TANAPA YASHINDA TUZO YA UBORA YA KIMATAIFA
Na Mwandishi Wetu, Ubelgiji
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa mara nyingine tena limeshinda tuzo ya Ubora ya Kimataifa ya mwaka 2022 – (Eurpopean Award for Quality Choice achievement 2022) katika daraja la Diamond inayotolewa na Jumuiya ya Ulayainayojishughulisha na utafiti wa ubora - European Society for Quality Research (ESQR).
Tuzo hii ambayo imepokelewa Desemba, 11, 2022 na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Massana Mwishawa - Mkuu wa Kanda ya Mashariki na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Beatrice Kessy anayesimamia Maendeleo ya Biashara wakiwa na wenyeji wao Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Juma Salum, Vivian Rutaihwa, Stella Mkude katika hafla ya chakula cha usiku iliyoandaliwa na ESQR katika Hotel ya Le Plaza jijni Brussels, Ubelgiji.
Hii ni ni tuzo ya tatu kutolewa na taasisi hii kwa TANAPA ambapo tuzo ya kwanza ilitolewa mwaka 2021 – “Best Practice Award – GOLD category, mwaka 2021 ilipata tuzo ya “Quality Achievement – PLATINUM category na mwaka huu 2022 inapokea tuzo ya Quality Choice – DIAMOND category.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa ESQR, Michael Harris jumla ya kampuni na taasisi 41 kutoka nchi 31 duniani zimeshirikishwa katika kinyang’anyiro hiki ambapo kwa Tanzania ni TANAPA pekee imeshirikishwa.
“TANAPA imekuwa mshindi wa tuzo ya ubora wa juu katika uhifadhi na huduma za kiutalii” Bwana Harris ametangaza wakati wa kukabidhi tuzo hiyo.
Kaimu Balozi wa Tanzania katika Jumuiya ya Ulaya, Ubeligiji na Luxembourg, Bwana Juma Salum ameipongeza sana TANAPA kwa kazi iliyotukuka ya uhifadhi na huduma za utalii kufikia kiwango cha kutambuliwa na jumuiya za kimataifa.
Kamishina wa Uhifadhi wa TANAPA, William Mwakilema amesema inatia moyo kuona jitihada za wahifadhi walioko katika hifadhi za taifa zimetambuliwa na jumuiya ya kimataifa.
“Bila shaka tuzo hii itachochea mioyo ya wahifadhi wetu kufanya kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu zaidi” Mwakilema amesema.
Kamishina Mwakilema amesema pia tuzo ya ubora wa juu itawapa imani watalii na wawekezaji juu ya utendaji bora wa nchi yetu katika myanja ya uhifadhi na utalii.
“Nina imani hii tuzo itakuwa na mchango katika jitihada za Rais wetu Mama Dkt Samia Suluhu Hassan za kuvutia watalii milioni tano kufikia mwaka 2025 kama ilivyoainishwa kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi” Mwakilema amesisitiza.
Post a Comment