HEADER AD

HEADER AD

TARIME TC YASHINDWA KUTEKELEZA AGIZO LA NAIBU WAZIRI TAMISEMI


>>Ni lile la kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 

>>Silinde aliagiza ifikapo Desemba 15 madarasa yawe yamekamilika na wamtumie picha


Na Dinna Maningo, Tarime

HALMASHAURI ya Mji Tarime imeshindwa kutekeleza agizo la Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) David Silinde la kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa vilivyotakiwa kukamilika Desemba, 15, 2022.

Naibu Waziri Silinde akiwa katika ukaguzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari Nyamisangura, aliiagiza Halmashauri hiyo ifikapo Desemba,15, 2022 iwe imekamilisha ujenzi.

Pia  itume TAMISEMI taarifa ya ujenzi wa madarasa ikionesha na picha za majengo yakiwa yamekamilika na ndani yakiwa na madawati huku akiahidi kurudi Tarime Desemba, 19, 2022 endapo ujenzi utakuwa haujakamilika.

Silinde alitoa agizo hilo mwezi Novemba, 27, 2022 wakati akiwa kwenye ukaguzi wa vyumba vya madarasa katika shule hiyo ambapo alikatisha ziara yake na kutoendelea na ukaguzi katika shule zingine baada ya kukuta ujenzi wa shule hiyo ukiwa hatua ya lenta na kusema hata shule zingine anajua hali ni hiyohiyo. 

           Waliosimama mbele ,kulia ni Naibu Waziri TAMISEMI David Silinde akizungumza jambo na Mkuu wa Wilaya ya Tarime Kanali Michael Mtenjele wakati akikagua ujenzi wa madarasa shule ya Sekondari Nyamisangura

DIMA ONLINE Mwezi Desemba, 18, 2022, imefika katika shule ya Sekondari Turwa B, Tagota, Bomani, Iganana na Nyamisangura na kukuta ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule hizo haujakamilika huku mafundi wakiwa wanaendelea na ujenzi, hakuna darasa lolote lililokamilika na kuwa na madawati ndani.

Katika shule mpya ya sekondari Turwa B iliyopo Kata ya Turwa ujenzi wa vyumba 10 vya madarasa unaendelea ambapo madarasa yote 10 yameezekwa kwa bati, yana madirisha, hatua ya upigaji lipu ndani ya vyumba tayari isipokuwa kuta  za nje madarasa  mengine hayajapigwa lipu na madarasa mengine hayajakaziwa tofari za juu.

       Madarasa shule mpya ya Sekondari Turwa B

vyumba hivyo vyote chini havijawekwa sakafu na vyumba vingine havijawekwa ubao wa wanafunzi kujifunzia, milango haijawekwa na hakuna vyoo vya wanafunzi.

Shule ya sekondari Tagota Kata ya Kenyamanyori ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa unaendelea, vyumba vitatu vimeezekwa bati, vimepigwa lipu ndani na nje vipo kwenye hatua ya uwekaji wa sakafu na madarasa mawili ujenzi wake bado ni wa kujikongoja upo usawa wa lenta.

             Vyumba vya madarasa shule ya Sekondari Tagota

DIMA ONLINE imefika katika shule ya Sekondari Bomani Kata ya Bomani na kukuta ujenzi wa madarasa matano ukiendelea, ambapo yote yameezekwa kwa bati na kupigwa lipu nje na ndani, pia hatua zingine za ukamilishaji bado kama milango, sakafu ,rangi.

          Madarasa shule ya Sekondari Bomani

Shule ya Sekondari Iganana madarasa manne yameezekwa kwa bati na kupigwa lipu ndani na nje,darasa moja limewekewa Gypsam, hatua zingine za ukamilishaji zinaendelea kama uwekaji wa sakafu.

Madarasa yote bado hayajapakwa rangi na madarasa mawili bado ujenzi ni wa kujikongoja moja lipo usawa wa lenta na lingine lipo usawa wa madirisha ujenzi unaendelea. 

            Ujenzi wa vyumba vya madarasa shule ya Sekondari Iganana

Katika ujenzi wa shule ya sekondari Nyamisangura shule ambayo ilifanikiwa kutembelewa na Naibu Waziri TAMISEMI na kukuta ujenzi wake ukiwa hatua ya lenta, hadi sasa madarasa yote 6 yameezekwa bati na kupigwa lipu, ila hayana sakafu, milango, hayajapakwa rangi, madarasa hayana madawati.

Vyumba vya madarasa vimeezekwa kwa bati aina ya Alaf Simba Dum saizi ya 28 na mbao zilizoelezwa ni aina ya Sepras na Saruji aina ya Twiga Plus.

         Madarasa Shule ya Sekondari Nyamisangura

Hata hivyo habari kutoka katika vyanzo mbalimbali vya habari zinasema kuwa, sababu ya vyumba vya madarasa kutokamilika kwa wakati ni pamoja na vifaa vya ujenzi kuchelewa kufika kwa wakati kwenye maeneo ya ujenzi hali inayosababisha mafundi ujenzi kukaa siku tatu hadi wiki bila kufanya kazi wakisubiri vifaa.

Inadaiwa kuwa, baadhi ya vifaa vya ujenzi kama mbao zilikwenda kununuliwa Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa huku mabati na vifaaa vingine vikienda kununuliwa Mkoani Dar es Salaam hivyo kuchelewa kufika kwa wakati.

                            Mbao

Habari zinasema mashine inayotengeneza (Kufyatua) tofali iliyopo ndani ya Halmashauri ya Mji Tarime haina uwezo wa kuzalisha tofali nyingi kwa wakati kwakuwa mahitaji ni makubwa na ndio pekee inayozalisha tofali za kujenga vyumba 41 vya madarasa katika shule zote zilizopata mradi wa ujenzi huo.

Inadaiwa kuwa, kutokana na madarasa kutokamilika kwa wakati na Halmashauri hiyo kujihukumu kwa Silinde kuwa ingekamilisha ujenzi Desemba, 15,2022, mafundi wamejikuta wakipokea na kutumia tofali mbichi ambazo hazijakauka zingine zikiwa na siku mbili tangu zifyatuliwe huku majengo hayo yakikosa muda wa kutosha wa kumwagiliwa maji  kutokona na kujengwa haraka haraka ili yakamilike.

Hali hiyo inaelezwa kuwa, huko mbeleni huwenda Serikali ikajikuta inaingia gharama zingine kukarabati majengo hayo kutokana na ujenzi huo kutofuata taratibu za ujenzi na hivyo kupoteza uimara wa  majengo kuweza kudumu kwa miaka mingi.


DIMA ONLINE ilifika ofisi ya Halmashuri ya Mji Tarime kupata sababu za kutokamilika ujenzi kwa wakati na madai ya vifaa kuchelewa kwasababu ya kufuatwa Iringa na Dar es Salaam juhudi hizo ziligonga mwamba kwa kile kilichoelezwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuri hiyo, Ntavyo Gimbana ndio msemaji na yupo safarini kikazi.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Daniel Komote na Makamu Mwenyekiti Thobias Ghati  wakisita kuzungumzia suala hilo. Juhudi za kumtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo zinaendelea.

Awali Naibu Waziri Silinde akikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Sekondari Nyamisangura, Mkuu wa wilaya ya Tarime Kanali Michael Mtenjele alisema sababu ya Halmashauri ya wilaya Tarime ujenzi wake kuwa katika hatua nzuri ni kutokana na wao kununua matofali kwa watu mbalimbali.

Alisema Halmashauri ya Mji Tarime wao walitegemea matofali kutoka kwenye kiwanda cha matofali cha Halmashauri kinachozalisha tofali za kujenga madarasa yote na hivyo kushindwa kumudu kwa muda unaotakiwa.


Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu imetoa fedha T.sh Milioni 820 katika Halmashauri ya Mji Tarime kujenga vyumba vya madarasa vipatavyo 41ambavyo ujenzi wake bado unaendelea.

Novemba, 27, 2022 kupitia Tovuti ya dimaonline.co.tz iliripoti habari yenye kichwa cha habari kisemacho " NAIBU WAZIRI TAMISEMI AKATISHA ZIARA YA UKAGUZI TARIME"

Ni baada ya kukagua ujenzi shule ya Sekondari Nyamisangura na kutoridhishwa na ujenzi, ambapo aliiagiza Halmashauri hiyo ifikapo Desemba 15,2022 itume TAMISEMI picha za ujenzi wa vyumba vya madarasa na zimfikie huku akiahidi endapo ujenzi utakuwa haujakamilika atarudi tena Tarime kufanya ukaguzi.

Nukuu ya Silinde:
"Mnasema Tarehe 15 ujenzi utakuwa umekamilika! mna uhakika? Kwingine huko ukiliangalia jengo unaona lipo kwenye hatua nzuri, yale ambayo yapo kwenye hatua za mwisho walishapiga plasta, wameshafunga Gypsum na ukamilishaji.

"Hata mtu akikwambia namalizia ndani ya wiki moja unaona kabisa inawezekana, sasa leo mtu anakwambia hapa wanapoweka lenta tarehe 10-15 patakuwa pamekamilika, sawa acha mimi nichukue hilo, lakini narudia tena mnanijua vizuri kwenye hili, sipendi kudanganywa, alafu sipendi mtu anaharibu kazi ya Mhe. Rais" alisema Silinde.

Aliongeza " Katika kitu ambacho tutagombana mapema sana na nitakuja kutolea mfano hapa hapa Tarime haya majengo yasipokamilika, hii nawahakikishia kwa asilimia 100, na niseme ukweli Mh. DC hawa wamekuangusha, wale wa Tarime Vijijini wamefanya vizuri"alisema Silinde.

          Naibu Waziri TAMISEMI David Silinde akiwa shule ya Sekondari Nyamisangura

"Kule Tarime Vijijini wamesema kila kitu wanatoa hapa mjini, simenti wananunua huku huku, mawe, nondo na vitu vingine wamesema wamenunua huku alafu nyinyi mmezubaa, mjini mnashindwa na kijijini! mmetuangusha" alisema Silinde.

 " Hii hali  ipo maeneo yenu madarasa mengi hayajakamilishwa, hata huko Turwa najua mko kwenye hali hii, Mkurugenzi tarehe 15, Desemba, 2022 nataka hiyo taarifa ikionesha picha za majengo yakiwa na madawati ndani yake.

" Narudia tena naongea kama natania tarehe 12, mwezi wa 12 taarifa hiyo mnapotuma Mkoani  na Ofisi ya Rais TAMISEMI ifike na inifikie, na tarehe 19 mwezi wa 12 nitakuwepo hapa nitapita Turwa B nitapita na maeneo mengine, nitachagua sampo mwenyewe shule nitakazozitembelea hamtanichagulia kwasababu nina vyanzo vya kupata taarifa.

Aliongeza " Nitakuja mwenyewe, nitamwambia Mh.DC nakuja taarifa kuhusu natembelea shule gani ataijua ofisini kwakwe siku hiyo, utani kwenye kazi sitaki tusiharibiane kazi, kila mmoja aheshimu kazi ya mwingine, najua mtafuatilia na hii kazi itakamilika......," alisema.

Picha za ujenzi wa Madarasa shule ya Sekondari Turwa B










Picha za ujenzi wa vyumba vya madarasa Shule ya Sekondari Tagota






Picha za ujenzi wa vyumba vya madarasa Shule ya Sekondari Bomani




Picha za ujenzi wa vyumba vya madarasa Shule ya Sekondari Iganana.












Picha za ujenzi wa vyumba vya madarasa Shule ya Sekondari Nyamisangura








Picha. Baadhi ya vifaa vilivyotumika kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Mbao Aina ya Seprasi



Picha za bati Aina ya Simba Dum






Saruji ya Twiga Plus

Gypsum



Picha hizi za ujenzi wa vyumba vya madarasa na vifaa vya ujenzi zimepigwa Tarehe , 18, Desemba, 2022 na Mwandishi wa Habari Dinna Maningo.

No comments