KANISA LA OMIC KUFUNGUA KITUO CHA WATOTO YATIMA
Na Mwandishi Wetu, Karagwe.
KANISA la kimataifa lijulikanalo kama One tree Mission International (OMIC) lililopo kata ya Kiruruma wilaya ya Karagwe mkoani Kagera linatarajia kufungua kituo cha watoto yatima ili kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu.
Askofu wa Kanisa hilo mkoa wa Kagera Goerge Mbandwa ameyasema hayo Januari 18,2023 baada ya zoezi la kugawa mavazi kwa watu wasiojiweza, watoto yatima na wenye ulemavu, zoezi lililofanyika Kanisa la Biyungu kata ya Kiruruma wilaya ya Karagwe.
Amesema katika kanisa la Biyungu kuna kituo cha uamsho kinachoshirikisha waumini wa madhehebu mbalimbali ambao hushiriki kujifunza neno la Mungu na kuifikia jamii katika kuwapa mahitaji ya lazima na kwamba ndani ya mwaka huu wanatarajia kuanza maandalizi ya kujenga kituo cha watoto yatima.
"Katika kituo chetu cha uamsho Biyungu ambacho wanashiriki waumini wa madhehebu mbalimbali tunayo malengo matatu, kufundisha neno la Mungu, kusaidia jamii kutoa mahitaji muhimu na mpango wa kujenga kituo cha watoto yatima ambapo kwa sasa tunagharamia mahitaji ya shule ya mtoto wa kike darasa la kwanza aliyefiwa wazazi wake" Amesema Askofu Mbandwa
Ameeleza kuwa, zoezi la ugawaji mavazi lilishafanyika pia mwaka jana na wanatarajia kuanza kutoa mahitaji ya chakula huku akiiomba jamii yenye uwezo wa kusaidia watu wenye mahitaji maalum kufanya hivyo ili waweze kuvuna thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Bernadol Rwabusisi ni miongoni mwa wazee waliopata msaada wa mavazi amesema kuwa, anashukuru kwa msaada huo kwani alikuwa hana nguo wala viatu vya kuvaa.
Jovina Feresian mwenye ulemavu wa macho amesema kuwa, wakati mwingine amekuwa akilazimika kuazima nguo ili atoke kwenda sehemu kwenye Jamii hivyo akashukuru Kwa msaada huo.
Katika tukio la ugawaji mavazi watu zaidi ya 150 walipata msaada huo wakiwemo wazee, wajane,wagane, wenye ulemavu na watoto yatima na nguo na viatu zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 1.5 zimegawiwa kama msaada kwa watu hao.
Post a Comment