JOYCE MANG'O AWASHAURI WANAWAKE KUPIMA AFYA MARA KWA MARA
Na Jovina Massano, Bunda.
WANAWAKE Mkoani Mara wameshauriwa kuwa na utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara hususani saratani ya shingo ya kizazi na ya titi ili wapate huduma stahiki kwa wakati pindi watakapogundulika kuwa na vimelea hivyo.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ( NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia Umoja wa wanawake Tanzania (UWT) Bara, Joyce Mang'o alipokuwa akizungumza na wanawake wa UWT Wilayani Bunda.
Joyce amesema hayo baada ya kukutana na Mwenyekiti wa UWT Kata ya Balili Veridiana Mackria aliyeondolewa titi lake moja baada ya kugundulika kuwa na saratani ya titi.
"Niwaombe wanawake wote tuwe na desturi ya kupima afya zetu mara kwa mara ili kujua kama una tatizo upate matibabu ya haraka, Miili yetu ina chembechembe hai nyingi zinazozaliana, hukua, na kufa kwa mpangalio maalum.
"Chembechembe hizi zinapobadilika na kuanza kuzaliana na kukua katika utaratibu ambao sio wa kawaida ndio zinasababisha saratani kwa mujibu wa wataalam wetu wa afya", amesema Joyce.
Sababu ya Joyce kufahamu tatizo la Mwenyekiti huyo ni wakati walipokuwa wakila chakula na kisha kumuona Mwenyekiti huyo wa UWT akiwa amekaa na kutoenda kuchukua chakula.
Joyce alimfuata mama huyo na kumuuliza kwa nini hajumuiki na wenzake kupata chakula, naye alimueleza tatizo lake. Joyce akawajulisha viongozi wenzake na kuanzisha harambee kumchangia fedha za chakula.
Ombi hilo la Mjumbe wa UWT likawagusa wanachama wote na kumchangia mama huyo fedha pamoja na kiongozi mwingine anayeuguliwa na mtoto.
Mjumbe wa Baraza la Umoja wa Wanawake Mkoa wa Mara, Latifa Hamis amesema Saratani ni uvimbe unaojitokeza mahala popote katika mwili wa binadamu.
Amesema uvimbe huo hauna maumivu yoyote mwanzoni na kwamba kiungo chochote chaweza shambuliwa, huku akitolea mfano shingo ya mfuko wa kizazi, Matiti, Ngozi, Koo na njia ya chakula.
"Sisi wanawake tumekuwa wahanga katika hili kwa kuwa muda mwingine tunaletewa vimelea vya Saratani na wenza wetu wasio waaminifu hasa kwenye saratani ya Shingo ya kizazi.
"Tujitahidi kupima katika vituo vyetu vya afya ili tuweze kujikinga na kupata matibabu kwa wakati kwa kuwa sisi ndio walezi wakuu wa familia zetu", amesema Latifa.
Mwenyekiti wa UWT Kata ya Balili Veridiana Mackria amewashukuru viongozi hao kwa kuguswa kwao na kuweza kuwapa faraja kwa kuwachangia fedha kwa kiasi walichokuwa nacho.
" Niligundua tatizo hili Juni, 2022 nilipofika katika hospital ya DDH iliyopo wilayani hapa nikaanzishiwa matibabu, walitoa uvimbe na wakagundua kuwa nina saratani, ilipofika mwezi Agasti nikafanyiwa upasuaji hospitali ya Bugando titi lote likatolewa na hivi sasa ninaendelea vizuri".amesema Veridiana.
Post a Comment