CCM MARA : MABALOZI WA MASHINA WAHESHIMIWE
Na Jovina Massano, Musoma
VIONGOZI na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Mara wametakiwa kuwaheshimu mabalozi wa mashina kwa kuwa ndio msingi mkuu wa Chama.
Hayo yameelezwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mara Patrick Chandi na Wajumbe wa Halmashauri kuu Taifa (NEC) ya Chama hicho, Christopher Gachuma na Joyce Mang'o wakati wa uzinduzi wa mashina 3 uliofanyika Manispaa ya Musoma.
"Chama cha Mapinduzi kinahitaji nidhamu na heshima lazima haya yaanzie chini kwa viongozi wetu wa mtaa mpaka mkoa kwani sote ni wajenzi wa nyumba moja na sisi ni viongozi wa wananchi hivyo ni vema tukatambua wajibu wetu na kuwaletea wananchi Maendeleo kuhakikisha nchi inasonga mbele",amesema Patrick.
Amesema mabalozi ni watu muhimu katika kukijenga chama cha CCM, amewasihi kuendelea kukitumikia chama kwa moyo wote huku akipongeza mabalozi kwa kufanya kazi yao vizuri ya kukisimamia Chama na kushiriki kikamilifu katika shughuli za chama.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) Mwita Gachuma amewapongeza mabalozi wote kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za chama kwa kutambua wajibu wao kwa chama bila kusahau mabalozi wanawake.
"Chama cha Mapinduzi kinawategemea sana kina mama nawaomba muendelee kuwa mstari wa mbele kukitetea kwa kuwa ninyi ndio walezi wakuu wa familia mnauvumilivu tofauti na sisi wanaume tukivurugwa kidogo tu tunahama na kutelekeza familia zetu simameni kidete nchi isonge mbele,"amesema Gachuma.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (,NEC) kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Bara, Joyce Mang'o amesema viongozi wa mashina ndio wanaoshikilia Chama kwa kiasi kikubwa hivyo chama kinatambua umuhimu wao.
Joyce Mang'o
"Viongozi wa shina ndio wanaoshika chama nawaomba viongozi wote kuwaheshimu mabalozi hawa kwani kazi yao ni kubwa, hawa ndio chanzo cha ushindi tuone thamani yao tuwe nao bega kwa bega ili chama kizidi kuimarika"amesema Joyce.
Post a Comment