HEADER AD

HEADER AD

MADIWANI WACHARUKA KADI ZA WAJAWAZITO, WATOTO KUUZWA


Na Daniel Limbe, Biharamulo

BARAZA la Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, limelalamikia vitendo vya baadhi ya wauguzi kuwauzia kadi za kliniki wajawazito na watoto wanaozaliwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa umma Tsh 3,500 -5,000 na zilizodurufiwa Tsh 200.

Ni baada ya Diwani wa kata ya Nyarubungo, Petro Kiziluja, kulieleza baraza hilo malalamiko aliyopokea kutoka kwa baadhi ya wazazi waliokwenda kujifungulia kwenye hospitali ya wilaya ya Biharamulo ambapo walitozwa kiasi cha shilingi 200 kwaajili ya kupewa kadi za kliniki zilizo durufiwa(photo copy).

Kauli hiyo imeonekana kuwakera madiwani hao ambao wamedai hakuna haja ya kuendelea kufumbia uozo huo kwa baadhi ya wauguzi wanaochafua taswira ya wilaya hiyo kwa maslahi yao binafsi.

Diwani wa kata ya Kalenge,Erick Method, akashauri kukomeshwa kwa vitendo hivyo kwa kuwa kadi za maendeleo ya makuzi ya mtoto ni haki ya mama na mtoto na kwamba zinapaswa kutolewa bure kama mwongozo wa afya unavyotaka.

         Diwani wa kata ya Kalenge,Erick Method,akitoa ushauri wake baada ya kuibuliwa hoja ya wazazi kuuziwa kadi za klikini.

Malalamiko hayo yakaungwa mkono na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo,Leo Rushau ambaye amesema anayo malalamiko yanayo wahusu baadhi ya wauguzi wasio waaminifu ambao wamekuwa wakiuza kadi halisi za kliniki kwa bei ya Tsh. 3,500 kinyume cha sheria.

" Mimi mwenyewe ninazo taarifa za uhakika ambapo kwenye baadhi ya vituo vyetu vya kutolea huduma za afya wazazi wanauziwa kadi za kliniki kati ya shilingi 3,500 hadi 5,000...Mkurugenzi hata ukitaka nikupeleke sasa hivi utalishuhudia hili nalosema" amesema Rushau.

Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti huyo amewaagiza madiwani kuhakikisha wanawaripoti kwenye vyombo vya sheria wauguzi wote ambao wanajihusisha na uuzaji wa kadi za kliniki kinyume cha sheria ili kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa.

      Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya  Biharamulo,Leo Rushau,akitoa msimamo wa madiwani

Aidha Rushau, ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuhakikisha anafuatilia kwa haraka malalamiko hayo na iwapo kadi hizo hazipatikani iwekwe wazi ili kutafuta ufumbuzi wa jambo hilo kwa maslahi mapana ya afya ya mama na mtoto.

Mganga mkuu wa wilaya ya Biharamulo, Benedicto Ngaiza, amesema kuna uhaba mkubwa wa kadi za kliniki kwenye wilaya hiyo ambapo hakuzungumzia suala la wauguzi kuuza kadi hizo kinyume cha sheria za nchi.

      Madiwani wakiendelea kuchangia hoja za kikao.
                         

No comments