HEADER AD

HEADER AD

RAIS SAMIA AOMBWA KUTEMBELEA KIKUNDI CHA WASICHANA CHA UMOJA


Na Nashon Kennedy, Mwanza

WASICHANA wa Kikundi cha Umoja kilichopo Wilayani Nyamagana jijini Mwanza wamemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu kukitembelea kikundi chao ili kujionea shughuli za ujasiriamali wanazozifanya pamoja na changamoto zinazokikabili kikundi.

Kikundi hicho kinafadhiliwa na mradi wa FIKIA+ kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani chini ya Mfuko wa Rais wa Dharura wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC) na Shirika la kimataifa la ICA.

Ombi hilo limetolewa kupitia risala yao iliyosomwa na Christina Jackson  Desemba, 22, 2022, mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya UKIMWI, Kifua Kikuu, Dawa za Kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza wakati walipotembelea miradi inayosimamiwa na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC) lilichopo mkoani Mwanza.

Mradi mwingine uliotembelewa ni mradi wa FIKIA+ unaotekelezwa na ICAP katika halmashauri zote nane (8) mkoani Mwanza, mradi unaolenga kuanzisha kwa haraka dawa za kufubaza VVU, kuimarisha mwendelezo wa matibabu na kufubaza virusi miongoni mwa watu wanaoishi na VVU. 

       Kushoto ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la ICAP - Tanzania Haruka Maruyana, anayepiga makofi ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge Dkt. Alice Kaijage, aliyesimama  kulia ni Mbunge wa Nyamagana Stanslaus Mabula wakiwa na Wajumbe wa Kamati katika kituo hicho.

Mradi wa FIKIA+  unalenga kuimarisha huduma za kuzuia maambukizi mapya kama vile tohara kwa wanaume, huduma zinazowalenga mabinti waliofikia umri wa balehe (DREAMS), tiba-kinga dhidi ya VVU (PrEP), na upatikanaji wa kondomu ili kuendelea kudhibiti janga la VVU  kwa walio katika  hatari zaidi.

Mmoja wa wanakikundi hicho Irene John(22) mhitimu wa kidato cha nne ameishukuru ICAP kwa jinsi walivyomuwezesha hadi kufikia hatua ya kujiamini na kwamba kabla hajajiunga na kikundi hicho hakuwa na shughuli yoyote ya kumuingizia kipato na ndipo alijiunga na kikundi hicho mwaka 2021.

      Irene John akishona nguo

“Nilipata mafunzo juu ya afya yangu, kujiwezesha kiuchumi na nilianza kujifunza kushona nguo za kike na kiume, kupitia ICAP nimepata mafunzo ya ushonaji kutoka SIDO na kujiongezea kipato, nina cherehani yangu mwenyewe na nina uwezo wa kuingiza Sh 300,000 kwa mwezi”, amesema Irene huku akionekana kuwa na furaha.

Mwanakikundi Zainabu Josephat (23) amekiri kuwa yeye ni mnufaika mkubwa wa mradi huo wa DREAMS na kufafanua kuwa, kabla hajajiunga na mradi alikuwa anafanya kazi ya kuuza baa hadi alipotembelewa na mwelimisha rika kutoka mradi huo aliyempatia elimu ya afya likiwemo suala zima la upimaji wa virusi vya UKIMWI.
            Baadhi ya wasichana wa kikundi Cha Umoja

“ Ilikuwa ngumu sana kwangu kujua afya yangu maana nilikuwa pia najihusisha na biashara ya ngono, lakini alinishawishi na kupimwa na nikakuta mimi ni mzima wa afya, nikajiiunga na kikundi na kupata pia elimu ya afya na ujasiriamali, kwa sasa nina biashara ya sabuni inayonipatia kipato.

Happines Peter (18) amesema alijiunga na kikundi hicho baada ya kuhitimu shule na kukosa kazi ya kufanya na kwamba kikundi hicho kilimsaidia na kupata mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya afya baada ya kujiunga na SIDO.

     Happynes Peter akionesha ngo aina ya Batiki aliyoitengeneza

Amesema baada ya kupata mafunzo ya ujasiriamali alianza kutengeneza vitenge aina ya batiki kwa mtaji wa TSh 45,000 aliyoitumia kununua bidhaa na vifaa ambavyo vinampatia faida japo awali alipata changamoto ya wateja na vifaa. amelishukuru Shirika la ICAP kwa kumjengea uwezo kupitia mradi wa FIKIA+.

Annastazia Samwel amesema amenufaika na mradi wa DREAM kwa kupatiwa elimu ya ujasiriamali kupitia SIDO na amewezeshwa kuifahamu afya yake na kufafanua kuwa alikuwa ni mhanga wa vitendo vya ukatili vya kupigwa alivyokuwa akifanyiwa na baba yake mlezi.

“Nashukuru ICAP nlipata elimu ya kutengeneza sabuni kupitia SIDO na  naiomba serikali yangu iniwezeshe zaidi mtaji ili niweze kujiendeleza zaidi kibiashara”, amesema Annastazia. 

Christina amesema kikundi chao kilicho chini ya mradi wa DREAMS, licha ya kuwezeshwa kwenye shughuli za ujasiriamali ikiwemo kutengeneza batiki, sabuni na kushona nguo, bado kinakabiliwa na changamoto ya masoko na bidhaa zao kutokuwa na ubora huku akisisitiza kuwa endapo Rais Samia akiwatembelea atajionea shughuli wanazozifanya na kuwasaidia kutatua changamoto.

      Makamu Mwenyekiti wa Kamati akiwa na wanakikundi

Amesema kikundi kinalishukuru Shirika la ICAP kuwaweka pamoja kwani kwa muda mrefu walikuwa wahanga wa ukatili huku baadhi wakijihusisha na  vitendo vya ngono isiyo salama kwenye kumbi za starehe na kufanya biashara ya ngono.

“ Lakini tunalishukuru sana Shirika la ICAP kwa kutuweka pamoja na kutupa mafunzo ya shughuli za ujasiriamali zinazotuwezesha kujikwamua kiuchumi, kikundi chetu kina wanachama 25 pia tumefundishwa namna ya kuweka akiba, elimu ya maadili na namna ya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya UKIM WI.

Anifa Eliud amesema kama itashindikana Rais Samia kukitembelea kikundi hicho, amemuomba Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya UKIMWI, Kifua Kikuu, Dawa za Kulevya na magonjwa yasiyoambukiza Dk Alice Kaijage aone namna ya kusaidia kikundi hicho kipate fursa ya kwenda bungeni ili kikaeleze bayana mambo wanayoyafanya kwa ufadhili wa ICAP na changamoto wanazokabiliana nazo.

“Tukifika Bungeni tutapata fursa ya kuonana na waheshimiwa wabunge na kuzungumza mambo yetu na hivyo hoja zetu tunaamini zinaweza zikamfikia Rais”, amesema.

Wanakikundi wamesema bado wana kiu ya kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo kwa ajili ya ustawi wa maisha yao kwakuwa tayari wamejengewa uwezo wanajiamini na kujitambua.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya UKIMWI, Kifua Kikuu, Dawa za Kulevya na magonjwa yasiyoambukiza Dk. Alice Kaijage amewashukuru viongozi wa DREAMS kwa mapokezi mazuri waliyoyapata na kuahidi kuchukuwa hoja zao kama walivyoomba ya Rais Samia Suluhu ya kuwatembelea na kulitembelea bunge na kusisitiza kuwa maombi yao yote mawili yanawezekana.

       Makamu Mwenyekiti  Dkt.Alice Kaijage na Wajumbe wa Kamati wakiangalia bidhaa za kikundi cha Umoja 

Dkt. Kaijage ameuomba uongozi wa Halmahauri ya jiji la Mwanza kuhakikisha kikundi hicho cha umoja kinapata mikopo ya vijana inayotolewa na Halmashauri ili waweze kuitumia kwenye shughuli zao za ujasiriamali.

“ Lakini nichukue fursa hii kuwashukuru sana ICAP kwa kuwafadhili vijana hao na ujuzi ambao tumeona wanafanya mambo makubwa sana”, amesema.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. PIUS Maselle amesema mkoa wa Mwanza kupitia Halmashauri zake nane, hospitali za rufaa na hospitali binafsi zimetengewa zaidi ya TSh. Bilioni 2.3 katika mwaka wa fedha ulioanza Oktoba mwaka huu hadi mwezi Septemba, 2023 kwa ajili ya utekelezaji wa afua zingine za kudhibiti UKIMWI na tohara.

Amesema fedha hizo zimetolewa na Shirika la ICAP kupitia mradi wa FIKIA+ unaolenga kuongeza chachu ya kufikia malengo ya 95-95-95 kwa kuhakikisha watu wanaoishi na VVU wanaanzishiwa dawa za kufubaza VVU,  kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani chini ya Mfuko wa Rais wa Marekani wa Dharula wa Kupambana na UKIMWI(PERFAR).

Ameongeza kusema ICAP kupitia mradi huo imeajiri watumishi 355 katika vituo vya kutolea huduma na zaidi ya Tsh Bilioni 3.5 zinatumika kwa mwaka kwa ajili ya kulipa mishahara na satahiki nyingine kwa watumishi wa kada ya afya.

       Wajumbe wa Kamati ya bunge wakionesha Batiki kutoka kikundi cha Umoja

Mbunge wa Viti Maalum kutoka mkoani Mara Agnes Marwa amewataka wasichana hao kuedelea kuishi na kufanya sahughuli zao kwa kuzingatia maadili na mwenendo wa tabia njema katika jamii.

“Tumefurahi sana kuwa na ninyi na niwaambie tunawapenda na mtakuja bungeni”, amesema Marwa.

Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Stanslaus Mabula, amelishukuru Shirika la ICAP kwa kazi kubwa ya kuwaweka vijana hao pamoja na kupata elimu ya ujasiriamali, aliahidi kufuatilia uongozi wa jiji la Mwanza ili kikundi hicho kiweze kupatiwa mikopo.

Mkurugenzi wa Utafiti wa THIS 2022-2023  Dk Deogratias Kakiziba amesema kwa mwaka huu, CDC na ICAP wanatekeleza utafiti wa viashiria na matokeo ya UKIMWI Tanzania, utafiti unaoongozwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).

Pia Tume ya Kudhibiti UKIMWI Zanzibar (ZAC), Wizara ya Afya Tanzania bara na Wizara ya Afya Zanzibar, Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar, na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

           Irene John akiwa na wasichana wenzake akimkabidhi Balozi wa Marekani nchini zawadi alipotembelea kituo hicho.

Amesema Utafiti wa THIS 2022-2023 ni utafiti wa kitaifa unaofanyika ngazi ya kaya nchi nzima ili kutathmini programu za tiba na matunzo ya VVU nchini na kutathmini hali ya mwitikio wa kitaifa wa VVU nchini Tanzania, hatari za VVU na utumiaji wa huduma za VVU miongoni mwa watu wazima wenye miaka 15 na zaidi. Utafiti huo pia utapima maambukizi ya Homa ya ini B na Homa ya ini C.

Dk Kakiziba amesema ukusanyaji wa taarifa za utafiti wa THIS wa mwaka 2022-2023 kwa sasa unaendelea katika maeneo yaliyochaguliwa Tanzania bara na Zanzibar, na utafiti huo unatarajiwa kufikia takriban kaya 20,000 zilizochaguliwa kwa sampuli wakilishi.

"CDC na ICAP inahudumia jumla ya vituo vya afya 208 ambavyo vinatoa huduma za tiba na matunzo ya VVU kwa watu 118,163 wanaoishi na VVU (kwa takwimu za mwishoni mwa Septemba 2022),".

Amesema katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2022, ICAP ilitoa huduma za upimaji wa VVU kwa watu 93,108, na watu 4,515 waligundulika kuwa na maambukizo ya VVU na 4,494 (99.5%) walianzishiwa dawa za ARV.


ICAP inatoa huduma za uchunguzi wa kifua kikuu (TB) katika maeneo hayo na jumla ya watu 117,714 walifanyiwa uchunguzi wa  Kifua Kikuu, watu 2,310 walionekana na dalili za Kifua Kikuu na kati ya hao 519 walipimwa na kuanza matibabu ya Kifua Kikuu. 

Upimaji wa Kifua Kikuu hufanywa kupitia vifaa vya kisasa (gene Xpert) na watu 8,616 wanaoishi na VVU walianzishiwa dawa kinga ya Isoniazid (IPT) kuwakinga dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa kifua kikuu.


No comments