WAIBA MTOTO WAKATI MAMA AKISINDIKIZA WAGENI
Na Alodia Dominick, Bukoba
WATU ambao bado hawajafahamika wanadaiwa kuingia ndani ya nyumba ya Joanitha Augustine mkazi wa mtaa wa Migera Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera na kuiba mtoto (kichanga) wa mwezi mmoja aitwae kwa jina la Benitha Benedicto.
Akizungumza na vyombo vya habari Desemba 02,2022, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Kagera William Mwampaghale amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa limetokea Desemba mosi, 2022 majira ya 21:30 usiku nyumbani kwa mama wa mtoto huyo.
Mwampaghale amesema Desemba mosi majira ya saa 19:00 jioni kabla ya tukio walifika wanawake watatu nyumbani kwa Joanitha kwa lengo la kumpa pongezi ya kujifungua.
Kamanda amesema watu hao walikuwa wanafahamiana naye na walikuwa majirani zake wakati alipokuwa akiishi Omukigusha kabla hajahamia Migera ambapo badae aliwasindikiza wakaondoka.
"Watu hao baada ya kuondoka miongoni mwao wawili walirudi kwa huyo mama majira ya saa 21:30 usiku na kumweleza kuwa wana mazungumzo naye aliwakatalia na kuwataka wazungumze Desemba 2,2022 hivyo wakamuomba awasindikize, akawasindikiza aliporudi ndani amekuta mtoto hayupo kitandani" amesema Mwampaghale.
Kamanda amesema Jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa kubaini waliohusika na wizi wa mtoto huyo na kwamba watakaobainika watafikishwa mahakamani.
Post a Comment