WALIORIPOTI KUANZA KIDATO CHA KWANZA NI ASILIMIA 22.7
IMEELEZWA kuwa asilimia 22.7 ndiyo wameripoti kuanza masomo ya kidato cha kwanza tangu kufunguliwa kwa shule Januari, 09, 2023 kwa mwaka wa masomo 2023 katika mkoa wa Simiyu.
Akizungumza katika kikao cha mapitio ya tathmini ya utekelezaji wa shughuli za uboreshaji na usimamizi wa elimu kwa mwaka 2022 na mwaka 2023, Afisa Elimu katika mkoa humo Mwl. Majuto Njanga amesema wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza ni 32,814 ambapo katika wiki ya kwanza wameripoti 7,272 sawa na asilimia 22.7.
"Kazi kubwa tunayofanya ni kuhamasisha jamii kuhakikisha wanafunzi wote ambao wamechaguliwa wanafika shule kwa muda unaotakiwa na tayari tumetoa taarifa kupitia vyombo vinavyohusika kwa kushirikisha vyombo vya ulinzi, Serikali za kijiji na kata kuhakikisha watoto wanafika shule" amesema Njanga.
Ameongeza kusema" Tunataka watoto wote wafike shuleni pasiwe na changamoto itakayowazuia kama ni sare za shule hana aende na zile za msingi wakati wazazi/ walezi wanaendelea kuwajibika kuwatafutia, tunatoa rai kwa wazazi wale wote ambao wataonekana wanasita pasipo na sababu kuwapeleka watoto shule basi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao" ameongeza.
Wadau wa elimu mkoani Simiyu wakiwa katika kikao cha mapitio ya tathmini ya utekelezaji wa shughuli za uboreshaji na usimamizi wa elimu kwa mwaka 2022 na mwaka 2023.
Mwakilishi wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, kutoka ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI) Mwalimu Suzana Nyarubamba amesema mkoa huo unapaswa kuchukua hatua madhubuti ili uweze kufanya vizuri kitaaluma kwani kwa sasa ufaulu mkoani humo umeshuka.
Paulina Nkwama ambaye ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) amesema ni vema kuhakikisha wanafunzi wanamaliza mzunguko ikiwa sambamba na kuhakikisha wanafunzi wanaoandikishwa kujiunga na elimu ya awali na darasa la kwanza na waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanaripoti shule.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu, mkuu wa wilaya ya Bariadi, Lupakisyo Kapange amewataka wazazi/walezi wote wenye watoto wanaopaswa kwenda shule kuwapeleka mara moja.
"Mkoa huu ni wa kichungaji wanaamini kwamba mtoto akienda kuchunga mifugo anakuwa amefanya tija ndani ya familia wanaamini kwamba wakiozesha mtoto wa kike ng'ombe 20 wanakuwa wamefaidika ndani ya jamii, sisi mkoa wa Simiyu hatukubaliani na hili.
"Hakuna mwanafunzi ambaye hatohudhuria darasani wanafunzi wote waliofaulu wanatakiwa kuwa shule.Walimu wetu wana utayari wa kufanya kazi, Rais ametujengea madarasa 239 mkoani kwetu, wote waliofaulu waende shule." amesema Kapange.
Post a Comment