HEADER AD

HEADER AD

WANANCHI WAVUTANA KUHUSU VIDEO CLIP

 


Dinna Maningo na Jovina Massano

Tarime/ Musoma

BAADHI ya Wananchi Mkoani Mara wameeleza mitazamo yao juu ya Video Clip ya hivi karibuni iliyosambaa katika Mitandao ya Kijamii.

Katika Video Clip alionekana Chacha Heche mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akimtaka Marwa Mgeni mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wote wakazi wa Tarime mjini  kuvua tisheti aliyokuwa ameivaa ya rangi ya njano yenye nembo ya kijani ambayo ni sare ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Marwa Mgeni alikuwa anafanya kibarua cha kuponda Kokoto katika familia ya Heche, naye akatii na kuvua sare hiyo kisha akaendelea na kazi akiwa kavaa kaushi. kitendo hicho kiliibua mijadala wengine wakisema ni kitendo cha udhalilishaji na wengine wakisema ni kitendo cha kawaida kwa wanasiasa.

DIMA Online imezungumza na baadhi ya wananchi mkoani Mara  ili kufahamu wao wanasemaje kuhusu Video Clip hiyo na nini maoni yao, nao walikuwa na haya ya kusema;

Mwita Mantago mkazi wa mjini Tarime  amesema " Siasa siyo ugomvi kazi ni kazi na siasa ni siasa ,kitendo nilichokiona kwenye Clip hakijanifurahisha, kimemdhalilisha yule mzee, anamwambia avue nguo mbona ana kaka yake ni kada wa CCM nyumbani wanakaa meza moja wanakula chakula na anavaa sare hizo za CCM mbona hajamfukuza au kumwambia avue nguo ya CCM ?

"Huyo Kaka yake ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa akitokea Wilaya ya Tarime na wakati wa uchaguzi huyo Chacha Heche ndiyo alikuwa anamtafutia kura kwa wajumbe na aliposhinda wakamfanyia sherehe, njaa tu ndiyo ilisababisha huyo mzee avue sare" amesema Mwita.

Mwita Marwa Mwendesha Pikipiki mkazi wa Mtaa wa Nyamisangura amesema" Huo ni ushamba kuvaa sare siyo kosa mbona kuna watu wanavaa sare za timu za michezo za Simba,Yanga na zinginezo na wanachanganyikana , wamemzalilisha tu yule mzee nguo siyo tatizo wewe angalia kazi mambo ya nguo ya mtu aliyoivaa hayakuhusu" amesema Mwita.

James Juma Mkazi wa Mtaa wa Mwangaza mfanyabiashara mjini Tarime amesema" Kumwambia mtu avue nguo aliyoivaa kwasababu anatoka chama ambacho si chako huo ni ubinafsi ,huo siyo utanzania tunaoutaka, watu tueneze upendo tusieneze uchama, Tanzania hatuna ukabila, udini wala uchama siasa imekuja juzi" amesema.

Ghati Marwa muuza Nyanya soko la Rebu amesema"Mtu avae nguo ya CCM au CHADEMA, ACT WAZALENDO, NCCR, CUF na vyama vingine ni sawa tu maana ni mapenzi yake, Chacha hapaswi kuangalia mambo ya vyama yeye aangalie kazi maana hata hiyo nyumba yake anayoijenga watakaoingia mle ni watu mchanganyiko wa CCM ataingia na wa CHADEMA ataingia"amesema Ghati.

Eva James Mkazi wa Mtaa wa Rebu mfanyabiashara wa samaki amesema " Huo ni unyanyapaa mimi ninavyojua kinachotakiwa ni kazi mimi nauza samaki namuuzia yeyote aje amevaa sare ya CCM au CHADEMA mimi nachoangalia ni pesa na siyo sare .

Marwa Ryoba Mkazi wa Mtaa wa Rebu Shuleni amesema" Vyama haviwezi kugawa watu hata kwenye ndoa zetu unakuta mmoja ni CCM na mmoja ni CHADEMA au Chama kingine ukisema umzuie mwenzio kisa utofauti wa Chama unataka afate chama chako mtakosana kwenye ndoa" amesema.

Wananchi wengine wao wamesema kuwa Video Clip ni ya kisiasa jambo ambalo ni la kawaida kwa wanasiasa.

Mariam Mwita mfanyabiashara wa vitunguu soko la Rebu amesema" Mimi hata haya mavyama yalishanishinda , alimwambia avue nguo ni sawa maana moyo wake ndiyo haupendi,mimi sioni ubaya maana ni kero katika moyo wake hataki kuona hiyo sare ambayo siyo ya Chama chake.

"Yule mzee ametii amri ya bosi wake yupo chini yake maana anapokea mshahara baada ya kazi, basi hao wa kijani wampe pesa ili awe anavaa sare zao, kuna watu chama kipo damuni sasa ukiwa kwenye himaya yake lazima utii bila shuruti masharti ya bosi wako" amesema Mariam.

Boniface Marwa mkazi wa Mtaa wa Songambele mfanyabiashara mjini Tarime amesema" Ni mara ngapi tukashuhudia watu wa CCM wakinyanyasa wana CHADEMA lakini huoni wakichukuliwa hatua.mfano Kwenye uchaguzi mkuu 2020 CCM waliwanyanyasa wapinzani kwa kuwatumia vijana wao wa CCM Tarime wakawa wanavamia vijana wa upinzani wanawakamata wanawasondeka kwenye magari.

 "Kisha wanawapeleka ofisi ya CCM wilaya wakapewa vichapo huko ofisi ya CCM wakisha waadhibu wanapiga simu Polisi wanakuja na difenda wanawabeba na kuwapeleka kituo cha Polisi wakati waliowaonea ni CCM lakini kwakuwa Serikali ni ya CCM ndiyo maana CHADEMA wanakosa haki"amesema Boniface Marwa.

Bhoke Chacha amesema"Hakuna udhalilishaji hapo isitoshe wenye matukio ya udhalilishaji ni CCM kwa sababu wana serikali wananyanyasa watu wanavyotaka, Chacha yupo sawa kabisa wewe unaendaje kwa mtu umevaa sare ya chama wakati unajua huyo mtu siyo CCM hizo ni dharau ".

" Ester John amesema" Chacha yupo sawa kila kazi mabosi wana masharti yao, hata serikali imeweka masharti kwa watumishi wake usipoyafuata unawajibishwa na hata kufukuzwa kazi sasa kuna ubaya gani Chacha kuweka masharti kwa mfanyakazi wake mi sioni ubaya.

Amina Ramadhani yeye amesema"Vyama vya upinzani vimekuwa vikinyanyaswa na hao wana CCM hasa viongozi wanadhalilishwa tena hadharani lakini wanafumbiwa macho ,mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu, leo wa kwao kaguswa wanawaka kwani wengine si watu wanavyokuwa wakiwanyanyasa, waanze kuonya wanachama wao ili vyama vingine vijifunze kutoka kwao" amesema Amina.

Katika Wilaya ya Musoma, Jovina Massamo anaripoti kuwa, Mkazi wa Mjini Musoma Jackson Mkono amesema kilichofanyika siyo udhalilishaji.

"Wana CCM ndiyo wanamdhalilisha huyo mzee kwa sababu CHADEMA ni Chama ambacho kimesajiliwa kisheria na kipo kisheria na kinatambulika na sisi kama wanadamu tunawajibu wa kuchagua ni chama gani nakihitaji mimi.

"CCM wajue kutangaza sera zao mzee alikuwa anaambiwa kuvua vazi ,yaani avue utu wa ndani siyo nguo, kuambiwa avue sare inakubalika kisiasa maana ni sehemu mojawapo ya kukieneza chama chake" amesema.

Mkazi wa Mtakuja A Kata ya Mwisenge Fabian Maengella ambae pia ni mwanachama wa Chama wa CCM yeye amesema tukio hilo ni ukikwaji wa haki kwani kila mmoja ana haki ya kupenda chama anachohitaji au dini kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi.

"Tukio hilo lililooneshwa kupitia Video Clip ni kutokukomaa kisiasa kila mtu ana haki ya kupenda chama chochote au dini kwa utaratibu wa katiba yetu kufanya hivyo ni ufinyu wa fikra ya mtu kulingana na uelewa wa halmashauri yake ya kichwa"amesema Maengella.

Julius  Stephano amesema kumekuwa na vitendo vya kiunyanyasaji, uonevu na udhalilishaji vinavyofanywa na wanachama wa vyama vya siasa na sheria haitumiki vilivyo kuhakikisha watu wanawajibishwa hali inayosababisha matukio hayo dhidi ya wanasiasa kuendelea kuwepo.

Julius anaiomba Serikali kusimamia sheria za nchi pasipo kuangalia watenda makosa wanatoka upande gani wa vyama vya siasa, kwa kufanya hivyo jamii itajifunza na vitendo vya ukiukwaji wa haki za Binadamu vitakoma. 

No comments