HEADER AD

HEADER AD

MWERA: SERIKALI INAFICHA NINI KUTOTANGAZA SHULE BORA, MWANAFUNZI BORA?

Na Dinna Maningo, Tarime

IMEELEZWA kuwa kitendo cha Serikali kupitia Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kutotangaza shule bora na mwanafunzi bora katika mtihani wa Taifa wa Kidato cha nne 2022 huenda kinatokana na wivu au ibu kwa serikali kwakuwa kwa miaka kadhaa shule binafsi zimekuwa zikiongoza kufanya vizuri.

Akizungumza na DIMA Online Mdau wa Elimu na aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Charles Mwera Nyanguru ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo mkoa wa Mara, amesema hata Serikali isipotangaza bado walimu, wazazi watafuatilia kujua ni shule zipi zimefanya vizuri na zilizofanya vibaya na wanafunzi waliofanya vizuri.

"Eti Kiongozi wa Baraza la Mitihani anasema walipotangaza shule bora na mwanafunzi bora ilikuwa ni kuzitangazia biashara baadhi ya shule kwamba huwezi kushindanisha wakati zinatoka mazingira tofauti hii hoja haina mashiko.

"Basi kama ni hivyo na mitihani ya kitaifa itungwe kwa kuangalia mazingira tofauti ya shule na wanafunzi, mbona Serikali hutangaza mikoa maskini sasa kwenye matokeo inaona aibu gani kuweka wazi shule zilizofanya vizuri na wanafunzi bora ?huu ni wivu tu kwamba shule za serikali zinafanya vibaya hivyo wanaficha aibu ni muhimu kuwa na takwimu za kielimu.

"Serikali ambacho ingefanya ingekuwa inatenganisha inatangaza shule bora za kata kuanzia mshindi wa 1-10 kitaifa, shule za makundi maalumu mshindi wa 1-10 na shule binafsi mshindi wa 1-10 na wanafunzi bora kutokana na mazingira husika". amesema Mwera.

Mwera amesema kutangazwa kwa shule bora na mwanafunzi bora ilisaidia kufanya tathmini kujua hali ya kiwango cha ufaulu na iliteta motisha kwa walimu,wanafunzi na wazazi, na shule zingine zilizofanya vibaya zilijitahidi kufanya vizuri ili kuondokana na aibu ya kutangazwa kufanya vibaya.

          Charles Mwera Nyanguru

"Hatuwezi kwenda hivyo sasa tunazipimaje shule na wanafunzi? watangaze tujue shule zilizofanya vizuri na zilizofanya vibaya, mambo yawe wazi kutangaza ni kipimo cha ushindani, ndio maana Serikali inatangaza inaweka wastani waliofaulu na walioshindwa.

Serikali inapaswa kutafuta mbinu nzuri kuhakikisha shule za Serikali zinafanya vizuri kama mimi nilipokuwa Mwenyekiti wa Halmashauri mwaka 2007 tulisimamia elimu kuhakikisha wanafunzi wasio na uwezo wa ada wanakwenda shule, Halmashauri ikawa inawalipia ada wanafunzi wa Sekondari wakati huo ada ilikuwa ni 20,000.

" Hata nchi zingine kama Kenya wanatangaza shule bora, wanafunzi bora na wanasema katoka mazingira gani, mbona somo la Hesabu wamelitangaza kuwa limekuwa la mwisho na ndilo limefanya vibaya ! wameona ni kasoro kubwa, basi wangenyamaza wasiseme, kwani ukisema shule fulani imefanya vizuri na hii imefanya vibaya kuna kosa gani?.

Mwera amesema kuwa Serikali kutotangaza shule bora na mwanafunzi bora haisaidii kitu kwani wananchi wakiwemo, wazazi, walimu na wanafunzi wengi wanauelewa na wanamiliki simu za kisasa hivyo watafuatilia kupitia Tovuti na mitandao mingine kwenye simu zao na watazijua shule bora, wanafunzi bora na shule zilizofanya vibaya kwakuwa ulimwengu wa sasa ni wa kimtandao.

Amesema Baraza la Mitihani lilipotangaza shule bora ilikuwa rahisi Wazazi kuzijua shule na taaluma za shule na iliwasaidia wao kufahamu ni shule gani ampeleke mwanae kwani baadhi ya shule zinatoza gharama kubwa lakini kiwango cha ufaulu katika mitihani ni mdogo.

Mwera amesema Serikali imekuwa na utaratibu wa kuwashindanisha wanafunzi ambapo ilianzisha shule za vipaji maalumu lengo likiwa ni kutofautisha viwango vya kitaaluma kwa wanafunzi wenye uwezo zaidi na wale wenye uwezo wa kati na wa mwisho

Pia imekuwa ikiwachuja kupitia mitihani, wale wanaofaulu uchaguliwa kujiunga na sekondari na elimu ya juu na wanaofeli mitihani hawachaguliwi kujiunga na masomo ambao nao utangazwa na Baraza la Mitihani kupitia viwango vya kitaaluma vya wastani.

"Kwani shule binafsi zikitangazwa zimefanya vizuri kuna kosa gani? nao ni watanzania, watoto wanaokwenda shule za vipaji wengi wao wanatoka shule binafsi, wasiwaonee wivu kuona wanazidi wanaotoka shule za Serikali, wanapoficha kutangaza huwenda shule za Serikali zimefeli ndiomaana wameona haina tija kuzitangaza shule binafsi wakati zao hazijafanya vizuri" amesema Mwera.

"Hata huku kwenye jamii unakuta kuna ukoo masikini na ukoo tajiri na unawatambua kwa kuwapima kiuwezo na unapotangaza shule iliyofanya vizuri au vibaya unakuwa umewapima kiuwezo, tunaomba shule zilizofanya vizuri zitangazwe na zilizofanya vibaya zitangazwe kuanzia Kitaifa, Kimkoa na hata Kiwilaya kama haitaki na huko shuleni wasitangaze wanafunzi bora kwenye mitihani, mshindi wa kwanza hadi wa mwisho nao wasitangazwe ".Amesema Mwera.

Januari, 29, 2023  Serikali kupitia Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) Athuman Salumu Amasi kupitia Vyombo vya Habari alisema Baraza la Mitihani limestisha utaratibu wa kutangaza shule bora na mwanafunzi bora matokeo ya kidato cha nne kwa wanafunzi waliofanya mtihani wa Taifa mwaka 2022.

Alisema utaratibu huo wa kutangaza shule bora na mwanafunzi bora ulikuwa unazitangazia biashara baadhi ya shule na kwamba hakuna tija kwani huwenda mazingira yao ya kusoma yalikuwa tofauti.


Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) Athuman Salumu Amasi

No comments