HEADER AD

HEADER AD

WASEMAVYO WANANCHI KUHUSU KUTOTANGAZWA SHULE BORA, MWANAFUNZI BORA

 


Na Dinna Maningo, Tarime 

BAADHI ya Wananchi Wilaya ya Tarime mkoa wa Mara wamesema kuwa kitendo cha Serikali kupitia Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kutotangaza shule bora na mwanafunzi bora kwa wahitimu wa Kidato cha nne mwaka 2022 kutashusha hamasa kwa wanafunzi na walimu huku wengine wakiunga mkono kutotangazwa.

DIMA Online imezungumza na baadhi ya wananchi kufahamu nini mawazo na mitizamo yao baada ya Baraza la Mitihani kustisha utaratibu wa kutangaza shule bora na mwanafunzi bora nao walikuwa na haya yakusema.

Mkazi wa mtaa wa Rebu shuleni Kata ya Turwa mwendesha pikipiki (bodaboda) Lucas Nyeika amesema " Serikali imekosea kutotangaza kufanya hivyo ni kutunyima haki ya kupata habari, tusipotangaziwa shule zilizofanya vizuri au zilizofanya vibaya sisi wananchi wa chini tutapataje hizo taarifa? wengine hatuna simu za tachi kwamba utafuatilia mtandaoni, tunasikiliza kupitia redio.

"Watangaze ili shule ijue imeshika nafasi ya ngapi lakini pia wananchi wana haki ya kujua kwenye Taifa lao ni shule zipi zinafanya vizuri na shule zipi zinafanya vibaya ili kama kuna mapungufu waongeze kasi ili nao baadae washike nafasi nzuri ".Amesema Lucus.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Ng'ereng'ere na mkazi wa Kijiji cha Ng'ereng'ere kata ya Regicheri, Bonphace Samwel amesema kutotangaza kutashusha hamasa kwa wanafunzi na motisha kwa walimu.

"Kustisha kutangaza wanafunzi walioshinda kitaifa ile hamasa kwa wanafunzi wenzake haitakuwepo kwasababu hajulikani ni nani, walipotangaza ilileta hamasa kwa wanafunzi kuongeza juhudi ili wawe kama mwenzao aliyeshinda kitaifa.

Amesema kutotangaza shule bora jitihada za walimu kufundisha zitashuka " Mwanafunzi aliposhinda nafasi bora Kitaifa na masomo husika ilikuwa inajulikana mwalimu aliyekuwa anafundisha ni nani, mwalimu wa somo husika ni nani na hakutakuwa na motisha kwa walimu watafundisha ilimradi."amesema Bonphace.

Ameongeza kuwa hamasa kwa wazazi itashuka " Mzazi aliposikia wanafunzi walioshinda kitaifa waliwahamasisha watoto wao kufanya vizuri, mfano mwanafunzi aliyekuwa bora hajatangazwa watu hawajui inakosesha hamasa kwa wazazi wengine.

Bonphace amesema Serikali inatakiwa kutafuta mbinu kujua kwanini shule za Serikali hazifanyi vizuri ikilinganishwa na shule binafsi na sio kutotangaza.

" Serikali inatakiwa kutafuta mbinu za shule zao kufanya vizuri hilo ndo wapambane nalo kujua nini ambacho Serikali hakifanyi hadi wanazidiwa na shule binafsi, mfano matokeo ya kidato cha sita shule za Serikali zinafanya vizuri kuliko za binafsi wajue wanakwama wapi matokeo ya kidato cha nne na shule za msingi"amesema.

Daniel Charles Mkazi wa Kijiji cha Matongo -Nyamongo amesema kutangazwa shule bora na mwanafunzi bora ni muhimu kwa sababu serikali imekuwa ikitangaza kuboresha elimu hivyo ni vizuri wananchi wakatangaziwa kujua  viwango vya ushindi kwa shule zao za serikali na binafsi.

                 Daniel Charles

"Waendelee kutangaza tuone je shule za serikali zina hatua gani, kutotangaza nikama vile serikali imeona namna ya kutozidhalilisha shule za serikali ukizingatia huwa inapata fedha za misaada za kuboresha sekta ya elimu.

"Inapoonekana shule binafsi zimeongoza inaonekana serikali haijaweka miundombinu rafiki kwenye shule za serikali, hakuna cha kutangaza biashara hata shule za serikali zikifanya vizuri nazo zitatangazwa.

"Shule za serikali zingefanya vizuri wananchi wasingekuwa wanapeleka watoto shule binafsi ambazo zina gharama kubwa, mtu anaacha cha bure anapeleka kwenye gharama anataka mtoto wake apate elimu bora". amesema Daniel.

Wananchi wengine wamesema serikali imewakosea kwa kutotangaza shule bora na mwanafunzi bora bila kuwashirikisha kutoa maoni yao na bila kufanya utafiti wa kina kujua faida na hasara ya uamuzi huo. 

"Suala la elimu ni la jamii wananchi wangeshilikishwa kwanza na tungeelezwa hasara za kutotangaza ni zipi lakini kusimamia hoja moja tu kuwa ni kutangaza biashara hiyo haina tija, mtu akifanya vizuri atangazwe na apongezwe, binafsi sioni hasara ya kutangaza shule bora na mwanafunzi bora maana inachochea zile shule ambazo hazijapata ushindi nazo  zizidi kufanya vizuri ili siku moja nazo zitangazwe.

Baadhi  yao wamesema serikali kutotangaza shule bora na mwanafunzi bora ni wivu kwa shule binafsi kwakuwa ndizo hufanya vizuri kwenye matokeo ya mtihani kuliko shule za serikali.

Mkazi wa mtaa wa Mwangaza Lucia Marwa amesema" Serikali isiseme kuwa imeacha kwasababu ni kutangaza biashara ikiri tu kuwa inaona wivu kwakuwa kila mwaka shule zinazoongoza kumi bora , wanafunzi bora ni za kutoka shule binafsi.

" Serikali inaona nikama inatangaza shule binafsi, hiyo sio njia ya kusaidia shule za Serikali kufanya vizuri ndo zitazidi kuporomoka maana hata zikifanya vibaya hazitatangazwa". Amesema Lucia.

Baadhi yao wameunga mkono kutotangazwa shule bora na mwanafunzi bora kuwa ilikuwa ni kuzitangaza kibiashara shule binafsi.

Marwa Sasi mkazi wa Kijiji cha Kewanja Kata ya Kemambo-Nyamongo amesema" Naunga mkono bora wastishe tu kutangaza  maana yalikuwa ni matangazo unakuta shule zilizoshinda karibia zote ni shule binafsi, kutangaza kule kukapelekea watu kuona shule binafsi ndio bora kumbe siyo ni kwasababu zenyewe zina wanafunzi wachache na zinamichujo kila darasa". amesema Marwa.

Perus Juma mkazi wa Nyamisangura amesema" Bora wastishe maana ilisababisha baadhi ya shule kuiba mitihani au walimu kuwaonesha wanafunzi majibu ili zipate ushindi na kutangazwa kwenye matokeo zionekane ndio zimefanya vizuri kumbe kiuhalisia si kweli" amesema.
Januari, 29, 2023 Serikali kupitia Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Athuman Salumu Amasi kupitia Vyombo vya Habari alisema Baraza la Mitihani limestisha utaratibu wa kutangaza shule bora na mwanafunzi bora matokeo ya kidato cha nne kwa wanafunzi waliofanya mtihani wa Taifa mwaka 2022.

Alisema utaratibu huo wa kutangaza shule bora na mwanafunzi bora ulikuwa unazitangazia biashara baadhi ya shule na kwamba hakuna tija kwani huwenda mazingira yao ya kusoma yalikuwa tofauti.


              Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Athuman Salumu Amasi





No comments