MKURUGENZI TARIME MJI ASEMA MWANDISHI WA HABARI NI MGANGA NJAA,MBABAISHAJI
>>>Ampiga Marufuku kwenda ofisini kwake
>>>Adai aliandika habari na kupiga picha za uongo za ujenzi wa vyumba vya madarasa
Na Mwandishi Wetu, Tarime
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Tarime Mkoani Mara, Gimbana Ntavyo amekataa kuhojiwa na Mwandishi wa Habari wa DIMA Online Dinna Maningo kwa madai kuwa aliandika habari na kupiga picha za uongo za ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Mkurugenzi huyo wa Halmashauri badala ya kumsikiliza mwandishi huyo kujua sababu za kufika ofisini kwake alianza kumtolea maneno makali akimlaumu kwamba anaandika habari za uongo huku akisema ni mwandishi mganga njaa ambapo aligoma kumsikiliza na kukataa kuhojiwa na amempiga marufuku kwenda ofisini kwake.
Mwandishi huyo alifika ofisini kwake Februari, 2, 2023 majira ya saa 2:55 asubuhi ili kuzungumza nae kupata ufafanuzi katika habari aliyokuwa akiifuatilia kuhusu mafanikio na changamoto katika shule ya msingi Magufuli ya Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum iliyopo Kata ya Nyamisangura katika Halmashauri hiyo.
"Leo umepata nafasi ya kuja maana kipindi kile uliandika kwamba ulikosa nafasi ya kuja, ulikuja hukunikuta? ulikuta ofisi haina Mkurugenzi?, taarifa yenyewe umeiripoti sijui ilikuwa jumatatu picha umepiga jumapili hiyo jumapili ofisi zinakuwa wazi? alafu unasema hukumkuta Mkurugenzi.
"Unaandika kwa kujifurahisha hata kama nimesafiri ofisi yangu haikosi kuwa na mtu ofisini, sasa hapa umekuja kufanya nini mwandishi wa habari za kubabaisha tu, waganga njaa tu".Amesema Mkurugenzi Gimbana.
Mwandishi huyo alimjibu kuwa alifika ofisini kwake na akaambiwa yupo safari hivyo hadi atakaporejea hivyo mwandishi aliendelea kutimiza majukumu yake ya kila siku ya utafutaji habari na upigaji picha za habari.
"Bahati mbaya umeumbuka umeandika vitu vya uongo, bahati nzuri Waziri alikuwa hapa amekuja kuangalia akakuta vitu ulivyoviandika ni vya uongo, amekuta majengo yamekamilika tofauti na ulichokiandika wewe.
"Uliandika uongo kwamba havijaezekwa umeandika uongo kwasababu amekuja akakuta vimeshaezekwa acha mambo yako umekuja kunihoji nini nenda ukaandike unachojua wewe kama ulivyozoea wala sitaki kuhojiwa na wewe, wewe sio mwandishi wa kwanza kuniandika" amesema Gimbana.
Shule ya msingi Magufuli ni shule inayotoa elimu ikijumuisha makundi ya Wanafunzi wenye Ulemavu wa Akili, wasio na uwezo wa kuona pamoja na wenye ulemavu wa kusikia.
Desemba, 19, 2022 DIMA Online iliripoti habari yenye kichwa cha habari " TARIME TC YASHINDWA KUTEKELEZA AGIZO LA NAIBU WAZIRI TAMISEMI ikiwa na picha za ujenzi wa vyumba vya madarasa iliyoandikwa na Mwandishi huyo ambayo imeonekana kumchukiza Mkurugenzi huyo.
Mwandishi wa Habari Dinna Maningo ni miongoni mwa baadhi ya Waandishi wa Habari Mkoani Mara walioshiriki mafunzo ya uandishi wa Habari za Elimu kupitia "Mradi wa Shule Bora" mwishoni mwa mwaka 2022 unaotekelezwa na Serikali katika baadhi ya mikoa hapa nchini ukiwemo mkoa wa Mara.
Mafunzo hayo yalitolewa na Serikali kupitia wakufunzi kutoka TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Elimu Mkoa wa Mara, yaliyowakutanisha Maafisa Habari wa Serikali ndani ya mkoa huo na baadhi ya Waandishi wa Habari Mkoani Mara.
Katika mafunzo hayo Waandishi wa Habari walisisitizwa kuandika habari za mafanikio na kuibua changamoto zinazohusu elimu.
Mradi huo umelenga kutatua changamoto za kielimu hapa nchini ambao umejikita katika vipaumbele vinne muhimu ambavyo ni kujifunzia (Wanafunzi), Kufundishia (Walimu), Elimu jumuishi kwa wanafunzi wa hali zote na uimarishaji wa shule.
Lengo ni kuhakikisha Elimu ya awali, msingi na sekondari inaboreshwa, mazingira rafiki, usawa wa kijinsia ili wanafunzi wapate elimu bila vikwazo.
Post a Comment