VIKOMBE RANGI NYEKUNDU, KIJANI VYAWATESA WAUZA MAHARAGE SOKONI
Na Dinna Maningo, Tarime
UKEREKETWA wa kisiasa kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na ushabiki wa mpira wa miguu timu ya Simba na Yanga umezua sura mpya.
Ni baada ya siasa za kivyama na kishabiki kuingia katika biashara ndani ya soko la Rebu Wilayani Tarime Mkoa wa Mara.
Wanawake wanaofanya biashara ya kuuza maharage katika soko hilo wanalazimika kuwa na vikombe vya rangi ya kijani, rangi ambayo inatumiwa pia kama sare ya CCM na nyekundi sare ya CHADEMA ili kuwapimia wateja.
Imeelezwa kwamba, mteja akifika kununua maharage akakuta muuzaji hana kikombe cha rangi hizo basi hulazimika kuomba kikombe kwa wenzake ili amuhudumie mteja rangi ya kikombe anachokitaka huku wateja wengine wakiacha kununua na kwenda kwa wauzaji wenye vikombe vya rangi hizo.
Wanawake wanaouza maharage kwa kutumia kipimo cha vikombe katika soko hilo, wameieleza DIMA ONLINE namna siasa ya kivyama na ushabiki ilivyopenya katika biashara yao na kusababisha ubaguzi wa rangi za vikombe vyenye rangi zinazofanana na sare zinazovaliwa na wanachama wa CCM na CHADEMA pamoja na timu ya Simba na Yanga.
Rhobi Chacha muuzaji wa maharage anayetumia kikombe kama kipimo cha nusu kilo amesema" Siasa ya vyama imepenya hadi kwenye biashara yetu ya maharage tunalazimika kuwa na vikombe vya rangi nyekundu na kijani ili biashara zetu ziende vizuri, usipokuwa na vikombe hivyo biashara yako itakuwa ngumu utakosa wateja.
"Wateja wakifika hapa kununua maharage wengine hawataki uwapimie kikombe cha kijani wengine hawataki kikombe chekundu na ni hiari yake huwezi kumshurutisha umpimie kikombe unachokitaka wewe unakubali maana wewe unachotaka ni pesa upo sokoni kwa ajili ya kutafuta pesa". amesema Rhobi.
Maria Turwa amesema" Watu huwa wanakuja hapa sokoni ukitaka kumpimia maharage anakwambia sikati hicho kikombe tumia hiki, mwingine alikuja nikataka kumpimia kwa kikombe cha rangi ya kijani akakirusha kule akaniambia wewe kama hutaki nikuchangie nitaondoka tafuta kikombe ninachokitaka.
"Nikamuuliza unataka kikombe gani ?akaniambia chekundu, sikuwa na kikombe chekundu nikawaambia wenzangu naomba kikombe chekundu nikapewa nikampimia nikalazimika kununua kikombe chekundu.
"Siku nyingine akaja mteja mwingine nikata kumpimia kwa kikombe chekundu akakataa akasema anataka kikombe cha kijani ikabidi nimpimie kwa kikombe anachotaka" amesema Mariamu.
Lucy Juma amesema " Ukiwauliza kwanini wanataka hizo rangi mwingine anakwambia mimi ni CCM mwingine mimi ni CHADEMA kwahiyo wanataka rangi zinazofanana na sare zao za Chama, kuna watu vyama vipo damuni utadhani wamechanjiwa.
" Unaona hapa tuna vikombe vya rangi zote na katika rangi hizo lazima rangi nyekundu na kijani iwepo akija anataka kikombe hiki unapima, na sisi tunavitumia kisiasa, ili biashara yako iwe nzuri lazima uwe na hizo rangi za wakereketwa ilimradi upate maslahi yako" amesema Lucy.
Walipoulizwa kwanini wanatumia vikombe kama kipimo badala ya kutuma mizani wamesema kuwa mizani ni gharama lakini vikombe ni bei nafuu.
"Unatuona sisi wanawake tunaouza maharage wengi wetu hapa maisha ni ya chini wengine hatuna wanaume tulishatelekezwa tunalea watoto wenyewe, wengine ni wajane, haya maharage ndio roho yetu, kulingana na hali ya maisha tunapima kwa kutumia vikombe hatuna uwezo wa kununua mzani.
"Vikombe tunavinunua sh. 500 kwa kila kikombe bei ambayo ni nafuu hata mwanamke maskini atajitahidi kununua ili apimie wateja, mizani ina gharama ili ununue ni zaidi ya 150, 000 hebu niambie mimi ninayeuza maharage kwa mtaji wa sh. 20,000 na wakati mwingine mzigo unaisha baada ya siku tatu, utapata lini pesa ya kununua mzani ili upime maharage?.
" Faida yenyewe tunayopata ni Tsh.3,000- 2,000 kwa mzigo unaoununua, bado watoto wale, wakiugua watibiwe, bado nguo, bado ununue mahitaji ya shule na hapo ujue kodi ya nyumba inahitajika kwa biashara hiyohiyo ya maharage, bado ulipe ushuru wa soko" amesema Ghati Mwita.
Ameongeza "Bado pesa ya mlinzi kila mwezi ulipe sh.1500 kwa biashara hii hii ya maharage huo muzani unaununuaje? istoshe bei tunayouza maharage kwa kikombe kimoja ni Sh . 1000 ambayo ni nusu kilo inapelea kidogo tu kukamilika nusu ukienda dukani kwenye kilo nusu ni Sh 1200," amesema Ghati.
Rebeka John amesema baadhi ya wauzaji wa maharage nao ni wakereketwa wa vyama, hutumia rangi inayofanana na sare ya chama alichopo, hawatumii vikombe vyenye rangi isiyofanana na rangi ya chama chake.
"Hata wauzaji unakuta ni wakereketwa wa vyama kama ni mwanaccm huwezi kukuta akitumia kikombe chekundu, au kama ni mwanachadema huwezi kumkuta akipimia kikombe cha rangi nyekundu kwahiyo rangi hizo wanazitumia kama kueneza vyama vyao" amesema Rebeka.
Ubaguzi wa rangi haupo tu kwenye vikombe upo pia kwenye mifuko maarufu mifuko ya Magufuli ambayo nayo baadhi ya wateja wamekuwa wakibagua rangi wanapofika dukani huchagua rangi ya kijani na nyekundu.
Fredi Hamis mfanyabiashara wa dagaa soko la Rebu amesema" Sio tu vikombe hata hii mifuko ya Magufuli wateja wakija wanabagua, ukitaka kumpimia dagaa huyu atakwambia nataka mfuko mwekundu mwingine atakwambia niwekee kwenye mfuko wa rangi ya kijani inabidi ufanye vile mteja anataka ili usikose pesa" amesema Fredi.
Nyagone Mwita mfanyabiashara mwenye duka la bidhaa za jumla amesema mifuko hiyo ubaguliwa kutokana na rangi za timu za mchezo wa mpira kati ya Simba na Yanga.
" Watu wanataka rangi kulingana na mapenzi na timu yake au chama chake, sisi kwakuwa ni wafanyabiashara tunasaka pesa tunalazimika kuwa na rangi zote iwe blue, kijani, nyekundu au rangi zingine maana wapo wengine siyo wanasiasa au wafuasi wa Simba na Yanga hawachagui rangi wanatumia rangi yoyote." amesema Nyagone.
Wananchi hao wamesema suala la ubaguzi wa rangi nyekundu na kijani ni la kawaida katika Wilaya hiyo kwakuwa baadhi ya wananchi ni wafuasi wa CCM na CHADEMA vyama vyenye nguvu kubwa Tarime pamoja na mashabiki wa timu ya Simba na Yanga hivyo wanakubalinana na mazingira hayo ya ubaguzi wa rangi kwakuwa ni jambo la kawaida kwa Tarime.
Wanawake wakiwa sokoni wakiuza maharage
Post a Comment