HEADER AD

HEADER AD

POLISI WALAUMIWA KUTOFIKA KUCHUKUA KIELELEZO NG'OMBE WANAODAIWA KUPIGWA RISASI


Na Dinna Maningo, Tarime

WANANCHI wa Kijiji cha Kegonga Kata ya Nyanungu Wilaya ya Tarime Mkoani Mara, wamelilaumu Jeshi la Polisi Wilaya ya Polisi Nyamwaga na kituo cha Polisi Kegonga kwa kutofika kuchukua kielelezo cha Ng'ombe wanne waliokufa wakidaiwa kupigwa risasi na Askari wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Wakizungumza na Waandishi wa Habari eneo linalodaiwa Ng'ombe walikuwa wakichunga na kupigwa risasi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kegonga Warioba Mogoyo amesema tukio hilo lilitokea Ijumaa, Desemba,2,2022 katika kitongoji cha Gwihema.

Warioba amesema Ng'ombe sita wa Bhoke Matiko walikuwa kwenye malisho mlimani eneo lenye mgogoro ambalo wananchi wanasema ni lao na Hifadhi inasema ni lao zilizokuwa zikichungwa na watoto.

 
   Mwenyekiti wa Kijiji cha Kegonga Warioba Mogoyo akizungumza katika eneo la tukio

Amesema baada ya kupata taarifa za Ng'ombe wanne kati ya sita kupigwa risasi na askari wa hifadhi kituo cha Kenyangagha, alifika eneo la tukio na kushuhudia ng'ombe wawili wakiwa wamekufa papohapo na mmoja alifia nyumbani na mwingine kutoonekana anayedaiwa kuchukuliwa na askari wa hifadhi.

Mwenyekiti huyo amesema baada ya tukio hilo alipiga simu kituo cha Polisi Kegonga lakini hakuna askari aliyefika eneo la tukio, ndipo alipoongozana yeye pamoja na wahanga ambao mifugo yao ilipigwa risasi kwenda kituo hicho cha Polisi kutoa taarifa.

              Kituo cha Polisi Kegonga

"Tukio lilitokea tarehe 2 siku ya ijumaa saa sita mchana, nilipata taarifa saa saba nikawasiliana na Mwenyekiti wa Kitongoji kulikotokea tukio ,nikaondoka hadi eneo la tukio nikashuhudia kitendo kilichofanywa na askari gemu, nikampigia simu Diwani nikamweleza kilichotokea nikampigia simu OCS wa kituo cha Polisi Kegonga lakini Polisi hawakufika.

"Majira ya saa moja nikaongozana na wahaga hadi kituo cha Polisi tulimkuta OCS tukamweleza tukio zima akiwa kama mlinda amani na usalama wa raia na mali zake na akiwa kama Polisi Kata, akatuambia taarifa hii itabidi mje kesho saizi muda umeenda tukaambiwa tuondoke turudi kesho yake ambayo ilikuwa siku ya jumamosi" amesema.

Mwenyekiti huyo ameongeza" Siku iliyofuata tulienda nikiwa na wahanga na Diwani tulikuwa naye jarada la kesi likafunguliwa ilikuwa siku ya Jumamosi.

            Ng'ombe anayedaiwa kufa Baada ya kupigwa risasi

"Viongozi wa Serikali wanakuja wanaishia Tarime mjini na Musoma hawafiki kwenye eneo la tukio hawazungumzi na wananchi, hizo tume zinazoundwa zikimaliza kazi zao wakienda ni jumla hawarudi kutupatia majibu"amesema Warioba.

Mwenyekiti huyo amesema eneo hilo ndilo wafugaji wanalitumia katika maliso ya mifugo ambapo pembeni yake kuna kisima ambacho watu huchota maji na mifugo kunywa maji pamoja na makazi ya watu.

                   Msichana akichota maji kwenye kisima cha asili kilichopo karibu na eneo linalodaiwa kuwa ni la hifadhi

" Askari wa SENAPA walitoka kambini kwao na gari wakavamia kwenye mlima mifugo ikiwa inachunga wakapiga risasi ovyo zikawashtua watu wakawafukuza huku wakirusha risasi kiasi kwamba walikuwa wamedhamilia kuuwa, watu wakakimbia wakauwa mifugo kwa risasi.

Warioba amesema migorogoro kati ya wananchi na hifadhi ya Serengeti kuhusu mipaka imekuwa ni mateso kwao huku baadhi yao wakipotelea hifadhini,wengine kuuliwa kwa kupigwa risasi ,wengine kupata vilema ,mazao kufekwa, kutaifishwa mifugo na mingine kuuliwa kwa kupigwa risasi hali ambayo imesbabisha umaskini kwa baadhi ya familia.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kwihema Marwa Nyamhanga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo la Ng'ombe wanne kupigwa risasi kwenye Kitongoji chake  huku mmoja akidaiwa kuchukuliwa na askari wa hifadhi.

        Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kwihema Marwa Nyamhanga

Bhoke Matiko Mwenye Ng'ombe waliopigwa risasi amesema ng'ombe hao walikuwa wakichungwa na watoto na alipata taarifa akiwa nyumbani, alipofika alishuhudia ng'ombe watatu wakiwa wamepigwa risasi huku mmoja kutojulikana alikopelekwa.

"Nina Ng'ombe sita, wanne wamewauwa wamebaki Ng'ombe wawili, ng'ombe mmoja aliyeuliwa ameacha ndama mdogo sijui ataishije na alikuwa anasaidia maziwa tunampatia baba hawezi kula nyama ni maziwa tu ,ng'ombe kafa hakuna ng'ombe mwingine anayenyonyesha ndama.

                 Ndama

" Baba yangu ni mzee ana miaka 106 atateseka sana wamebaki ng'ombe wawili wasiotoa maziwa, hao ng'ombe walikuwa wanatusaidia kwenye shughuli za kilimo sasa hatuna ng'ombe wa kulimia shamba , TANAPA imetupa umaskini, mifugo haijui kitu wameiuwa bure" amesema.

                 Mzee Ernest 

Mkazi wa Kijiji hicho Marwa Magarya ameilaumu Serikali kwa kushindwa kuumaliza mgogoro huo licha ya tume mbalimbali kuundwa pindi yanapotokea matukio ya mauwaji yanayotendwa na askari wanyamapori ambapo chanzo ni migogoro ya mipaka.

                     Marwa Magarya

"Matukio yanayokuwa yanatokea hapa kijijini taarifa zimekuwa zikitumwa kila mara lakini utatuzi hakuna, Serikali ilishakaa kimya ,tunasikia tume zimeundwa lakini hatuzioni zikija kijijini kuongea na wanachi wala kutuletea mrejesho wa ripoti zao.

" Mawaziri wanaohusika na Wizara ya Ardhi na ya Maliasili waje Kegonga watueleze ukweli, Serikali ije itutamkie wazi kwamba eneo siyo letu tujue isikae kimya" amesema Marwa.

Marwa Mariba mwenye umri wa miaka (14) mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Kegonga aliyekuwa akichunga mifugo yeye na ndugu yake  Elisha  Ernest amesema wakati wakichunga mifugo alikuwa yeye na watoto wenzake.

                Marwa Mariba

"Nilikuwa nachunga Serikali walikuja wakanifukuza walikuwa na bunduki wakaanza kupiga risasi ng'ombe, nami nikajificha kwenye ng'ombe ndio risasi ikampata ng'ombe nikakimbia kwenda kujificha kwenye miji watu wakaja tukaenda kuangalia ng'ombe nikakuta wamekufa mmoja alikuwa bado hajafa wakambeba akafia nyumbani" amesema Marwa.

Elisha Ernest mwenye umri wa miaka (10) Mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Kegonga amesema;

                      Elisha Ernest

"Walitaka kutupiga risasi mimi nikalala chini ile risasi ikampiga ng'ombe ningekuwa nimesimama ingenipata mimi, walikuwa watu watatu wakiwa wamevaa sare za maaskari wa hifadhi ,walikuwa wamesimama pale chini na sisi tulikuwa hapa mlimani wakawa wanapiga risasi kuja huku tulipokuwa sisi.

"Wakati tunachunga tulikuwa sisi watoto hapakuwa na watu wakubwa wale wenzangu walikuwa wanachunga pale wao hawakupigwa tulilengwa sisi, tulienda kuchunga saa tano muda zilipopigwa risasi sijui ilikuwa saa ngapi maana mimi sikuwa na simu ila wanasema ilikuwa muda wa saa sita wakati risasi zinapigwa"amesema Elisha.

Diwani wa Kata ya Nyanungu Tiboche  Richard amesema baada ya kupata taarifa hizo alipiga simu polisi lakini hawakufika eneo la tukio ili kuchukua vielelezo vya ng'ombe waliopigwa risasi jambo ambalo limesababisha ushahidi kupotea baada ya wanachi kusubiri polisi bila mafanikio na hivyo kuamua kujitwalia nyama kama kitoweo.

                 Diwani Tiboche Richard akiwa ameshika risasi iliyokutwa kwenye mwili wa ng'ombe

"Nilifanya juhudi ya kumpigia simu OCS, OCD kama msimamizi lakini hakufika, nikampigia Dc akasema yeye hausiki hivyo niiambie polisi, niliwafahamisha lakini hawakufika wakaja usiku nyumbani kwa Mwenyekiti wakaondoka hadi navyoongea hakuna polisi aliyefika eneo la tukio kuja kuona vizibiti.

"Ng'ombe mmoja aliyechinjwa alikutwa na risasi ndani ya mwili na risasi ndio hii hapa, hizi risasi je zingempata mtu! hapa kuna kisima watu wanachota maji, wanafua nguo ,mifugo inakunywa maji hapa.

"Chama changu cha CCM wakati wa kampeni kiliwaambia wananchi kuwa wakichagua viongozi wa CCM watatekeleza na kutatua kero za wananchi na hifadhi lakini utatuzi hakuna" amesema Tiboche.

           Mifugo ikinywa maji pembeni kukiwa na watoto wadogo karibu na eneo walikofia ng'ombe waliodaiwa kupigwa risasi na Askari wa SENAPA.

Ameongeza kuwa tume zimeshafika kufuatilia lakini hazijawahi kuwa na matokeo chanya zaidi ya migogoro kuongezeka  na hazirejeshi majibu kwa wananchi hivyo anakiomba Chama cha Mapinduzi (CCM) kinachoisimamia Serikali kiwasemea na kuwatetea wananchi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyandage Kata ya Nyanungu Mwita Kiha amesema Novemba,2022 Askari wa Hifadhi ya Serengeti waliuwa ng'ombe mmoja kwa kumpiga risasi, wakafeka migomba, mtama, mahindi na kung'oa mihogo katika Kitongoji cha Nyandage, Nyarususuni na Ngori.

Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Izumbe Msindai amesema Askari walikuwa wakitekeleza majukumu yao ambapo walikamata ng'ombe walioingia hifadhini lakini kundi la watu liliwavamia na kuwalazimu kujihami kwa kupiga risasi hewani kuwatawanya na kwamba hakuna mifugo iliyopigwa risasi na kama imepigwa risasi ni kwa bahati mbaya.

DIMA ONLINE ilipomuuliza kuwa kuna risasi inayodaiwa kupatikana kwenye ndani ya mwili wa Ng'ombe aliyedaiwa kupigwa risasi na Askari wa Hifadhi amesema;

                Risasi inayodaiwa kukutwa kwenye mwili wa Ng'ombe 

"Lile ni eneo la Hifadhi hiyo mifugo ilikuwa imekamatwa na askari kundi la watu likawavamia, askari walitumia nguvu kujihami kwa kupiga risasi hewani ili kuwatawanya, hawakuwa na nia ya kumlenga mtu wala mifugo kama mifugo imepigwa risasi imetokea kwa bahati mbaya wakati wakiwa wanajihami.

"Ni mara ngapi tunakamata mifugo alafu hii ndiyo ipigwe risasi? hii imetokea baada ya askari kujihami, hilo eneo ni la hifadhi tunawaomba wanasiasa wawaambie ukweli wananchi wao "amesema Izumbe.

Alipoulizwa kuwa kama mifugo hiyo inadaiwa kuwa katika eneo la Hifadhi je na nyumba zilizojengwa juu ya mlima jirani na zilikofia ng'ombe napo ni eneo la Hifadhi ? amesema;

         Wananchi wakitafuta risasi eneo lililodaiwa Ng'ombe kufa baada ya kupigwa risasi

"Sijui kama kuna nyumba zimejengwa kwenye hilo eneo nitafika niangalie, wananchi wanajua mpaka wa Hifadhi alama za mipaka zimekuwa zikiwekwa wanaziondoa wakisema ni eneo lao hawataki kukubali .

Mhifadhi huyo amesema eneo hilo lilitengwa na Serikali kuwa la hifadhi tangu mwaka 1968 na mipaka ikawekwa lakini wananchi wamekuwa hawakubaliani na mipaka hiyo iliyowekwa na Serikali.

"Eneo hilo lilitengwa na Serikali tangu 1968 kuwa hifadhi tafuta GN usome mpaka wa hifadhi imeonesha kila kitu, wanachi tumekuwa tukiwaita hata kwenye vikao hawashiriki ,eneo ambalo wanaling'ang'ania ni eneo ambalo mwekezaji angewekeza hoteli ya kitalii wangenufaika lakini wanaling'ang'ania eneo hilo.

          Eneo lenye mgogoro 

Amewaomba wanasiasa wawaambie ukweli wananchi wao kuhusu mipaka ya hifadhi na wasitumie maeneo hayo kuomba kura kwamba wakipewa Kura watawasaidia kuyarejesha maeneo hayo kwa wananchi.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Polisi Tarime Rorya, ACP Geofrey Sarakikya amesema Polisi hawakufika eneo la tukio kwakuwa eno hilo ni la hifadhi ili waingie mpaka wapate kibali kutoka hifadhi ya Serengeti na kwamba wameshawasiliana na uongozi wa hifadhi ili kufika kwenye eneo hilo lililodaiwa ng'ombe kufa  kwa kupigwa risasi na askari wa hifadhi.

          RPC Geofrey Sarakikya

"Sisi hatujui mipaka ya Hifadhi na eneo hilo tunaelezwa ni la hifadhi hatujui kama lina wanyama wakali ili kwenda huko lazima tuwe na wenyeji wa hifadhi watupeleke kwenye eneo hilo, ng'ombe walikuwa nane wakichungwa na watu wawili mmoja alikuwa na ng'ombe sita wakafa wanne akarudi na wawili mwingine alikuwa na wawili wakarudi wote.

"Hao wananchi wamefika polisi jana jioni (Jumamosi) kutoa taarifa na kufungua jarada la kesi, na tayari wameshapoteza ushahidi kwa kuwatoa eneo la tukio wamewachinja wakagawana nyama.

         Ng'ombe aliyedaiwa kupigwa risasi

Ameongeza "Taarifa hutolewa na mlengwa mwenyewe ambaye ndiye anaandikisha maelezo na kesi inafunguliwa na siyo watu wengine ,Mwenyekiti alitoa taarifa lakini siyo mwenye kesi, Polisi baada ya kupata taarifa wamefika kijijini kufuatilia hivyo uchunguzi bado unaendelea"amesema Sarakikya.

>>>Jeshi la Polisi lipo kwa lengo la kuwahakikishia Wananchi usalama wao na mali zao, kudumisha amani na utulivu katika jamii, pia kuzuia, kubaini na kupambana na uhalifu.

>>> Kwa miaka kadhaa Vijiji 8 vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA ) vimekuwa na migogoro ya mipaka na Hifadhi ambavyo ni Kijiji cha Kenyamsabi, Masanga na Masurura vilivyopo kata ya Gorong'a, kijiji cha Karakatonga, Gibaso na Nyabirongo kata ya Kwihancha, na kijiji cha Nyandage na Kegonga kata ya Nyanungu.


Wananchi wakiwa wamembeba Ng'ombe aliyedaiwa kupigwa risasi wakimpeleka nyumbani

                           Nyama ya ng'ombe aliyechinjwa baada ya kupigwa risasi ikiwa imetunzwa kwa kutundikwa  ndani ya nyumba kama kitoweo






        Barabara yenye mawe inavyokwenda hadi hifadhini

            Eneo lenye mgogoro










No comments