AGONGWA NA GARI LA SERIKALI AKISHEREKEA TOHARA (SARO)YA KIJANA WAKE
Na Dinna Maningo, Tarime
MKAZI wa Kijiji cha Nyabichune Kata ya Regicheri Wilaya ya Tarime Mkoa wa Mara, Mwita Magabe mwenye umri wa miaka (43) anauguza mguu uliovunjika baada ya kugongwa na gari inayodaiwa ni ya Halmashauri ya Mji Tarime yenye namba za usajili DFP 4614 (Donor's Fund Project).
Desemba,11, 2022, DIMA ONLINE ilifika katika Kijiji cha Nyabichune kitongoji cha CCM nyumbani kwa Mzee Simion Magabe anayemuuguza mwanae Mwita Magabe aliyegongwa na gari na kuzungumza na baadhi ya wananchi ambao wameelezea tukio hilo.
Namba hizo za gari zimetajwa na wananchi walioshuhudia tukio hilo ambapo Sagara Magabe kaka wa mgonjwa amedai kuwa, gari hilo lilikuwa likitokea Sirari na alilifuatilia hadi lilipokamatwa na askari wa usalama barabarani.
Amesema tukio hilo limetokea Desemba, 5, 2022 majira ya saa sita hadhuhuri katika Kijiji cha Remagwe barabara kuu ya Mwanza-Sirari, na kwamba mgonjwa aligongwa na gari wakati akiwa na wananchi wenzake waliokwenda kumpokea kwa shangwe, vigeregere na vifijo kijana wake Elvis Mwita wa miaka (16) mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya Sekondari Regicheri aliyetoka kutahiriwa jandoni katika Kijiji cha Remagwe.
Sagara anasimulia tukio na kusema," mnamo tarehe 5, Desemba, 2022 tukiwa tunatoka kweye Tohara ya kijana wa kiume wa kaka yangu aliyegongwa na gari la serikali barabara ya lami inayokwenda Sirari, kama unavyojua Kabila la Wakurya hudumisha mila ya asili ya Tohara.
" Kijana anapokwenda kweye Tohara usindikizwa na vijana wa rika lake anaporudi baba mzazi anaenda kumpokea, tukiwa barabarani watu walikuwa wengi wakisherekea tohara (Saro) kijana alisimamishwa ili baba yake ampe zawaidi ya fedha, ghafla lilifika gari likiwa spidi likitokea Sirari likawa linakosakosa watu ndio kumgonga kaka kisha dereva akaondoka na garia bila kusimama.
" Nikaomba msaada wa pikipiki ili kulifukuzia gari nilipofika eneo wanakokuwa askari wa usalama barabarani nikawaambia hilo gari limepita hapa limemgonga mtu na huko sijui ana hali gani ndipo wakawapigia simu kwa wenzao wanaokaa eneo la mto Mori, kweli walisimamisha hilo gari.
Ameongeza " Nikafika nikawaeleza ilivyokuwa askari mmoja akasema tayari tumemkamata tunampeleka kituo cha Polisi Tarime mjini akaingia ndani ya gari hilo wakaondoka, na mimi nikaendelea kuwafuatilia kwa nyuma nikiwa kwenye pikipiki wakafika eneo moja karibu wanakooshea magari na pikipiki jirani na hoteli ya Crisi.
"Nikaona anashuka mwanafunzi mmoja kutoka ndani ya gari akashusha na sanduku, nikamweleza askari kuwa hiyo gari imemgonga mtu kule Remagwe, askari akasema tayari amemkamata anampeleka kituoni.
"Akapiga simu kituo cha Polisi Sirari kuuliza kama kuna mtu kapata ajali na kama kafikishwa kituoni akaambiwa bado akaniambia nifuatilie nione kama wamempeleka kituoni nichukue hiyo PF3 niilete kituoni wathibitishe kama kweli amepata ajali.
Sagara anazidi kueleza,"Gari hilo alikuwemo askari wa usalama barabarani aliyewakamata pale Mori wakawa wanaelekea kama wanaenda kituo cha Polisi Bomani nami nikarudi Sirari kufuata PF3 kisha nikaenda nayo ofisi ya usalama barabarani Bomani.
"Nilipofika ofisi ya usalama barabara nikawaelezea, askari mmoja akanipeleka kituo cha Polisi kipo jirani na ofisi ya usalama barabarani, nilimkuta askari polisi ambaye simjui kama ni OCS.
"Simfahamu kwa jina ila nikimuona nitaitambua sura yake, akaniuliza na wewe? nikamwambia mimi ni ndugu yake na aliyepata ajali, askari aliniambia niende nikalete PF3 ili mthibitishe kama amepata ajali ili faili lifunguliwe kisha nirudishe PF3 hospitali .
" Nikamuonesha PF3 akaniuliza hiyo PF3 umeichukua Sirari au hapa Bomani ? nikamwambia imetoka kituo cha Polisi Sirari alikofikishwa mgonjwa aliyepata ajali, nimekuja hapa Bomani kwakuwa Gari limekamatiwa Tarime mjini mimi natoka Tarime vijijini kule alikogongewa kaka yangu.
Sagara anazidi kueleza " Askari akasema nyie ujinga wenu wa Kikurya hatuhitaji serikalini kwanza huruhusiwi kutembea na PF3 umeishikilia akaninyang'anya na kuniambia nenda mkatibu mgonjwa wenu, mtu wa serikali hawezi kufungiwa ndani wala gari kuzuiliwa kufanya kazi, dereva aliyesababisha ajali sikumkuta kituoni wala gari aliyokuwa anaiendesha sikuikuta.
"Akasema kwanza hiyo ni gari ya serikali haifunguliwi mashtaka istoshe gari imepasuliwa kioo nyie ndio mtatusaidia ushahidi nitawakamata nawadai laki nane ya kupasua kioo, nikamwambia kwahiyo raia hatuna haki ya kushitaki ila watu wa serikali ndiyo wana haki ya kushitaki?.
"Akamwambia yule askari wa usalama barabarani aliyenipeleka kituoni kwamba anikamate aniweke ndani ili nijue kwamba wao ni askari wenye haki nilivyoona anazidi kunipa vitisho nikaondoka zangu kesi haikufunguliwa.
"Nilirudi nikamweleza Mwenyekiti wangu wa Kijiji na Diwani kilichotokea nao wakapiga simu Polisi lakini hawakupewa ushirikiano wowote ,ikabidi ofisi ya serikali ya Kijiji iliandikie barua Jeshi la Polisi Wilaya ya Polisi Sirari kuhusu kitendo kilichotokea nikaipeleka nikaambiwa OCD hayupo askari akanielekeza kwa anayehusika na ajali naye akaniuliza ni ile ajali ya Saro? akasema mwenye gari tayari kawafungulia kesi hawakunisaida nikaondoka"amesema Sagara.
Simion Magabe mweye umri wa miaka (74) baba mzazi wa Mwita aliyepata ajali amesema kuwa, eneo kunakofanyika tohara ya vijana wa kiume ni karibu na barabara kuu ya kwenda Sirari, wakati wa Tohara watu wengi huwa barabarani ambao hufika kuwapokea vijana wao wanaotoka kutahiriwa na husherekea kwa kucheza ngoma ya kikurya (Ritungu).
" Kila mwezi Desemba hufanyika Tohara na inafanyikia pale Buhemba karibu na barabarani na tumekuwa tukipita na vijana wetu kwenye hii barabara, madereva wakishaona Saro hupunguza mwendo na wengine kusimamisha gari, hata gari za serikali zikiwemo za polisi usimamisha gari wanaangalia na kucheka jinsi watu wanavyocheza alafu wanaondoka zao.
"Ila huyu dereva kwanini aendeshe kwa spidi kubwa akijua watu wamejaa barabarani! alifanya makusudi. Na kitendo cha kuchukua PF3 ni kumkwepesha aliyefanya ajali, wamemficha badala ya kutuunganisha pamoja na familia, tangu amemgonga hajawahi kufika kuona hali ya mgonjwa, nina muuguza hapa nyumbani kwangu, wao wanabaki kutishia watu ili wasiende polisi hii imeniuma sana.
Mzee huyo ameongeza kusema " Hata kama mtu alikuwa barabarani serikali haijasema kuwa ukimuona mtu barabarani umgonge umvunje mguu au umuuwe, kwakuwa sheria zipo humwajibisha mtu huyo aliyekwenda kwenye barabara, Rais wetu mama Samia anataka haki kila upande, haki haina maskini wala tajiri," amesema.
Ameongeza," Hata kama gari ni la serikali halitoi haki ya kumgonga mtu naiomba serikali imsaidie mwanangu asiozee ndani, baada ya kuona vile vitisho tulihofia usalama wa mgonjwa maana halikotibiwa ni hospitali ya serikali, gari lililomgonga ni la serikali na askari anayetoa vitisho ni wa serikali, tukaomba uongozi wa hospitali umruhusu atoke tukamtibu nyumbani, yupo nyumbani ameungwa mguu na Mganga wa tiba asilia.
"Mimi sitaki vyesi nachoomba aliyemgonga atoe ushirikiano wa matibabu asiiachie tu familia wakati tatizo kalisababisha yeye. Hatujamleta kumficha taratibu zote za serikali zimefuatwa tukaruhusiwa kumchukua, serikali imetumia kofia zao za madaraka kuficha vitendo vya ajali," amesema Simion.
Shuhuda wa tukio Julius Wang'eng'i amesema " Hiyo barabara gari zinapita nyingi, wakati wa saro (Tohara) madereva wakiona watu wengi barabarani hupunguza mwendo au kusimama. Ndiyo mara ya kwanza kuona gari linamgonga mtu akiwa kwenye saro, gari za serikali, polisi hata wao huwa wanasimama saro inapita kisha wanaondoka lakini huyu alifanya makusudi maana hakupiga hata honi akagonga na kuondoka zake."amesema.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha CCM amethibitisha Mwita Magabe anayepata matibabu nyumbani kwa baba yake mzazi kugongwa na gari na kusema kuwa swala la mahusiano ni muhimu hivyo ni vyema aliyemgonga akafika kumjulia hali mgonjwa na kuchangia matibabu.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Remagwe Antony Barante kulikotokea ajali amekiri kutokea tukio hilo katika kijiji chake lililomuhusisha Mwita Magabe na kusema kuwa, barabara hiyo inatumiwa na watu wengi na ndiyo inayotenganisha Kijiji na Kijiji na kwamaba serikali imeweka mipaka ya utawala lakini haizuii mtu kutumia barabara.
Kijiji cha Nyabichune kinachoongozwa na Mwenyekiti wa Kijiji hicho Wandwi Magola Desemba 10,2022 kiliandika barua kwenda Jeshi la Polisi Wilaya ya Polisi Sirari ikieleza familia hiyo ilivyokosa ushirikiano polisi na kuomba haki itendeke.
Diwani wa Kata ya Regicheri John Bosco amesema baada ya kupokea taarifa za ajali iliyotokea kwa mwananchi wake aliwasiliana kwa njia ya simu na Viongozi wa jeshi la Polisi lakini simu hazikupokelewa mara kadhaa hivyo akailekeza familia kwenda serikali ya Kijiji kuandikiwa barua kisha waipeleke Polisi ili imsaidie mgonjwa kupata haki yake.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Polisi Tarime Rorya ACP Geofrey Sarakikya amesema PF3 ni kielelezo cha Polisi mgonjwa akishapelekwa hospitali na kupata matibabu inatakiwa kurudishwa katika kituo cha Polisi na kwamba kama Polisi haijafungua kesi yao ameiomba familia hiyo kufika ofisini kwake na wafungue kesi.
PF3 ni nini
>>>PF3 ni Polisi Fomu namba 3 (Police form No. 3) ipo kwa mujibu wa kifungu cha 170 cha kanuni za kudumu za Jeshi la Polisi ili mgonjwa aliyepatwa na tukio aweze kupokelewa na kupewa matibabu katika hospitali .
>>>Msingi mkubwa wa hiyo fomu ni kutaka kujua mazingira ya mtu huyo aliumia wapi na alikuwa anafanya nini.
>>> PF3 inatumika pia kama kielelezo mahakamani kama mtu ameshambuliwa, amepigwa au amepata ajali ili Mahakama ijue ameumia kiasi gani na kuwa rahisi kutoa adhabu.
Post a Comment