HEADER AD

HEADER AD

WATUMISHI IDARA YA HUDUMA ZA UCHUNGUZI WATAKIWA KUWAJIBIKA


Na. WFA – Dar es Salaam 

KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi amewataka watumishi wa Idara ya Huduma za Uchunguzi na Vifaa Tiba kufanya kazi kwa uwajibikaji wa haraka na kuleta matokeo chanya katika ubora wa majibu ya vipimo kwa Wananchi.

Prof. Makubi ametoa kauli hiyo Desemba, 24,2022, Jijini Dar es Salaam wakati alipofanya kikao kazi na watumishi wa Idara ya Huduma za Uchunguzi na Vifaa Tiba iliyoko Wizara ya Afya kilichofanyika ukumbi wa NIMR Jijini Dar es Salaam.

Prof. Makubi amesema anataka mabadiliko yatakayosaidia wananchi kupata majibu ya vipimo yenye viwango na usahihi,  na kwa muda mfupi. 

Prof. Makubi amesema Wananchi wamekuwa wakilalamika kuhusu usahihi wa baadhi ya majibu kama UTI, Malaria, Typhod, huduma za radiolojia, damu na mengineyo na hivyo lazima Idara ya uchunguzi itimize jukumu lake katika sekta. 

Prof. Makubi ameelekeza hospitali za Rufaa za Mikoa na Halmashauri kuhakikisha zinajengewa uwezo wa wao kufanya matengenezo ya vifaa vyao vya maabara na kufuata  miongozo itolewayo na wizara ili kuongeza ufanisi katika maabaara zote nchini”, amesisitiza Prof. Makubi.

Vile vile amesema kuwa wasimamie miongozo yote inayotolewa na wizara ya afya katika maabara zote nchini ili kutatua changamoto ya wananchi kupewa majibu yasio sahihi na kucheleweshewa majibu ya vipimo vyao.

“Ili kufanikisha usimamizi wa miongozo katika maabara zetu jengeni utamaduni wa kukagua maabara mara kwa mara kama zinafuata miongozo iliyotolewa na wizara”, ameeleza Prof. Makubi.

Hata hivyo, Prof. Makubi amewataka kuwa na uwajibikaji wa ndani ya ofisi kwa kutaka majalada  yanayoletwa kwenye idara yanafanyiwa kazi kwa haraka na kurudishwa sehemu husika.

 "Haiwezekani mnakuwa mnaacha ofisi zenu muda mwingi kwa Mwezi mkiwa mnaacha kazi za ofisi haziendi. lazima mgawe muda wa kwenda kukagua kazi mikoani na pia muda wa kushughulikia majalada ofisini na siyo kuzurura muda wote". Prof Makubi amesema.

Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu amesema kuwa huduma zitolewazo katika maabara za hospitali ziendane na thamani ya fedha iliyotumika kuwekeza vifaa hivyo ili kuweza kuwa na maabara bora katika kuelekea utalii wa afya.



No comments