HEADER AD

HEADER AD

CHADEMA: CCM ISHUGHULIKIE RUSHWA UCHAGUZI WAO SIYO VIDEO CLIP


Na Dinna Maningo, Tarime 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, kimekitaka Chama cha Mapinduzi (CCM) kushughulikia vitendo vya rushwa vilivyokithiri na kuota mizizi katika uchaguzi wa viongozi ngazi mbalimbali ndani ya Chama huku Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ikikaa kimya bila kuchukua hatua.

CHAMA hicho kimesema CCM kabla ya kuinyooshea kidole CHADEMA ijitathmini matukio mbalimbali ya kiunyanyasaji, uonevu na udhalilishaji yaliyofanywa na wanachama wake dhidhi ya wanachama wa CHADEMA.

Akizungumza na DIMA Online Mkurugenzi  wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, John Mrema amesema hayo kufuatia taarifa iliyotolewa kwa umma na Chama cha Mapinduzi ikilaani vikali kilichofanyika kupitia Video Clip iliyosambaa Mitandaoni.

Video hiyo ilikiibua Chama cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya Taifa  Novemba,29,2022 kupitia Katibu Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu, Chama kililaani vikali kitendo kilichofanywa na Mwanachama wa CHADEMA Mwl. Chacha Heche dhidi ya Marwa Mgeni kumtaka avue vazi ambalo ni sare ya CCM.

 Shaka Hamdu wa CCM

CCM imesema kitendo hicho ni cha udhalilishaji na utwezaji wa haki ya msingi ya mtanzania kuamini katika imani ya chama chake bila kuingiliwa na ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 3 (1) na ibara ya 20 (1) na Sheria namba 5 ya Vyama vya Siasa na marekebisho yake 2018.

Pia Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Tarime kikizungumza na Waandishi wa Habari kupitia Katibu wa Chama hicho Varentine Maganga, kimemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Tarime Kanali Michael Mtenjele kuchukua hatua huku kikiwataka Viongozi wa CHADEMA na Chacha Heche wajitokeze kuomba msamaha kwa watanzania, CCM na kwa Marwa Mgeni kwa kitendo kilichofanyika kupitia Video Clip.

John Mrema amesema hizo ni propaganda na hawana muda wa kujibu hizo propaganda kwani wenzao wa CCM wanataka kuanzisha mijadala baada ya uchaguzi wao kukumbwa na rushwa rukuki sasa wanatafuta mahali pakushikilia iwe ndiyo ajenda ya nchi.

               John Mrema wa CHADEMA

"Washughulike kwanza na rushwa kwenye uchaguzi ndani ya chama chao ambayo imekithiri imeota mizizi , kuna Video Clip zimesambaa nchi nzima na hatuoni hata mmoja akinyanyua mdomo akichukua hatua kuwa fulani achukuliwe hatua, hatuoni TAKUKURU ikichukua hatua, matokeo yake tunaona wapo kimya tu.

"Sasa wanatafuta kitu cha kufanya jamii iwe bize badala ya kujadili mambo makubwa ya kitaifa wanaenda kujadili mtu mmoja aliyejirekodi anavua nguo, mi nafikiri huo ni mwendelezo wa propaganda na sisi kiukweli hatuna muda wa kijubu hizo propaganda tuna mambo mengi" amesema John.

John Mrema amesema wapo wanachama wa CHADEMA waliovuliwa nguo, wakachukuliwa kwa nguvu na Video Clip zilisambaa mitandaoni lakini hawajawahi kuona CCM ikikemea hata siku moja wala kuchukua hatua.

" Wapo waliokuwa viongozi wa CCM tena ngazi ya kitaifa akiwemo ambaye sasa ni DC wa Ubungo alikuwa akitoa matamshi mabovu kwenye nchi hii, hakuchukuliwa hatua yoyote badala yake alipongezwa na kupandishwa cheo kuwa mkuu wa wilaya.

"Kuna matukio mabaya yamefanywa na wana CCM lakini hawajawahi hata kukemea , Katibu Mkuu wa UVCCM alipokuwa Katibu wa Chama kule Iringa alitoa kauli zenye ukakasi sana badala yake alipandishwa cheo akapelekwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Arusha, nako akatoa kauli mbaya kabisa hasa kwenye uchaguzi mkuu wa 2020, wakaona huyu anastahili akapandishwa cheo na siyo kukemewa ndiyo akawa Katibu mkuu wa Umoja wa Vijana Taifa" amesema.

Amesema matukio ya uonevu na udhalilishaji ni mengi yaliyofanywa na wanaccm" Umewauliza CCM kuhusu Mkuu wa Wilaya ya Hai mwanachama wao alipoumiza watu? sasa tatizo lenu mnataka kutuuliza sisi Chama wakati siyo kazi ya Chama wala Chama hakikuzungumza kwenye hiyo Video Clip.

Ameongeza " Huyo mwanachama wa CCM kwanini yeye alikubali kuvua nguo? alijidhalilisha mwenyewe, angekuwa anaona ni udhalilishaji angemwambia bwana kazi yako haina umuhimu kwangu kwa sababu hii ni nguo ya chama changu alafu ninaondoka zangu.
   
           Marwa Mgeni aliyevua sare ya CCM baada ya kuambiwa avue

" Kwanini aliamua kuvua nguo, anarekodiwa na kusambaza mitandaoni alafu wanasema kadhalilishwa, ndiyo maana nasema hii ni propaganda wanajaribu kuziseti ambazo kwa sasa sisi hatuana nafasi za kuzijibu, tujadili masuala makubwa ya Taifa" amesema John.

Mkurugenzi huyo amesema anamshangaa Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime Varentine Maganga kwa kumwagiza Mkuu wa Wilaya ya Tarime Kanali Michael Mtenjele kuchukua hatua na kwamba hana mamlaka hayo.

             Varentine Maganga Katibu CCM

"Nimemsikiliza huyo Katibu wa CCM Wilaya akiwa anamtaka mjumbe wake wa kamati ya siasa achukuwe hatua, kwa mujibu wa katiba ya CCM ibara ya 77 kifungu (c) wajumbe wa siasa Wilaya kina mtaja Mkuu wa Wilaya husika, sasa katibu anatoka kwenye kikao cha kamati ya siasa alafu anaenda kumuagiza mjumbe wake wa kamati ya siasa achukuwe hatua na hasemi ni kwa mujibu wa kanuni ipi.

"Huo ni mwendelezo tu wa propaganda yanaenezwa kwa makusudi kwahiyo sisi hatuna muda wa kijubu hizo propaganda, kwa wakati huu tuna mambo mengi ya kushughulika nayo, usajili wa wanachama kwa njia ya mtandao, tuna mambo mengi yakufanya kama Chama" amesema.

John Mrema amesema kilichozungumzwa kwenye Video Clip hakikuzungumzwa na Chama na siyo maneno ya Chama.

            Chacha Heche aliyemwambia mwana CCM avue sare 

" Kama unaulizia kuhusu Video Clip watafute wenye Clip yao uwaulize, wanachama wetu hatujawawekea mipaka ya kuzungumza kwa mambo binafsi ya watu hatuna mamlaka nayo, mtu kuwa mwanachama siyo kwamba Chama kina uhuru na mambo yake binafsi anayofanya.

" Katibu wa CCM ametumia uhuru wake kumwagiza mjumbe wa kamati yake ya siasa ya wilaya achukue hatua.Mkuu wa Wilaya ni mjumbe wa kamati ya siasa kama wanataka awe kiongozi wa Serikali wafute hiyo ibara ya 77.

" Lakini hawajafuta mpaka leo kwahiyo ni mwanachama wake, katibu anamwagiza mjumbe wa kikao chake aende achukue hatua dhidhi ya mwanachama wa chama kingine bila hata kusema ni kwa mujibu wa ibara ipi au katiba ipi au sheria ipi, katibu hana mamlaka ya kuagiza" amesema John.

Je Wanachi wao wanasema nini kuhusu Video Clip hiyo? Endelea kufuatilia DIMA Online itakujuza.


No comments