SERIKALI YASIKIA KILIO CHA MABODABODA TARIME
Na Dinna Maningo, Tarime
SERIKALI imesogeza huduma ya leseni za udereva Wilayani Tarime kwa kuleta mtambo wa kutengeneza leseni ambapo awali wananchi walilazimika kutumia gharama za usafiri kwenda kufuata leseni mjini Musoma mkoani Mara.
Wakizungumza na DIMA ONLINE, Madereva wa Pikipiki Wilayani Tarime wameipongeza Serikali kwa kusikia kilio chao kwa kile walichoeleza kuwa, baadhi ya waendesha pikipiki walishindwa kumudu gharama za usafiri kwenda kufuata leseni Musoma jambo ambalo limesababisha wengi wao kuendesha pikipiki bila kuwa na leseni ya udereva.
Marwa Chacha mkazi wa Rebu amesema kuletwa kwa mtambo wa kutengeneza leseni utachochea waendesha pikipiki kupata leseni kwakuwa ni karibu hawatagharamika tena kuzifuata Musoma.
"Kuletwa mtambo Tarime wa kutengeneza leseni waendesha pikipiki watashawishika kwenda chuo cha udereva ili wapate vyeti kisha leseni ya udereva jambo ambalo litasaidia kupunguza ajali za barabarani kwakuwa wengi watakuwa wamepata elimu ya udereva maana ili upewe leseni ni lazima uwe umejifunza udereva "amesema Marwa.
Katibu wa Waendesha Pikipiki (Bodaboda) Wilaya ya Tarime, Dikson Christopher amesema" Tunaishukuru serikali yetu kwa kusikia kilio chetu kwa kuleta mtambo wa kutengeneza leseni za udereva hapahapa Tarime hatutoenda tena kuzifuata Musoma.
"Kabla ya kuletwa huu mtambo tulisumbuka sana kufuatilia leseni Musoma, unatumia nauli ukifika unakuta foleni unakosa huduma unaambiwa uje kesho, inabidi ulale gesti au kama huna pesa urudi Tarime kujipanga upya, watu wana vyeti vya udereva lakini leseni ikawa shida, tunaishukuru serikali kutukumbuka."amesema Dikson.
Mwenyekiti wa Waendesha Pikipiki Wilaya ya Tarime Joseph James amesema" Mimi mwenyewe nilitumia zaidi ya 280,000 kufuatilia leseni ya Tsh 40,000, tunaishukuru serikali kwa kuleta mtambo hapa Tarime nina imani waendesha pikipiki wengi watapata leseni kwakuwa wamepunguziwa gharama za kufuata Musoma"amesema Joseph.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Tarime, Sadru Kamugisha amesema huduma ya leseni ya udereva imeanza kutolewa Wilayani humo tangu mwezi uliopita, gharama yake ni 70,000 kwa miaka mitano ambapo awali ilikuwa 40,000 kwa miaka mitatu.
Sadru amewasisitiza madereva wa pikipiki kuchangamkia leseni pamoja na madereva wengine wa vyombo vya moto na ili wapate lazima wafuate vigezo vinavyohitajika vya kupata leseni.
Amesema mwombaji wa leseni kwa mara ya kwanza anatakiwa awe amehudhuria mafunzo katika chuo chochote kinachofahamika na kupewa cheti, awe na umri unaozidi miaka 18 kwa ajili ya gari na umri wa miaka16 na kuendelea kwa ajili ya pikipiki.
"Awe na Leseni ya kujifunzia / ya muda ya udereva, awe amelipa ada ya kufanyiwa majaribio GRR, awe na cheti cha kupimwa macho, awe amepeleka maombi kwenye ofisi ya Polisi wa uslaama barabarani kwa ajili ya kufanyiwa majaribio.
"Aende ofisi za polisi wa usalama barabarani akiwa na gari au pikipiki kwa ajili ya kufanyiwa majaribio, baada ya mwombaji kufanyiwa majaribio anaweza kuruhusiwa kuendesha pikipiki na magari madogo" amesema Sadru.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Polisi Tarime Rorya SSP Denis Kunyanja amesema serikali imeweka sheria zake na ili mfanyabiashara awe halali anatakiwa awe na vigezo vinavyotambulika ikiwemo leseni ya udereva.
>>>Rejea
Mara kadhaa waendesha Pikipiki wilayani Tarime wamekuwa wakiiomba serikali kuwasogezea karibu huduma ya leseni ya udereva, malalamiko waliyokuwa wakiyatoa kupitia vikao mbalimbali na Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Tarime na Mkoa wa Polisi Tarime Rorya.
Pia Mwezi Mei, 2022 Waendesha Pikipiki na Bajaji wakiwa kwenye mafunzo ya Urasimishaji wa Biashara yaliyotolewa na Taasisi ya Serikali chini ya Ofisi ya Rais -Ikulu kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) yaliyotolewa na wakufunzi Zabron Makoye na Joseph Timanye, Bodaboda walisema umbali uliopo wa kufuata leseni Musoma umekuwa ni adha kwao .
Walisema umbali huo ni chanzo cha madereva wengi kutokuwa na leseni kwakuwa baadhi wameshindwa kumudu gharama za usafiri na malazi huku wengine waliokwisha kulipa fedha ili kupata leseni wakizisotea kwa zaidi ya mwaka bila mafanikio.
Waendesha pikipiki waliiomba serikali kuwasogezea huduma karibu ili leseni hizo zitolewe Wilayani Tarime kwani kwa kufanya hivyo itawezesha madereva wengi kuwa na Leseni.
Dereva wa Pikipiki (Bodaboda) Boniface James alisema "Ili upate leseni ni lazima ufunge safari kwenda mkoani TRA Musoma lazima uwe na nauli, uwe na pesa ya kula, uwe na pesa ya kulala gesti maana ukifika kule huduma huipati kwa siku hiyo, wakati mwingine foleni kubwa unajikuta umeingia gharama nyingi, hiyo hali inawakwamisha mabodaboda wengine maana ni kero" alisema Boniface.
Ally Meremo alisema licha ya baadhi kuwa wamelipia fedha za leseni lakini wamekuwa wakipigwa danadana "Mtu unafuata taratibu zote unalipia Leseni lakini unamaliza mwaka mzima hujapewa ukifuatilia ni mizunguko tu utaambiwa subiri siku fulani ukienda bado.
" Au unaambiwa mtambo ni mbovu haufanyi kazi na umetumia gharama za usafiri umelala gesti wengine wanatoka vijijini wametumia nauli kubwa kufika Tarime bado aende Musoma ni pesa nyingi unajikuta unatumia zaidi ya 50,000 kama gharama za usafiri lakini unafika bado unazungushwa"alisema Meremo.
Chacha Marwa aliiomba serikali kusogeza huduma karibu badala ya kuifuata mjini Musoma "Upatikanaji wa leseni umekuwa ni mgumu umelipia fedha Tsh.70,000 lakini ili uipate utasota sana.
"Hali hii imesababisha baadhi yao watumie njia za mkato kupata leseni na ujue njia za mkato zina madhara yake utagharamika pesa nyingi hata 150,000- 300,000 kuipata leseni sasa wengine hizo gharama hawana, mtatulaumu sana kuwa hatuna leseni lakini upatikanaji wake ndio kikwazo"alisema Chacha.
Kamanda wa waendesha pikipiki ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha Wamachinga wilaya ya Tarime Juma Range alisema utaratibu wa kupata leseni ni mgumu .
"Taratibu za kupata leseni kwa mabodaboda ni ngumu watu wameshapatiwa mafunzo ya udereva lakini leseni mpaka Musoma ukienda huko ni foleni unakaa hadi siku mbili hupati tunaomba mtambo wa kutengeneza leseni uletwe Tarime/Rorya ukizingiatia ni mkoa wa Polisi.
Afisa Biashara wa Halmashauri ya Mji Tarime Seleman Dawood alisema wanafanya mazungumzo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuona uwezekano wa kusogeza huduma hiyo Tarime kwakuwa imekuwa ni kikwazo kwa waendesha pikipiki na kusababisha madereva kutokuwa na leseni.
"Tunafanya mazungumzo na TRA hata TIN namba awali ilikuwa inatolewa Musoma watu wa Tarime walilazimika kuifuata Musoma lakini watu walilakamika wakaomba huduma isogezwe Tarime, serikali ikasikiliza kilio cha wananchi na huduma hiyo sasa inapatikana ofisi za TRA Tarime, kwahiyo na hili la leseni tunalishughulikia"alisema Seleman.
Akitoa mafunzo ya urasimishaji wa biashara kwa waendesha pikipiki na Bajaji Joseph Timanye kutoka MKURABITA alitaja mambo muhimu ambayo wanapaswa kuzingatiwa katika urasimishaji wa biashara ikiwa ni pamoja na kuzingatia taratibu za biashara na miiko ya biashara.
"Mnatakiwa kurasimisha biashara zenu za bodaboda na bajaji uzingatie taratibu za sheria na miiko ya biashara, biashara yako isajiliwe uwe na leseni, dereva apate mafunzo ya udereva na kupata leseni halali.
"Tumeongea na Halmashauri na Jeshi la Polisi kwa wale ambao hawajapata mafunzo ya udereva wakusanywe wapatiwe mafunzo kwa pamoja, dereva anatakiwa kuwa kwenye chama kilichosajiliwa na kutambulika" alisema Joseph.
Post a Comment