HEADER AD

HEADER AD

WANANCHI WANUNUA NG'OMBE WALIOGONGWA NA LORI KWA 50,000

Na Dinna Maningo, Tarime

BAADHI ya Wananchi wa Kijiji cha Surubu Kata ya Komaswa Wilaya ya Tarime Mkoani Mara, wamenunua ng'ombe waliojeruhiwa kwa kugongwa na Lori kwa bei ya Tsh 50,000 -100,000 kila mmoja huku wengine wakichukua ng'ombe waliokufa kwa ajili ya kitoweo.

Licha ya Mahakama kutoa kibali cha kuteketeza mifugo iliyokufa iliyogongwa na Lori Kijijini hapo katika barabara ya lami ya Mwanza- Sirari, wananchi wamegomea kibali hicho na kugawana nyama kwa ajili ya kitoweo huku mifugo yenye majeraha wakiinunua kati ya Tsh. 50,000  hadi 100,000.

DIMA ONLINE ilipowauliza kwanini wanachukua nyama ambayo ni ng'ombe waliokufa wengine huita nyamafu au kibudu ambayo kwa taratibu za kiafya haziruhusiwi kuliwa wamesema;


"Wengine nyama tunaila wakati wa sherehe au mgeni akikutembelea, maisha ni magumu hata kupata pesa ya kununua nyama ya ng'ombe kilo moja Tsh 7,000 ni tabu, alafu tuangalie kabisa ng'ombe wakiteketezwa hii haikubaliki, sisi wakurya baadhi yetu tunakula vibudu tumekataa hicho kibali cha Mahakama tumezichuna na kugawana nyama tunaenda kupika tule.

Mwananchi mwingine amesema" Mwandishi kwani hizo nyama mnazonunua buchani na kula huwa zipo hai ?zote huwa zinachinjwa zinakufa alafu watu wanakula nyama, ng'ombe haliwi akiwa mzima analiwa akiwa tayari amekwisha kufa kwahiyo sioni ubaya sisi kula nyama ya ng'ombe aliyekufa wengine watazikausha watakula.

"Ukitaka kuchinja ng'ombe unatumia panga kumuuwa ili afe kisha uchukue nyama yake na hawa ng'ombe wamechinjwa kwa kutumia taili la Lori utofauti ni ule hii imekufa kwa panga na hii imekufa kwa Lori kwahiyo nyama zinazoliwa zote ni za ng'ombe waliokufa" amesema mwananchi mmoja.

Chacha Marwa amesema ng'ombe walio na majeraha wananchi wamewanunua kati ya Tsh. 50,000 hadi 100,000 kutegemea na ukubwa wa ng'ombe na  wengine wamepeleka kuuza nyama kwenye bucha .


Wakizungumzia tukio la ng'ombe kugongwa na Lori,  Ryoba Chacha amesema" ilikuwa Tarehe 11, mwezi huu mida ya saa 12 jioni kuelekea saa moja, Ng'ombe walikuwa wanatoka malishoni wakati wanavuka barabara ya lami Mwanza-Sirari eneo la kivuko cha Ng'ombe wakagongwa wengine wakafa hapohapo na wengine wamevunjika miguu hawatembei.

"Tunaomba mwenye ng'ombe alipwe mifugo yake, lile eneo walikogongwa kuna kibao kimechorwa ng'ombe na kuna alama zimeoneshwa unatakiwa kutembela km ngapi ukifika hilo eneo, alama za barabara zinakutaka upunguze spidi dereva alikuwa spidi hakujali alama za barabarani.

" Wengine wanasema hakuna kesi eti kivuko cha ng'ombe kinatumika mwisho saa kumi na mbili jioni ikifika saa moja hakitumiki tena, ng'ombe wamevuka saa moja kasoro, inamana kivuko cha watembea kwa miguu nacho kinatumika mwisho jioni!  "amesema Ryoba. 

Joseph Matiko amesema" Tunasikia wanamshawishi mwenye ng'ombe eti wayazungumze wamlipe wayamalize kesi isiende mahakamani, kwamba ikienda mahakamani mwenye ng'ombe atalipwa kwa viwango vya serikali ambavyo ni pesa kidogo eti bora wamalizane tu kijijini, sijui kama ni kweli mahakama hulipisha fidia kidogo?.


" Ili kuonesha utekelezaji wa sheria ya usalama barabarani na uharibifu wa mali, kesi iende mahakamani ili iwe fundisho kwa madereva wasiozingatia sheria za usalama barabarani, kama huko mahakamani fidia ni kidogo basi ndio maana matukio ya ajali za barabarani hayaishi kwakuwa wanajua hata wakikamatwa watalipa faini kwakuwa fidia ni kidogo na wataachiwa"amesema Joseph.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Surubu Tabhora Machera amesema ng'ombe hao ni mali ya Mseti Nyamhanga waligongwa wakivuka kwenye kivuko cha ng'ombe na anaiomba Serikali iingilie kati mwanakijiji wake apate haki," Tukio lilitokea saa kumi na mbili jioni mvua ilikuwa inanyesha ikiwa na upepo mkali.

"Ng'ombe walikuwa wanatoka malishoni wakiwa wanavuka kwenye kivuko cha mifugo barabara ya lami mpakani mwa kitongoji
cha Buguba na Komaswa, wengine walikufa palepale na wengine wamepata majeraha, dereva hakujali kuwa kuna mvua ya upepo ambapo alipaswa kupunguza mwendo, Lori lipo kituo cha Polisi". amesema Tabhora.

Mseti Nyamhanga ambaye pia ni mfanyabiashara wa ng'ombe aliyegongewa mifugo yake na mingine kufa amesema tayari jambo hilo linashughulikiwa na Serikali.


Awali akizungumza na DIMA ONLINE Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Dkt. Joseph Marwa aliyefika eneo la tukio, amesema Desemba, 11,2022 katika barabara ya lami ya Mwanza -Sirari, ng'ombe 39 waligongwa na Lori lililokuwa likitokea Sirari.

Amesema kati ya ng'ombe hao, 13 walifia eneo la tukio, ng'ombe 10 wana hali mbaya ni wa kuchinjwa, ng'ombe 16 wana majeraha yanayoweza kutibika na kwamba tayari Mahakama imetoa kibali cha kuruhusu kuteketezwa mifugo iliyokufa.


"Ng'ombe waliovunjika miguu hawawezi kusimama na ng'ombe akilala zaidi ya saa 48 huyo ng'ombe hawezi kuendelea, ng'ombe 16 wanaendelea na matibabu walipata majeraha madogo yanayoweza kutibika.

"Ng'ombe 10 hai wana majeraha makubwa matibabu yake ni makubwa sana wanaweza kuchinjwa nyama yake ikatumika kuliwa haina shida, mf. ng'ombe kavunjika tu miguu ni hai huwezi sema kuwa hawezi kuliwa, hiyo itachinjwa utatumia zile sehemu zisizo na majeraha," amesema.

Kuhusu ng'ombe 13 waliokufa amesema" Tumeshachukua vielelezo na kibali kutoka mahakamani cha kuteketeza hiyo mifugo iliyokufa lakini pia imsaidie huyo aliyegongewa mifugo hata kama akifungua kesi, ile ni Traffic kesi, Dereva alikamatwa pamoja na Lori, Lori lilikuwa kubwa na mifugo yote ni ya mtu mmoja amesema ", Joseph.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi Tarime Rorya, ACP Geofrey Sarakikya amesema gari lenye namba za usajili T 578 DPN aina ya Scania  Lori lilikuwa likisafirisha mzigo wa biashara kutoka Tarime kwenda mkoa wa Dar es Salaam, likiendeshwa na dereva ambaye hakumtaja jina.


"Ng'ombe 13 wamekufa, ng'ombe 10 wana majeraha na ng'ombe wengine ni wazima hawana majeraha, Mahakama imetoa amri waliokufa wateketezwe na walio na majeraha wakabidhiwe kwa mlalamikaji waendelee na matibabu, mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani" amesema ACP Geofrey.

Hata hivyo wananchi wa Kijiji cha Surubu wametoa pole kwa mwanakijiji mwenzao na wameipongeza Serikali hususani Wataalamu wa mifugo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na ngazi ya Kata pamoja na Askari Polisi kufika kwa wakati kwenye eneo la tukio, wanaiomba Serikali kumsaidia mwanakijiji huyo kupata haki ya mifugo yake.





No comments