SERIKALI YA KIJIJI YAKERWA ZAHANATI KUCHELEWA KUTOA HUDUMA
Na Dinna Maningo, Tarime
SERIKALI ya Kijiji cha Bisarwi Kata ya Manga, Wilaya ya Tarime Mkoa wa Mara, imeiomba Halmashauri ya Wilaya hiyo kukamilisha mapungufu yaliyopo katika Zahanati ya Kijiji ikiwemo ukosefu wa nyumba ya mganga, vitanda na kichomea taka ili iweze kutoa huduma kwa wananchi.
Pia imesema kitendo cha Mhandisi wa Halmashauri hiyo kutofika kwa wakati kukagua ujenzi kunarudisha nyuma spidi ya ukamilishaji wa Zahanati.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Bisarwi, Robert Mosonja amesema Mwezi Novemba na Desemba, 2022 walipokea dawa za Binadamu za Serikali kutoka Halmashauri hiyo na kwamba walitarajia itaanza kutoa huduma mapema mwezi huu lakini hadi sasa haitoi huduma.
Amesema ujenzi wa Zahanati ulianza mwaka 2012 kwa nguvu za wananchi na Serikali hatua ya ukamilishaji na kwamba bado ina mapungufu kadhaa, hakuna nyumba ya mganga, vitanda, kichomea taka, vifa, vifaa tiba, maji na umeme.
Robart amesema kusota kwa Zahanati bila kutoa huduma wananchi wanaendelea kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya Mtana takribani km.5 na Surubu takribani km.3.
"Zahanati imeanza kujengwa mwaka 2012 kwa nguvu za wananchi na Serikali hatua ya ukamilishaji, ina vyoo matundu mawili, Kijiji kina Kaya ya watu 750, ilikuwa imebaki milango imekamilika ila tunasubiri injinia aje akague ili ipachikwe lakini hajafika.
" Tulipokea dawa tangu mwezi Novemba,2022 zipo ndani, Zahanati haijaanza kwasababu milango bado haijapachikwa na bado kuna mapungufu mengine.
"Tunashangaa tunaambiwa eti tutengeneze kichomea taka sisi hatuna huo uwezo, tumetengeneza mabenchi ya kukalia tutengeneze meza pamoja na bankara la kutunza dawa hayo mengine ni ya Serikali tunaomba ikamilishe ili huduma ianze " amesema.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Makoro Juma Matinde amesema" Zahanati imekamilika tatizo ni injinia afike akague ili milango ipachikwe pia vifaa vinunulie huduma ianze "amesema.
Johanes Chacha Mjumbe wa Halmashauri ya Serikali ya Kijiji amesema" Wananchi walichangia nguvu kazi jumla Tsh.Milioni 45, Tsh Milioni 30, zikatolewa tena Milioni 10 kisha Milioni 5 ambazo ni fedha za Serikali kwa ajili ya ukamilishaji kama kuweka vioo,rangi, milango, sisi tulikuwa tunapokea tu vifaa.
Mganga Mkuu Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Joseph Mziba amesema sababu ya Zahanati kutokamilika kwa wakati ni tatizo la kimfumo la kifedha na kwamba Mhandisi ujenzi amechelewa kufika Kwenye Zahanati hiyo kutokana na kukagua miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.
"Kuna changamoto ya kimfumo fedha haijatoka unatamani utembelee vituo vya afya na Zahanati lakini unakosa mafuta, pia tulikuwa na ujenzi wa vyumba vya madarasa Mhandisi alikuwa akizungukia hiyo miradi, tutafika huko na miradi viporo itakamilishwa ili kupunguza changamoto" amesema.
Kuhusu kutokuwepo kichomea taka amesema" Kichomea taka kinawekwa kwa fedha za Serikali, tatizo fundi ni mmoja Wilaya nzima anakuwa na kazi nyingi ila tumejaribu kuongea na fundi aliyeko Mwanza akatuahidi kuja ndio tunamsubiri.
Ameongeza" Tutaweka vitanda, vifaa na vifaa tiba na huduma itaanza tunaomba wananchi watusaidie kutengeneza viti na meza pamoja na bankara kwa ajili ya kutunza dawa" amesema.
Ilani ya CCM
Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi CCM ya mwaka 2020-2025 Ibara ya 83 inasema lengo la Chama ni kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya njema ili kuwezesha kushiriki katika shughuli za ujenzi wa Taifa na kuboresha maisha yao.
Ilani inaeleza kwamba Chama kitaisimamia Serikali katika kutekeleza ikiwa ni pamoja na (a) kuimarisha huduma ya afya ya mama na mtoto na kuzitoa bila malipo ili kupunguza vifo vya akinamama, wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka 5.
(b) Kujenga na kuimarisha vituo vya kutolea huduma ya afya ili viweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.
Katika kuhakikisha mazingira ya watumishi wa afya yanaboreshwa Ilani hiyo Ibara ya 81 imeelekeza Serikali (a) kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa sekta ya afya kwa kuhakikisha kuwa kila kituo cha afya au Zahanati inayojengwa inakuwa na nyumba za watumishi.
Post a Comment