RAS MARA: UELEWA MDOGO SHERIA YA ARDHI UNAWAKOSESHA HAKI WANANCHI
Na Jovina Massano, Musoma
KATIBU Tawala mkoa wa Mara Msalika Makungu amewahimiza wananchi kutembelea mabanda ya maonesho yaliyopo uwanja wa Mukendo Manispaa ya Musoma waweze kupata elimu ya sheria na huduma mbalimbali zinazowahusu ili kuondokana na sintofahamu ikiwemo migogoro na ukatili.
Ameyasema hayo alipotembelea mabanda mbalimbali yakiwemo ya huduma za sheria na kubaini mwitikio mdogo wa wananchi wanaofika kupata elimu ilihali wananchi wengi wamekuwa wakifika katika ofisi ya mkuu wa mkoa kupeleka malalamiko ya migogoro ya ardhi inayowakabili.
Katibu Tawala mkoa wa Mara (Kushoto) Msalika Makungu akizungumza jambo
"Moja ya malalamiko makubwa tunayoyapokea ni migogoro ya ardhi kutoka kwa wananchi, elimu ndogo na uelewa mdogo wa sheria za ardhi zinawafanya kukosa haki zao, niwahimize wananchi kuitumia wiki hii kujifunza ili waweze kuondokana na adha wanazokutana nazo wakati wa kudai haki zao, amesema Msalika.
Katibu huyo hakusita kuongelea ukatili kwa watoto na akina mama ambapo ametolea mfano video iliyokuwa ikisambaa mitandaoni ikionesha mwanafunzi akiadhibiwa na mwalimu.
Akiwa katika banda la Mahakama linalosimania masuala ya mirathi,ndoa,talaka,na ukatili kwa watoto aliwahoji namna wanavyosimamia sheria hiyo ipasavyo.
"Adhabu aliyokuwa akitoa mwalimu iliyoonekana kwenye video clip huo ni ukatili mkubwa huwezi kumpiga mtoto kwa kumkanyaga hata angekuwa wa kwako huwezi kufanya ukatili kama ule" amesema Msalika.
Hakimu Mkazi Mahakama Kuu Musoma Donald Zephania ameongeza kuwa aliyesambaza video ile hakukosea amefanya vizuri kwani ameonesha uhalisia wa ukatili unaofanyika mashuleni kwa watoto bila hivyo jamii isingejua kama kuna ukatili wa namna hiyo unafanyika.
"Hapa sasa mzazi au mlezi anatakiwa ajitathmini kama anawajibika kufuatilia mienendo na maendeleo ya mtoto na mahusiano yao na walimu kwani hivi sasa wazazi wengi hawafuatilii watoto wakishanunua vifaa vya shule na sare za shule wamemaliza muda wa kuwa karibu na watoto ni mdogo wapo kwenye utafutaji zaidi ndio maana ukatili kwa watoto unaongezeka, amesema Donald.
Aidha amesema kuwa kuna sheria inayomlinda mtoto namba 21 ya mwaka 2009 ambayo ilifanyiwa marejeo mwaka 2019 inalenga kuimarisha ulinzi,mafunzo haki za watoto kupata mahitaji ya msingi kama chakula malazi,matibabu,chanjo ikiwemo na elimu.
Kwa upande wake Mwajuma Adam Mtundi, Muuguzi katika hospitali ya mkoa katika kitengo cha kuzuia udhalilishaji wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto amesema kuwa vitendo vya ukatili kwa watoto vinaongezeka hivyo kuna haja ya kuongeza kuielimisha jamii ili kuondoa vitendo hivi katika jamii.
"Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ni vingi tatizo lipo kwa jamii kutoelewa madhara ya ukatili, wengi wanafanya makubaliano bila kujua athari alizozipata mhanga wa tukio, niiombe jamii kutotumia njia za mkato kwa kufanya makubaliano na mtekelezaji kwa malipo kidogo bali wafuate utaratibu wa kisheria haki itendeke,amesema Mwajuma.
Ameongeza kuwa hivi sasa matukio ya ubakaji kwa watoto yanaendelea kuongezeka lakini pia kwa wakinamama wanaofanyiwa ukatili ambao hupokelewa na kupatiwa huduma kwa kushirikiana na watoa huduma wa Ustawi wa jamii.
Katibu Tawala wa mkoa huo ameongeza kusema kuna haja ya kutengeneza mawakala wa mabadiliko watakaotoa elimu na kukemea bila kutumia nguvu na jamii ikatoka kwenye janga la ukatili.
Post a Comment