HEADER AD

HEADER AD

WANANCHI WAIOMBA TAKUKURU KUWAPA ELIMU UTOAJI TAARIFA ZA UBADHILIFU

 


Na Jovina Massano, Musoma.

WANANCHI Mkoani Mara wameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutoa elimu zaidi kwa kina ya namna ya utoaji taarifa dhidi ya ubadhilifu wa miradi ya maendeleo inayojengwa hapa nchini.

Wameyasema hayo baada ya kupata elimu kutoka kwa Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma Mkoa wa Mara Amos Ndege kutoka TAKUKURU, katika mkutano wa hadhara wa Kata ya Kwangwa.

Mkuu huyo ametoa elimu ya rushwa kwa jamii ambapo ameeleza umuhimu wa wananchi katika utoaji taarifa ofisi za TAKUKURU dhidi ya ubadhilifu unaofanyika katika miradi ya maendeleo iliyopo kwenye maeneo ili miradi hiyo isifanyike chini ya kiwango.

               Amos Ndege

"Watu wengi wanapata matatizo katika huduma tofauti tofauti na hawajui haki zao ukiona mambo yanakwenda sivyo toa taarifa lakini pia nawasihi wananchi kulea familia zenu katika maadili kwani rushwa ni tabia inayoanzia chini namna malezi yanavyotolewa kwa watoto wetu.

"Iwapo tutawaelimisha vitendo hivyo vitapungua ,nawasihi pia kuwa macho katika kufuatilia  miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yetu kama kuna ubadhilifu unafanyika katika mradi toeni taarifa ili tushughulikie".

Ameongeza kuwa miradi inajengwa kwa fedha zinazoletwa na serikali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi zinazotokana na kodi zao hivyo waone umuhimu wa kusimamia ili kodi zao zitumike vizuri kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kituo cha afya Makojo

DIMA ONLINE imezungumza na baadhi ya wananchi kupata maoni yao juu ya uwajibikaji wao katika usimamiaji wa miradi ya maendeleo inayojengwa kwa fedha za Serikali.

Mkazi wa Kijiji cha Makojo Lucy Mgini ameiomba TAKUKURU kutoa elimu kwa kina ili uelewa wa wananchi kuhusu miradi hiyo uwe mpana zaidi.

"Binafsi mie sifahamu kama sisi wananchi tuna nafasi hiyo kwenye miradi ya maendeleo najua ufuatiliaji ni wa viongozi wa Serikali pekee kwa kuwa huwa tunaona wanakuja na magari yao katika miradi na kukagua sisi wananchi tunakuwa tunawaangalia na kuwasikiliza, tunaomba elimu zaidi ili tuelewe na kuwa mstari wa mbele kufuatilia hayo", amesema Lucy.

Mkazi wa Mtakuja Lawi Mgeta amesema mtu akiwa hajihusishi na kitu chochote katika miradi ni vigumu kuelewa kama miradi hiyo imejengwa chini ya kiwango na miradi mingine wananchi hawashirikishwi kujua mapato na matumizi katika ujenzi wa miradi.

                     Lawi Mgeta

"Naiomba TAKUKURU kutoa elimu zaidi ya kutosha kwa wananchi kuhusiana na namna ya kutoa taarifa ya ubadhilifu kwani ni vigumu kutambua kama haupo kwenye kamati ya maendeleo katika Kata na maeneo mengine ni bora kuwepo na elimu endelevu ili wananchi waelewe namna ya kuisimamia miradi hii",amesema Lawi.

Mkazi wa Kiara A Mshua Magabi ameshukuru TAKUKURU kwa kuwafungua macho na masikio kwa elimu ya usimamizi wa miradi hiyo na kuahidi kuwa watahakikisha wanatoa taarifa, lakini ameiomba TAKUKURU kuchukua hatua kwa haraka pindi wapatapo taarifa kutoka kwa wananchi.

               Mradi wa Vyumba vya madarasa

"Kwanza nampongeza Mama yetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu kwa kutuletea fedha za miradi ya vyumba vya madarasa   kwani hapo nyuma tulikuwa tunachangishwa na ukiwa hauna pesa utauza hata kuku utoe mchango ukizingatia hivi sasa mzunguko wa fedha ni mdogo.

"Rais Samia ametupunguzia kimbizana kimbizana na viongozi wa Kata, kwa elimu hii kutoka TAKUKURU tutahakikisha fedha alizozileta tunazutendea haki kwa kufuatilia kwa ukaribu, tunamuomba muelimishaji atuelimishe zaidi kwa kina ili miradi iwe ya kiwango kulingana na fedha zilizotengwa",amesema Mshua. 
                   

No comments