WASANII WA MUZIKI KUTOKA NCHI MBALIMBALI KUTUA ZANZIBAR
Na Andrew Chale, Dar es Salaam.
TAMASHA kubwa la Kimataifa la Muziki la Sauti za Busara ambalo kwa mwaka litakuwa ni la 20 linatarajiwa kulindima katika viunga vya Ngome Kongwe Zanzibar ambalo litawashirikisha wasanii kutoka mataifa mbalimbali.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mapema Januari, 31,2023 Jijini Dar es Salaam katika Kituo cha Utamaduni cha Ufaransa Alliance Francie Dar (AFDAR)Meneja wa Tamasha hilo, Journey Ramadhan amesema Tamasha hilo litakuwa na wanamuziki mashuhuri kutoka nchi mbalimbali.
Meneja huyo amewataja wasanii watakaoshiriki ni pamoja na Tiken Jan Fakoly kutoka nchi ya Ivory Coast ambaye ni nyota wa Reggae barani Afrika ambaye maneno yake yanatoa wito kwa Umoja Afrika kuimarika kiuchumi, kisiasa na Kitamaduni.
"Mwimbaji wa singeli Mzee wa Bwax toka Tanzania na Patricia Hillary na Wasanii wengine wa kimataifa wakiwemo kutoka Afrika Kusini, Sudan/Misri , Zimbabwe, DRC/Canada, Ethiopia/Italia na Senegal na kwingineko.
Naye Mkurugenzi wa tamasha hilo Yusuf Mahmoud amesema maandalizi yote yameenda vizuri zikiwa zimebakia siku chache pekee.
"Sauti za Busara 2023,ni msimu wa 20, litafanyika Februari 10 hadi 12 visiwani Zanzibar, limekuwa jukwaa la uzinduzi wa kazi ambalo limewavutia wasanii wengi wanaokuja katika eneo hilo na kupata fursa za utalii wa kimataifa." Amesema Yusuf.
Aidha amesema licha ya changamoto nyingi tangu lianze mwaka 2003 Sauti za Busara limebakia kuwa moja ya tamasha moto kwenye kalenda ya kitamaduni ambayo washereheshaji wanatazama kila mwaka ambapo mwaka huu linaadhimisha miaka 20 ya kuonyesha muziki bora wa kiafrika.
“Katika miongo miwili iliyopita tumebarikiwa kuwa na eneo la kihistoria na la kipekee na safu ya kuvutia ya wasanii ambayo iliacha kumbukumbu za kudumu kwa kila mtu aliyehudhuria.
"Tumeendelea kubakia kwenye asili ya kudumisha tamaduni tajiri na tofauti za Baraza la Afrika, ” kaulimbiu ya mwaka huu ni “Tofauti Zetu Utajiri Wetu:Utofauti Wetu ni Utajiri Wetu,” amesema Yusuf.
Ameongeza kuwa wakati wa kupanga programu wanahakikisha kuwa kila wakati vijana, wanawake na wasanii waliotengwa wanajumuishwa pamoja na wasanii wa kipekee wanaowawakilisha Kaskazini, Kusini, Mashariki na Kati.
“Wasanii wengi waliotumbuiza kwenye jukwaa la Sauti za Busara wamekwenda kualikwa kwenye matamasha mengine barani Afrika na kwingineko, baadhi ni Siti &The Band na Tausi Women’s, Taarabu kutoka Zanzibar, Madalitso Band kutoka Malawi, Sarabi kutoka Kenya, Msafiri Zawose, Wamwiduka Band, Jagwa Music kutoka Tanzania na wengine wengi” Amesema Yusuf.
Post a Comment