WASOMAJI WAIOMBA DIMA ONLINE KUZIDI KUIBUA HABARI ZA KIJAMII
Na Waandishi Wetu, DIMA ONLINE
WASOMAJI wa DIMA ONLINE Chombo cha Habari cha Mtandaoni kinachoripoti Habari mbalimbali kupitia Blogu ya dimaonline.co.tz, Twitter @dimaonline255 na Instagram dima_onlinenews, wamekipongeza chombo hicho cha Habari kwa kuripoti Habari za Kijamii zikiwemo changamoto za wananchi na makundi ya watu wa hali ya chini.
Wasomaji wamekiomba chombo hicho cha Habari kuendelea kuposti habari za kijamii na kuibua changamoto kwani zikiripotiwa zitasaidia mamlaka husika kuchukua hatua na kuwajibika jambo ambalo litachochea maendeleo ndani ya jamii.
Waandishi wa DIMA ONLINE wamezungumza na baadhi ya wasomaji ili kupata maoni yao ikiwa ni miezi mitatu tangu chombo hicho cha habari kianze rasmi kuripoti habari Septemba, 21, 2022 ambapo katika kipindi cha miezi mitatu jumla ya habari 151 zikiwemo makala zimepostiwa.
Waandishi wa Habari wamezungumza na wasomaji kufahamu kwa kipindi cha miezi mitatu wao kama wasomaji je wamejifunza nini au wameelimika vipi kupitia habari mbalimbali zilizoripotiwa?, je ni mapungufu yapi wameyaona na nini ushauri wao katika kuboresha DIMA ONLINE ?, miongoni mwao walikuwa na haya ya kusema;
Nashon Kennedy msomaji wa DIMA ONLINE na Mwandishi wa Habari kutoka Mkoani Mwanza amesema " Hakika nimejifunza vitu vingi! Kubwa ni uandishi wa habari za kijamii unaoibua changamoto na makundi ya hali ya chini.
" Wakiwemo wazee ikiwemo habari ya Mzee Kichonge ambaye baada ya kufanya mahojiano naye alifariki! Mungu ailaze pema roho yake!. Stori ile imegusa watu wengi yaani hongera za kumwaga. Pia nashauri DIMA ONLINE ianzishe TV Online kuwe na mahojiano ya online kwa wadau na wananchi wa kawaida ili kuwa na vitu vyote Habari za Blogu na Online TV" amesema Nashon.
Christopher Masanja Mkazi wa Mkoa wa Dodoma amesema" Mmepiga hatua nzuri, kikubwa ni kuendeleza juhudi, ushirikiano na wananchi ili kupata taarifa nyingi za kuripoti, hii itaifanya Blogu itembelewe na watu mara kwa mara" amesema Christopher.
Diwani wa Kata ya Kwangwa Wilaya ya Musoma Mkoani Mara, Fredrick Charles Mganga kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amesema DIMA ONLINE niwafuatiliaji wazuri wa matukio na wanafuatilia kuhakiki ukweli wa tukio na uwepo wa tukio.
"Wanaripoti tukio kama lilivyo bila kumlinda mwenye tukio kama tunavyoona baadhi ya vyombo vya habari vinavoiogopa Serikali au viongozi wa Serikali, na sio wapenda rushwa ili kupeperusha ama kuyeyusha habari,
hawana gharama katika kuchukua na kutoa habari na niwatoa huduma wazuri"amesema Fredrick.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Kata ya Turwa Wilaya ya Tarime Mkoani Mara, Sheby Timoro amesema " Mwenyezi Mungu aibariki DIMA tunashukuru kuanzishwa kwa chombo hiki cha Habari kwasababu kuna vitu vingi vilikuwa vimejificha lakini DIMA inavichunguza na kuibua hadi watu wanaviona.
" Endeleeni kuibua habari zilizojificha, pia ipanue wigo mikoa yote, najua mwanzo ni mgumu maana bado ni chombo kimya ila naamini huko mbeleni mtaifikia mikoa yote nchini hakika DIMA ni Nuru ya Jamii." Amesema Sheby.
Annastazia Paul Mwandishi wa Habari kutoka Mkoani Simiyu amesema "Ni mwanzo mzuri nashauri pia habari za michezo ziongezwe maana kuna watu wanapenda michezo" amesema.
Marwa Charles kutoka Wilaya ya Rorya Mkoani Mara amesema" Nawapongeza sana endeleeni kuchapa kazi, kubwa zaidi endeleeni kuzingatia misingi, miiko, maadili na uweledi wa taaluma ya habari" amesema Marwa.
Hellena Magabe Mwandishi wa Habari kutoka Mkoani Mara amesema " DIMA ONLINE iko vizuri sana habari hizo ni nyingi kwa kipindi cha miezi mitatu imejitahidi sana kaza buti" amesema Hellena.
Deus kutoka Mkoani Dar es Salaam amesema" Hongera sana kazi ni nzuri DIMA iendelee kusonga, habari zinagusa jamii moja kwa moja siyo udaku tunaomba iendelee hivi hivi"amesema Deus.
Uongozi wa DIMA ONLINE unawashukuru sana wasomaji wote ndani ya nchi na nje ya nchi kwa kutenga muda wao na kutembelea mitandao ya chombo hiki, na unawaomba waendelee kusoma habari bila kuchoka.
Uongozi umepokea kwa moyo wa dhati maoni yote yaliyotolewa na wasomaji pamoja na pongezi na inaahidi kuendelea kuripoti habari mbalimbali zikiwemo za kijamii.
Uongozi wa DIMA ONLINE unawashukuru sana Waandishi wa Habari wa Chombo hiki kwa moyo wao wakipekee katika upashaji Habari bila kuwasahau baadhi ya Maafisa Habari kutoka baadhi ya Wizara za Serikali ikiwemo Wizara ya Afya wanaoshirikiana na chombo hiki katika upashaji wa habari.
Katika kipindi cha miezi mitatu DIMA ONLINE imeposti habari zipatazo 151, kundi linaloongoza kwa habari nyingi ni kundi la Afya likiwa na habari 28 likifuatiwa na kundi la Habari Mchanganyiko habari 25 na Siasa habari 17.
Makundi hayo ya Habari ni Habari za Kilimo ambazo zimepostiwa habari 9, Maliasili/Utalii 9, Habari Mchanganyiko 25, Maji 4, Siasa 17, Afya 28, Biashara/Uchumi 11, Barabara 4, Polisi 5, Dini 4, , Elimu 14, Mifugo 10, Mila/Utamaduni 2, Teknolojia/Ubunifu 2, Watoto 2, Mazingira 2 na Michezo habari 3.
Jumla ya makala 17 zimepostiwa zikiwa kwenywe kundi la makala na makundi mengine. Katika makundi hayo ya Habari, Habari za Kitaifa ni 58, Habari za Kimkoa ni 67 na Habari za Kimataifa ni 9.
Mikoa iliyoripotiwa habari ni Mara Habari 59, Dodoma 09, Mwanza 10, Mbeya 01, Manyara 01, Arusha 03, Shinyanga 07, Dar es Salaam 19, Simiyu 18, Kagera 06, Tanga 01, Pwani 03, Lukwa 01, Lindi 01, Kigoma 02 na Zanzibar 01.
Habari zilizoripotiwa kutoka nje ya nchi ni Marekani 03, Ubelgiji 02, Kenya 01, Rwanda 01, Katari 01 na Afrika Kusini 01. Hata hivyo baadhi ya habari katika makundi hayo ya habari kama vile habari za afya, Mchanganyiko n.k zimepostiwa katika kundi la Kitaifa na kimataifa na hivyo habari chache kupostiwa katika makundi husika kutokana na uzito wa habari uliopelekea zipostiwe Kitaifa na Kimataifa.
Hata hivyo kutokana na kwamba chombo hiki bado ni kichanga hakijafanikiwa kuripoti habari kutoka Mikoa yote ya Tanzania hivyo juhudi zinaendelea kuhakikisha DIMA ONLINE inaifikia mikoa yote kihabari.
Pia uongozi unawashukuru wananchi, wadau na viongozi mbalimbali wakiwemo wa Serikali kwa ushirikiano wao kuhakikisha DIMA ONLINE inatimiza wajibu wake kihabari.
DIMA ONLINE inawatakia kheri na mafanikio tele katika mwaka mpya wa 2023. DIMA ONLINE "Nuru ya Jamii.
Post a Comment