WAANDISHI WA HABARI DAR WAPEWA ELIMU YA UGONJWA WA EBOLA
Na Andrew Chale, Dar es salaam
WIZARA ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Sayansi ya Usimamizi wa Afya (Management Science for Health) MSH wanatarajia kuwafikia Wanahabari zaidi ya 120 wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwajengea uwezo wa namna sahihi ya kuripoti na kutoa elimu juu ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola endapo utaingia Nchini.
Akizungumza wakati kuwasilisha mafunzo hayo kwa kundi la pili Desemba 11,2022, kwa Waandishi 40, mratibu wa kitengo cha kujikinga na kudhibiti maambukizi kutoka wizara ya afya Dkt.Joseph Hokororo amesema ushirikiano wa pamoja na wadau mbalimbali nchini wakiwemo wanahabri utasaidia jamii kupata uelewa wa kutosha katika kukabililiana na ugonjwa.
Dkt. Joseph Hokororo amesema Ebola ni ugonjwa hatari unaoambukizwa kwa kasi na kusababisha vifo kama hatua za haraka hazitachukuliwa, ushirikiano wa pamoja ni muhimu sana, pia tuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha tunaendelea kuelimisha jamii zetu ili ziweze kuwa na ustaarabu wa kuzingatia miongozo na kanuni za usafi.
Afisa Mawasiliano mwandamizi kutoka Kitengo cha Mawasiliano Serikali Wizara ya Afya Catherine Sungura amesema wameamua kutoa mafunzo hayo kwa kundi hilo la wanahabari ili kuwawezesha kutoa taarifa sahihi zinazohusiana na ugonjwa huo ili kuepuka upotoshwaji unaoweza kuleta taharuki katika jamii.
Catherine amesema mafunzo kama hayo tayari yametolewa kwa waandishi wa habari mkoa wa Kagera lengo likiwa kuwajengea uwezo wanahabari hao kutoa elimu sahihi juu ya kujikinga na Ebola.
Naye mwezeshaji na mtaalamu wa Kujikinga na kudhibiti Maambukizi kutoka Taasisi ya Jamii Bora Health Services Network Bwana Said Chibwana amesema njia za kujikinga na ugonjwa wa Ebola ni kufuata taratibu na miongozo ya afya ambayo imekuwa ikitolewa na wataalamu wa afya ikiwemo kuzingatia suala la uoshaji wa mikono kwa sabuni na maji tiririka.
Dkt. Doris Lutkam mwakilishi kutoka MSH amehamiza Wanahabari hao kuhakikisha wanaripoti taarifa kwa usahihi na hata kuwa Walimu kwa wengine sambamba na kuhimiza kufuata kanuni sahihi kama walivyofundishwa na watalaam.
Wanahabari wengine kundi la tatu wanatarajiwa kujengewa uwezo Desemba 12, 2022 huku lengo likiwa kuwafikia Wanahabari pamoja na Wahariri na waandaji wa vipindi zaidi ya 120 Kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
Post a Comment