VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA VYATAKIWA KUTENDA HAKI.
Na Dinna Maningo, Tarime
CHAMA cha ACT Wazalendo Mkoa wa Mara kimevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutenda haki pasipo kuegemea upande wowote wa Chama cha Siasa pindi vinapokuwa vinaimalisha ulinzi na usalama katika mikutano ya hadhara.
Imeelezwa kuwa katika mikutano ya hadhara kumekuwepo na uonevu na upendeleo unaofanywa na baadhi ya viongozi wa Serikali wakiwemo wa Jeshi la Polisi, Wakuu wa Wilaya na Mikoa kukipendelea Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuminya uhuru wa mikutano kwa vyama vya upinzani jambo ambalo linasababisha wao kuwa sehemu ya kuchangia kuwepo kwa fujo na vurugu katika mikutano ya hadhara.
Akizungumza na DIMA Online Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo mkoa wa Mara na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho, Charles Mwera Nyanguru aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na baadae kuhamia ACT Wazalendo amesema vyombo vya ulinzi na usalama vifanye wajibu wao kwa kusimamia Sheria za nchi na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Vyombo vya ulinzi na usalama vilinde mikutano kwa haki, mkoa wa Mara tuna ma RPC wawili, majeshi yao yalinde mikutano wasigeuke kuwa wanasiasa, Viongozi wa Serikali watende haki katika mikutano ya hadhara, tunajua baadhi yao ni makada wa CCM na ni wajumbe Kwenye vikao vya CCM kama Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mkoa.
"Wapo wengine wametoka kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, wengine ni wanajeshi ambao ni makada wa CCM, mambo yakutumiana vimemo na kuingilia mikutano kama tulivyoona kwenye mikutano iliyopita waache mikutano iwe huru" amesema Charles.
Charles ameongeza kusema" Viongozi walinde wananchi na nchi sio kugeuka kuwa wanasiasa na kufanya uonevu, nchi zingine wanajeshi hawapewi ukuu wa Wilaya wala ukuu wa mkoa kazi yao ni kulinda nchi maana nafasi hizo ni za kisiasa , DC, RC ni mjumbe kwenye vikao vya CCM unategemea atakuwa na usawa katika maamuzi ?.
"Wananchi hawawezi kufanya fujo kama mikutano inafanyika kwa haki, wao kazi yao ni kusikiliza hoja na kueleza kero zao lakini mkutano huo usiposimamiwa kwa haki inasababisha kuzuka kwa vurugu, kwahiyo nasisitiza vyombo vya ulinzi na usalama vitende haki"amesema Charles.
Akizungumzia kuondolewa kwa zuio la mikutano amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ametekeleza matakwa ya Katiba huku akivitaka vyama vya upinzani kushirikiana pamoja bila kubaguana.
" Mikutano ya hadhara ni haki ya kikatiba, aliyekuwa Rais Hayati John Pombe Magufuli alivunja katiba kwa miaka mitano, akaja Rais Samia nae akavunja kwa mwaka mmoja, wakati mikutano imezuiliwa Rais Samia alikuwa ni Makamu wa Rais na wasaidizi wake walishiriki vikao hivyo vya zuio la mikutano, ile siku ya kwanza anaapishwa alipaswa kuondoa marufuku hiyo lakini nae akatukandamiza" amesema.
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Jimbo la Tarime Mjini Didas Nchama Makaranga amelitaka Jeshi la Polisi kusimamia haki kwa kile alichosema kuwa baadhi ya vyama vya siasa wanapokwenda kutoa taarifa za kufanya mikutano huzuiliwa na wakati mwingine taarifa ugeuzwa kuwa kibali.
"Unapotaka kufanya mkutano unawenda Polisi kutoa taarifa ili mkutano wako ulindwe, lakini unapofika kutoa taarifa chenga zinaanza mara unaambiwa kuna kiongozi anakuja wakati eneo kunakofanyika mkutano ni mbali na anapokwenda huyo kiongozi.
"Inafika wakati inakuwa sio tena taarifa ni kibali na kibali kuna kukubaliwa au kukataliwa, matokeo yake ukifanya mkutano mnafungiwa kwamba hamkuwa na kibali cha kufanya mkutano wakati kazi yako ilikuwa ni kuwapa tu taarifa." amesema Didas.
Kiongozi huyo amepongeza Rais Samia kwa kuondoa zuio na kusema kuwa kutofanyika mikutano ya hadhara kuliwanyima haki wananchi kusema kero zao kupitia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na ilileta athari kwa vyama kutovuna wanachama wapya.
Pia Katibu wa ACT Wazalendo Jimbo la Tarime Mjini Ibrahim Sengamgoda amesema vyama vya siasa vina kamati zao za ulinzi na usalama ambazo ushirikiana na jeshi la Polisi kuhakikisha mikutano inafanyika salama kwa amani.
"Siku za nyuma jeshi la Polisi lilikuwa halitoi ushirikiano kwa vyama vya upinzani, ulikuwa unapewa ruhusa ya kufanya mkutano lakini wakati mpo kwenye vikao vikiwemo na vya ndani unashtukia Polisi wamefika wanawazuia kuendelea na mikutano na wakati mwingine mnakamatwa yaani kama vile wamepewa maelekezo" amesema Ibrahim.
Katibu huyo amempongeza Rais Samia Suluhu kwa kuondoa marufuku ya mikutano na kusema kuwa mikutano ya hadhara ya kisiasa inasaidia kutoa elimu ya uraia na wananchi kuvifahamu zaidi vyama vya siasa.
Naye Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Jimbo la Tarime Vijijini Yohana Nyangi Mwikwabe amesema kazi ya Jeshi la Polisi ni kulinda raia na mali zao na kwamba vyama vya siasa ni mali ya Tanzania hivyo hawategemei kuona Polisi wakitoa vitisho, mabomu.
Ameongeza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vina haki ya kushiriki kwenye mikutano ya hadhara kuhakikisha ulinzi na usalama unaimalika lakini pia kusikiliza, kufahamu kile kinachozungumzwa kwenye mikutano ili yaweze kufanyiwa kazi.
Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa huo wa Mara Charles Mwera amesema chama hicho kipo kwenye maandalizi ya kupanga ratiba za mikutano na baada ya kukamilika kitafanya uzinduzi wa mikutano.
Post a Comment