SERIKALI YAIPATIA BILIONI 6 KAMPUNI YA MBOLEA NCHINI
Na Mwandishi Wetu.Dar es Salaam
Ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha mbolea sahihi na bora zinawafikia wakulima wote kwa wakati na kwa bei nafuu, Serikali imeipa Mtaji wa Tsh. Bilioni 6 Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) ili isambaze mbolea ya ruzuku nchi nzima.
Taarifa hiyo imetolewa tarehe 27 Januari, 2023 Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde alipokuwa akizindua zoezi la usambazaji wa mbolea za ruzuku za TFC.
"Ni zaidi ya miaka nane (8) sasa imepita tangu TFC mara ya mwisho wasambaze mbolea kwa wakulima. Pongezi kubwa ni kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imedhamiria kwa dhati kuhakikisha kuwa TFC inasambaza mbolea kwa wakulima mpaka maeneo yote nchini hususani yale ambayo hayafikiwi na wafanyabiashara wengine.
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa TFC na inafahamu kuwa wanao mtandao mkubwa na madhubuti wa usambazaji wa mbolea nchini, hivyo anatarajia kuona wanatumia vizuri kufikisha mbolea hizo za ruzuku kwa wakati kwa wakulima wote nchini.
Naibu Waziri amesema mbolea si tu ni muhimu kwa wakulima katika kuongeza tija ya uzalishaji, bali pia ni mhimili mkubwa wa kuhakikisha nchi inazalisha zaidi na kuwa na uhakika na usalama wa chakula.
"Ninaamini kuwa, kupitia mikakati tunayoenda nayo sasa, hatutorudi tena tulipotoka miaka 8 iliyopita, na naitaka Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya TFC kufanya kazi kwa uweledi na uadilifu mkubwa" amesema.
Ameongeza kuwa Serikali imeanza utekelezaji wa miradi mikubwa nchi nzima ili kuwezesha Sekta ya Kilimo kukua kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, miradi hiyo ikiwemo na ujenzi wa Mabwawa mapya 14 ya umwagiliaji ambayo yatahifadhi maji takribani lita Bilioni 131 na kuhudumia zaidi ya hekta 90,000.
"Ni dhahiri kwamba mahitaji ya mbolea yataongezeka ili kuendelea kuzalisha kwa tija, niwaombe TFC mchangamkie fursa hii na kufanya biashara yenye tija na faida” Amesema Mavunde.
Awali akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi, Meneja Mkuu wa TFC Samuel Mshote ameishukuru Serikali kwa kuipa mtaji TFC na kuahidi kuwa yeye na Timu yake watasimamia ipasavyo mtaji huo ili waweze kufikia matarajio makubwa ya Serikali.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt. Stephan Ngailo amepongeza hatua zilizochukuliwa na Serikali za kuifufua TFC na kuipa mtaji ianze kufanya biashara, na kuongeza kuwa TFRA ipo tayari kuendelea kutoa miongozo thabiti ya Udhibiti ili TFC iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Dkt. Florence Turuka ameshukuru jitihada za Serikali kuipa nguvu tena TFC iweze kutekeleza majukumu yake ya msingi.
Ameahidi kuwa maeneo yote kwenye usambazaji wa mbolea ambayo yanakubwa na uhaba kutoka na ushindani wa kibiashara nchini, TFC ni chombo sahihi na atahakikisha kinakuwa msaada mkubwa kuondoa changamoto hizo.
Post a Comment