HEADER AD

HEADER AD

MADIWANI WAMFUKUZA KAZI AFISA UGAVI, WENGINE KUKATWA MSHAHARA

Na Daniel Limbe, Kakonko

KATIKA kukabiliana na mmomonyoko wa maadili kwa Watumishi wa Umma nchini, Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Mkoani Kigoma limeazimia kufukuzwa kazi Ofisa Ugavi msaidizi, Msafiri Hiza, huku Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dk.Edward Malima, akishushwa cheo pamoja na mshahara wake.

Uamuzi huo umefikiwa juzi kwenye kikao cha dharura kilichoketi kwaajili ya kutoa uamuzi wa ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Kamati maalumu ya mkoa huo ambayo ilibainisha makosa mbalimbali ya ukiukwaji wa maadili ya utumishi ikiwemo ubadhilifu wa fedha za umma kinyume cha sheria za nchi.

Wakitoa uamuzi, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,Fidel Nderego, amesema kutokana na uchunguzi wa Kamati hiyo, Baraza hilo limeazimia hatua kali zichukuliwa ikiwa ni pamoja na kumfukuza kazi ofisa ugavi msaidizi.

             Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko,Fidel Nderego,akitoa msimamo wa Baraza la Madiwani

"Mbali na Msafiri Hiza, pia Mganga mkuu wa wilaya Dk. Malima naye ashushwe cheo pamoja na mshahara wake...ofisa ugavi daraja la pili, Linus Kagoma, atakatwe mshahara wake kwa asilimia 15 kila mwezi kwa kipindi cha miaka mitatu mfurulizo,pamoja na Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari, Sebastian Bukombe, naye akatwe asilimia 15 ya mshahara wake kwa kipindi cha miaka mitatu"amesema Nderego.

Licha ya kutotajwa kiasi cha fedha kilichotafunwa na watumishi hao, Nderego amesema uamuzi huo unalenga  kuziba mianya ya wizi wa pesa za miradi ya maendeleo ya wananchi na kwamba halmashauri hiyo siyo shamba la bibi.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Kakonko, Saamoja Sadock, mbali na kulipongeza Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kwa uamuzi wake, amewatahadhalisha watumishi wengine wenye lengo la kuhujumu fedha zinazotolewa na Serikali ya CCM, kwamba wao kama Chama hawatokubali kufumbia macho vitendo hivyo.

"Watumishi wenye maadili tunawapenda lakini wanaohujumu fedha zinazotolewa na Rais Samia kamwe hatuto wafumbia macho...lazima fedha ziende kwenye miradi iliyokusudiwa ili kupunguza adha kwa wananchi...CCM ndiyo tunaoisimamia Serikali kwahiyo mambo yanapoharibika hasira za wananchi zinakigharimu chama kwenye sanduku la kura" amesema Saamoja.

Ameipongeza Tume iliyoundwa na mkoa wa Kigoma kufanya uchunguzi wa tuhuma za ubadhilifu wa fedha kwenye Halmashauri ya Kakonko, kwani imesaidia Madiwani hao kuchukua hatua stahiki.

Nje ya kikao hicho, baadhi ya wananchi wa Wilaya hiyo, Adellina Chabilonda na Andrea Jonathan, wamesema hatua iliyofikiwa na Madiwani hao siyo ya kupongezwa kwa madai kwamba watumishi hao walipaswa kutimuliwa kazi.

Kadhalika wamedai uamuzi huo wa Madiwani bado unaipa nafasi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (TAKUKURU) kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao kwaajili ya hatua zaidi za kisheria.

                       

No comments