HEADER AD

HEADER AD

JAJI MFAWIDHI : KINACHOANGALIWA NI USHAHIDI NA SI FEDHA

Na Jovina Massano, Musoma.

WANANCHI mkoani Mara wametakiwa kuondoa fikra ya ununuzi wa haki pindi wanapokuwa na mashauri mahakamani.

Hayo yamesemwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Musoma Fahamu Mtulya January 29,2023 alipokuwa akitoa elimu ya sheria katika maonyesho ya wiki ya Sheria kuelekea kilele cha Sheria February 1 mwaka huu.

         Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Musoma Fahamu Mtulya.

Amesema kuwa kuna wananchi wana mawazo kwamba lazima uwe na fedha ili upate haki au kuna ubaguzi kwa mtu mwenye hela na asie na hela na kwamba hakuna mahusiano ya fedha na haki katika mahakama kuanzia ya mwanzo hadi mahakama kuu kwakuwa kinachoangaliwa ni ushahidi unaoletwa kwa mahakimu na majaji kwenye utoaji wa hukumu.

"Lazima itambulike mahakama ni kama Taasisi nyingine yeyote ya Umma  wakati fulani unapofungua mashauri inaweza zikatakiwa ada mbalimbali  katika kuendesha mashauri ambayo yanatokana na madai.

    Washiriki wa maonyesho ya wiki ya Sheria walitunukiwa vyeti vya ushiriki

"Mashauri ya jinai hayalipiwi, hivyo nawaomba wananchi wasichanganye kesi za madai na za jinai na utaratibu huu wa malipo upo kwa mujibu wa Sheria"amesema Mtulya.

Kwa upande wake Agatha  Mwita mkazi wa Kyagata wilayani Butiama amesema kuwa kuna haja ya Taasisi hiyo ya  mahakama kutoa elimu ya kutosha kipindi cha maadhimisho ya Sheria ili kuondoa mkanganyiko wa uelewa wa utoaji haki na huduma za mahakama.

     Agatha Mwita mkazi wa Kyagata wilayani Butiama.

"Nawaomba wahusika wa mahakama zetu hapa nchini kutumia hata vikao vya kata na vijiji kutuelimisha juu ya sheria ili watusaidie sisi wananchi kupata uelewa wa kutosha kuhusu mahakama zetu"amesema Agatha. 

Ameongeza kuwa elimu pia itolewe juu ya sheria ya ardhi ili kupunguza na kuondoa kabisa migogoro ya ardhi kwa jamii.

Wananchi zaidi ya 4500 wameweza kupata elimu ya Sheria kutoka kwenye Taasisi 27 ambazo ni TRA, NSSF, PSSSF, NPS,OSG,CMA, USTAWI WA JAMII ,ULEKEBISHAJI TABIA(PROBATION), EWURA CCC ,TLS.

Taasisi zingine ni LEGAL AID, AFYA MKOA, TAKUKURU, NIC,NHIF, TCCIA, POLISI, ZIMAMOTO,UHAMIAJI, MAGEREZA, RITA,TWCC,TIGO, MAHAKAMA YA ARDHI,TCCIA na ARDHI Mkoa wa Mara.
               
         Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Musoma Fahamu Mtulya.







No comments