HEADER AD

HEADER AD

PROF. ABEL ASISITIZA ELIMU YA BIMA ITOLEWE KWA WANANCHI


Na WAF, Dodoma

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesisitiza elimu ya Bima ya afya itolewe kwa wote ili kuongeza idadi kubwa ya wananchi walio na Bima.

Prof. Abel ameyasema hayo wakati alipokuwa akifungua kikao kazi cha Menejimenti ya Wizara na Taasisi za Wizara hiyo kilicholenga kupitia utendaji kazi wa Wizara na Taasisi zake ikiwa ni pamoja na kuendelea kuweka mikakati ya uboreshaji wa huduma za afya nchini.

“Tuendelee kushirikiana kutoa elimu ya Bima ya Afya kwa kadri inavyowezekana, ile kasi ambayo tulikuwa nayo tuendelee nayo kwa sababu wananchi wengi bado wanahitaji kuelewa juu ya Elimu ya Bima ya Afya” amesema Prof. Makubi.

Prof. Makubi amesema kuwa maswali yote ambayo bado hayajapata majibu yajibiwe na kutoa sintofahamu kwa wananchi kabla ya kuekelea kwenye mchakato wa  Bima ya Afya ambao unatarajiwa kurudi Bungeni mnamo mwezi Januari 2023.


“Elimu hii ya Bima ya Afya pia itolewe katika Hospitali zetu ngazi zote hivyo niwatake Waganga Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Waganga Wafawidhi wa Hospitali zetu zote kutoa elimu ya Bima ya Afya kwa wote” amesisitiza Prof. Makubi.

Amesema hospitali zetu zinategemea Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kujiendesha hivyo kwa Bima ya Afya  ni lazima taasisi zetu zilee na kuutunza Mfuko huu usife ili uweze kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.

Prof. Makubi amewataka watendaji katika vituo vya kutolea huduma za afya kuboresha utoaji wa huduma za afya ili kuwa na uhakika wa kutoa huduma bora za bima kwa wateja pindi Bima ya Afya kwa wote itakapopitishwa.



No comments