto mdogo ameamka asubuhi saa nyingine usiku hakula vizuri alafu ameenda shuleni amekaa mpaka jioni hajala alafu unataka asome vizuri inawezekana?. Onesha upendo kwa mtoto bila masharti na ukionesha upendo kwake bila masharti ina maana unamjengea kujiamini na pia unamuondolea ukatili wa kijinsia, kutopeleka watoto shule ni ukatili ,kumsomesha mtoto wa kiume na kumuacha wa kike huo ni ukatili," amesema Frank.
Isabela Nyaulingo ni Afisa Tarafa ya Dutwa amewaasa wazazi kuachana na vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani kwa watoto na badala yake wawe chachu ya mafanikio ya watoto hao kitaaluma huku Pastory Msilanga ambaye ni afisa elimu kata hiyo (Dutwa) akisisitiza ufuatiliaji wa kesi za ukatili wa kijinsia zinazoripotiwa ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wahusika.
"Ule mtindo wa kuozesha watoto tuuache ule mtindo wa kusema huyu mtoto mwenyewe hataki shule tuuache tuingie kwenye ushindani wa kitaaluma sawa na mikoa mingine, akina mama tuwe chachu ya kuwaamasisha watoto wetu kwenda shule, watoto wa kike wengi wanafanya biashara na tunawaona kule kwenye biashara ndiko wanakutana na vishawishi". Amesema Nyaulingo.
Mradi huo wa kampeni ya kuimarisha usawa wa kijinsia mkoa wa Simiyu unatekelezwa kwenye kata sita katika wilaya za Bariadi na Busega chini ya ufadhili wa FCS kwa kipindi cha miezi nane kuanzia Septemba 2022 mpaka Aprili 2023.
Post a Comment