ALICHOKISHAURI KANALI KICHONGE WAKATI WA UHAI WAKE
Kanali Kichonge uliniambia kwamba Chifu Manye Mageta alikuwa Chifu toka koo ya Wasweta, alikuwa ni Chifu Mkuu wa Machifu wote Tarime Chifu ambaye katika uongozi wake Mji wa Tarime ulijengwa, bila kusahau ujenzi wa barabara.
Uliniambia Chifu Manye alipambana na wizi wa ng'ombe na kuhimiza watoto kwenda shule, katika uongozi wake walijenga baraza la Machifu walilofanyia vikao na machifu wenzake jengo ambalo kwa sasa linatumiwa na Halmashauri ya Mji Tarime Idara ya elimu, ukatamani eneo hilo kingewekwa kibao chenye jina la Chifu Manye ili kumuenzi.
Chifu mwingine ni Mahende Masero huyu alikuwa Chifu kutoka koo ya Nyabasi Jamii ya Wakurya, huwezi kuamini mwaka 1949 wakati wa uongozi wake lilijengwa baraza la kichifu Nyamwaga katika koo ya Wairege ambapo kwa sasa ndipo ilipo Halmasauri ya Wilaya Tarime.
Kanali Kichonge ulitamani katika Halmashauri hiyo iwepo kumbukumbu ya kibao chenye jina la Chifu Mahende ambaye pia alipambana na wizi wa ng'ombe na kuhimiza watoto kusoma.
Ukasema alikuwepo Chifu Marwa Otaigo ambaye alifanya kazi ya uchifu kwa mwaka mmoja 1950, alifariki Dunia kwa ajali ya pikipiki baada ya hapo Chifu Harun Rhobi aliafanya kazi toka mwaka 1951 hadi 1962.
Uliniambia kuwa, katika uongozi wa Chifu Harun lilijengwa jengo la baraza la Machifu kijiji cha Nyamwigura alipambana na wizi wa ng'ombe.
Kanali Kichonge uliwataja baadhi tu ya Machifu kama mfano, ukasema wapo pia viongozi wengine waliokuwa watumishi ndani ya Serikali wakiwemo viongozi wa Serikali za Mitaa na Serikali kuu waliochangia maendeleo ya Tarime.
Uliniambia Kichonge Mahende alikuwa Mkurugenzi wa kwanza wa Wilaya ya Tarime kazi aliyoianza baada ya uhuru, maendeleo yake yalionekana katika jamii, katika uongozi wake zilijengwa zahanati, shule za msingi pamoja na barabara katika vjiji mbalimbali.
Maendeleo mengine ni ujenzi wa Zahanati ya Nyamwigura, Itandora,Nyamongo,Nyamwaga, Nyakunguru pamoja na Ochuna na Kinesi ambazo ziko Wilayani Rorya kabla ya Rorya kuwa Wilaya .
Shule za msingi zilizojengwa ni Magoto,Nyamongo Sirari na nyinginezo pia alihimiza upandaji miti mjini na vijijini, barabara mfano barabara ya Borega ,Magoto na nyinginezo.
Si hayo tuu yalijengwa malambo ya maji pamoja na majosho ya ng’ombe ambayo mengine yanaendelea kutumiwa hadi leo. Zilijengwa Mahakama ndani ya Wilaya ya Tarime na baada ya hapo alipanda cheo na kuwa Mkaguzi Mkuu wa Mahakama zote Tanzania.
Kanali Kichonge ukazidi kunisimulia watu mashuhuri ukamtaja Bhoke Mnanka huyu alikuwa mbunge na Waziri wa Kilimo akiwa Waziri wa kwanza toka Tarime.
Uliniambia katika uongozi wa Bhoke ilijengwa shule ya Sekondari Tarime ambayo baadaye ilibadilishwa kuwa shule ya wavulana kwa ngazi ya Kidato cha tano na sita, kilijengwa kiwanja kidogo cha ndege na kuiboresha Hosptari ya wilaya Tarime.
Ulimtaja Werema Chambiri ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, katika uongozi wake alipinga mila potofu ya kukeketa watoto wa kike, alizuia wanawake kutoboa masikio na kuvaa vyuma mikoni vilivyowaumiza na kuwaachia alama.
Ukaniambia vyuma hivyo vilikuwa vinaitwa "VITANKE", alisisitiza elimu , alipambana na wizi wa ng’ombe, barabara ziliboreshwa, katika uongozi wake likajengwa jengo la ofisi ya CCM Wilaya ya Tarime, bila kumsahau Christopher Ryoba Kangoye aliyefanya kazi mbalimbali Serikalini ikiwemo nafasi ya ukuu wa Wilaya zilizochangia yeye kuleta maendeleo Tarime.
Alikuwepo Charles Musama Nyirabu ambaye alikuwa Gavana wa pili wa Benki kuu Tanzania toka Tarime akidumu katika nafasi hiyo tangu 1974-1989, alifanya kazi na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwaka 1990-1994 aliteuliwa kuwa balozi Nchini Marekani huyu ndiye kiongozi aliyefanya kazi miaka mingi kwenye benki ya Taifa, katika uongozi wake ikaletwa huduma ya umeme pamoja na simu za mezani.
Ulisema Gavana huyo katika uongozi wake ililetwa kampuni ya Cocacola kanda ya ziwa, aliwaunganisha wafanyabiashara, pia atakumbukwa katika uongozi wake zilijengwa baadhi ya benki, Arusha, Mwanza, Mbeya pamoja na chuo cha biashara CBE.
Ukaniambia aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi katika uongozi wake ndiye aliyewatoa gizani wananchi wa Tarime vijijini kwa kupata umeme wa Rea kwa gharama nafuu, katika uongozi wake ikajengwa shule ya sekondari ya Wasicha Borega, alitoa vibali kwa wachimbaji wadogo wa madini.
Yupo pia aliyekuwa Katibu Mkuu TAMISEMI Eng. Joseph Nyamhanga, huyu kupitia uongozi wake baadhi ya barabara zilijengwa na baadhi ya vijana walipata ukurugenzi, lilijengwa daraja la Mto Mara pamoja na barabara ya Tarime - Mugumu.
Mwita Mahende Masero aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Kilimo na Mifugo alitoa ajira kwa vijana wa Tarime pia aliwapatia vijana wa Tarime miradi ya kufuga kuku bila kumsahau Mama Gaudensia Kabaka ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Ajira na Kazi akiwa ni Waziri wa kwanza Mwanamke toka Tarime, alisaidia vijana wa Tarime wakapata ajira na baadhi walijiendeleza na hadi kupata ukurugenzi.
Kanali Kichonge hukuishia hapo uliwataja waliopata Ujenerali wazawa wa Tarime ambao wanastahili kuenziwa ili kutunza historia kwa vizazi vijavyo ambapo Generali Mwita Kiaro alikuwa Mkuu wa Majeshi wa kwanza toka Tarime akifuatiwa na Generali George Waitara.
Uliniambia wapo Viongozi wastaafu na waliopo kazini wazawa wa Tarime, wakiwemo Maafisa wa Usalama wa Taifa na Viongozi wa Majeshi mbalimbali waliochangia maendeleo Tarime wakiwemo Majerali ,Meja, luteni, Mabrigedia pamoja na makanali.
Ulisema viongozi hao walitoa michango yao katika Wilaya ya Tarime kama vile Luteni General Chacha Ryoba, Meja General Mwita Marwa,Meja General Maseke Gimonge, Meja General Igoti, Meja General Mbuge, Meja General Sibuti,LT. COZ Kanal Muhindi walikuwa na mchango mkubwa ambao walisaidia pia vijana wa Tarime kupata ajira Jeshini.
Bila kumsahau Kanali Mstaafu Ambrose Magabe toka Tarime ambeye pia aliwahi kuwa Mwambata wa Kijeshi Nchini India (Military Attach), alipokuwa Makao Makuu ya Jeshi Jijini Dare es salaam wakati huo alisaidia vijana toka Tarime wakapata ajira na kozi mbalimbali Jeshini.
Ulisema alikuwepo Mbote Nyirabu alikuwa Katibu Mkuu Utumishi wa kwanza toka Tarime, alitoa ajira kwa vijana toka Tarime ambao waliajiriwa kwenya mradi wa magugu maji pia ajira kwenye utumishi na ualimu na aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Mambo ya Ndani.
Kanali Kichonge uliniambia unasikitika kuona hali ya mazingira ilivyo sasa Tarime, unamtaja aliyekuwa Afisa Misitu na Wanyama 1970-1998, Beatus Mnibi kuwa anastahili kuenziwa kwa jinsi alivyoifanya Tarime ya miaka ya nyuma kuwa ya kijani na yenye kupendeza, unasema misitu iliyoanzishwa wakati wake Tarime na Rorya imeharibiwa.
Ulisema alipanda miti kwa bidii Tarime ikapendeza lakini kwa sasa hakuna tena historia hiyo, misitu iliondolewa maeneo mengine zikajengwa nyumba na misitu mingine iliharibiwa na wananchi ambao hawakujua umuhimu wake.
Kanali Kichonge uliniambia unashangazwa na jina la kibao ukiwa unaingia Tarime njia panda ya kuingi Tarime Mjini na ile barabara ya kuelekea mji wa Sirari ulioko mpakani na nchi jirani ya Kenya, licha ya kibao hicho kuwepo ukiwa unaingia Tarime mjini kimeandika Kenya Road, ambapo kilipaswa kuwekwa kule Sirari kata ya mpakani na Kenya.
“ kile kibao nashauri kibadirishwe jina na kuwekwa jina la kiongozi yeyote mashuhuri lakini sio kuitwa Kenya road inamana unapoingia nyumbani tena ni Kenya unaingia?, wapo viongozi wengi wanaweza kuangalia watumie jina la nani sio kuandika Kenya, pia viongozi mashuhuri wapewe majina ya mitaa ya mjini kati sio pembezoni mwa mji.” ulisema Kanali Kichonge.
Ulisema Wilaya ya Tarime ina wasomi mahiri na wakufunzi kama vile Prof. Manamba Binagi, Mwita Wangwe, Mohabe Nyirabu, Chacha Nyaigoti pamoja na Prof. Ibrahim Juma Jaji Mkuu wa Tanzania wa kwanza toka Tarime.
Ukaniambia katika uongozi wake zimejengwa Mahakama mbalimbali nchini na zingine kuboreshwa, amefanikisha vijana kupata ujaji na uhakimu, katika uongozi wake kesi nyingi za uonevu zimepunguzwa pamoja na kudhibiti maadili ya watumishi wa Mahakama.
Kanali Kichonge hukuwasahau kuwataja Wafanyabiashara wenye mchango mkubwa wilayani Tarime kama vile Mjumbe wa Halmashuri Kuu Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Christopher Mwita Gachuma Mkurugenzi wa Kampuni ya Cocacola, alisaidia Zahanati kujengwa Manga, Alikuwa tajiri wa kwanza kujenga hoteli ya CMG anayemiliki pia Mwanza Hotel, amekuwa na mchango mkubwa ndani ya CCM.
Uliwataja baadhi ya walioanzisha biashara ya usafirishaji wa abiria miongoni mwao ni Chacha Mkohi, Mwita Chacha Manko na baadae Peter Zakaria hukumsahau pia mfanyabiashara maarufu mwanamke Agnes Mwita Chacha Manko.
Katika utoaji wa Huduma ya Afya kwa jamii hukusita kumtaja Dkt. Hadson Weinani aliyekuwa daktari wa kwanza kujenga Hospitali binafsi inayotoa huduma ya upasuaji, alileta chakula cha msaada kwa waliopatwa na njaa na misaada mingine.
Ushauri wa Kanali Kichonge
Kanali Kichonge ulishauri kwamba kama itawapendeza wanatarime basi viongozi mashuhuri wa kiserikali na machifu wazawa waliosaidia maendeleo majina yao yaenziwe kwa kuandikwa kwenye vibao vya mitaa katikati ya mji na siyo vibao vyenye majina ya viongozi mashuhuri kuwekwa barabara za pembezoni ya mji maeneo kuliko jengwa nyumba zao ambako watu hawapitipiti kwa wingi.
Uliniambia kuwa mjini kati wanapita watu wengi hivyo wakiviona watakuwa na uchu wa kufahamu sifa na histori zao ambazo zitasaidia kudumishwa kizazi hadi kizazi kuliko vinapokuwa pembezoni.
Ulishauri libadilishwe jina kwenye kibao kilichopo njia panda unapoingia Tarime mjini kilichoandikwa Kenya road badala yake kibao hicho liandikwe jina la kiongozi mashuhuri, na jina la Kenya road likawekwe Kata ya Sirari jirani na forodhani mpakani na nchi ya Kenya.
Pia ulisema ni vyema yale maadhimisho ya siku ya uhuru yakafanyika pia na wilayani ili kutoa fursa ya kuwaenzi viongozi mashuhuri waliosaidia wilaya zao kupata maendeleo, kukumbushana historia ya wilaya na mafanikio yake, kwakufanya hivyo vizazi vijavyo vitajifunza na kuenzi yaliyotendwa na viongozi hao mashuhuri.
Makala hii imeandaliwa kwa ushirikiano wa Kanali Mstaafu wa Jeshi la Wananchi (JWT) Kichonge Mahende Masero, aliyetumikia Jeshi hilo tangu mwaka 1971-2004 ambaye kwa sasa hatuko naye baada ya kufariki dunia ghafla.
Rejea:
Kanali Kichonge wakati wa uhai wake mwezi Julai, 2020 alijitosa kuchukua fomu ofisi ya CCM Wilaya ya Tarime kutia nia ya kugombea ubunge jimbo la Tarime mjini ambapo alifika kuchukua fomu na kurejesha kwa kutumia usafiri wa mkokoteni, kura hazikutosha kumwezesha yeye kuteuliwa Kugombea ubunge.
Kwaheri Kanali Kichonge, pumzika kwa amani.
Post a Comment