HEADER AD

HEADER AD

TANAPA YANADI VIVUTIO VYA UTALII KOMBE LA DUNIA NCHINI QATAR

Na Mwandishi Wetu, Doha,Qatar

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za Wizara ya Maliasili na Utalii (TTB,TFS) na kituo cha uwekezaji Tanzania -TIC limefanikiwa kutangaza vivutio vya utalii na fursa mbalimbali za uwekezaji Nchini Qatar.

Vivutio hivyo vya utalii kutoka nchini Tanzania vimetangazwa Doha mji mkuu wa nchi ya Katari (Qatar) kunakofanyika michuano ya mpira wa miguu kombe la Dunia (FIFA World Cup 2022).

Katika maonesho hayo, Tanzania ni nchi pekee kutoka Afrika iliyopewa nafasi ya kuwa na banda huku nchi ya Korea, Marekani na Uturuki nazo zikishiriki maonesho.


Wageni kutoka Mataifa mbalimbali waliofika nchini humo kwa ajili  ya mashindano ya kombe la Dunia, wamepata taarifa muhimu kwa karibu na kwa urahisi zinazohusu vivutio vinavyopatikana Tanzania, huduma muhimu na njia za kuwafikisha.

Balozi wa Tanzania nchini Qatar Mahadhi Juma Maalim amepata nafasi ya kukutana na washiriki wa maonesho hayo na kufanya kikao kilichojadili masuala ya kuendeleza utangazaji wa vivutio vya Tanzania ikiwa ni pamoja na kuwa na vipeperushi vya lugha ya kiarabu ambayo ndiyo inatumika zaidi nchini humo.

Pia ofisi ya ubalozi imewakutanisha washiriki na wawekezaji walionesha nia ya kuwekeza nchini na kufanya nao mazungumzo ili kuongeza wigo wa matangazo na uhamasishaji washiriki kwa kushirikiana na ofisi ya ubalozi na kwamba ajenda kuu ni pamoja na kuzungumzia masuala mbalimbali yahusuyo utalii wa Tanzania na uwekezaji.  




No comments