WANAWAKE ACT WAZALENDO WAVUTIWA NA UONGOZI WA RAIS SAMIA
Na Dinna Maningo, Tarime
NGOME ya Wanawake wa Chama cha ACT Wazalendo mkoa wa Mara, wameonesha kuvutiwa na uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya kuondoa zuio la kutofanyika mikutano ya hadhara iliyozuiliwa mwaka 2016 na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano Hayati John Pombe Magufuli.
Wakizungumza na DIMA Online Viongozi wa Ngome ya Wanawake ACT Wazalendo mkoani humo wamesema kuwa wanaimani na uongozi wa Rais Samia kwani amefanya jambo la busara la kikatiba kuondoa zuio la mikutano ya hadhara.
Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake wa Chama cha ACT Wazalendo mkoa wa Mara, Ester Charles Mwera amesema kuzuiliwa kwa mikutano kuliathiri Ngome ya Wanawake kwakuwa walishindwa kuvuna wanawake kujiunga na chama, hivyo kurejeshwa kwa mikutano ya hadhara itawezesha chama kunadi Sera zao zitakazosaidia wanawake kujiunga na ACT.
"Ngome ya Wanawake tumefurahi sana kwa uamuzi alioufanya Rais Samia mwanamke mwenzetu ni hakika wanawake tunaweza kuongoza, Rais anasimamia haki, sheria na katiba ndio sababu amefuta zuio la mikutano ya hadhara.
"Tunamuomba Rais Samia kwakuwa ni msikivu atusaidie huu mgogoro wa vibanda soko la Rebu, tulijenga vibanda wenyewe lakini Halmashauri imetunyang'anya kwa nguvu wakati mkataba haujaisha tunalazimishwa kulipa kodi ya pango laki sita kwa mwaka bila kulipa unafungiwa kibanda ukiwaambie ulipe kwa kila mwezi hawataki wanataka ulipe yote ya mwaka mzima jamani hali ni ngumu" amesema Ester.
Mwenyekiti huyo amesema zuio la mikutano ya hadhara lilidhoofisha vyama vya upinzi kwakuwa walikosa pakusemea kero za wanachi na viongozi wa vyama vya upinzani hawakuweza kusema walifungwa midomo kupitia zuio la mikutano ya hadhara.
"Wanasema wapinzani wanapiga kelele kama jambo halitendeki vyema lazima wapige kelele kushinikiza Serikali ili mambo yaende vizuri ambayo hayatendeki ipasavyo, kwahiyo mimi nimefurahi kwa uamuzi wa Rais wa kuondoa zuio, ni wakati wa sisi ngome ya wanawake kuzunguka kunadi sera zetu ili chama chetu kiwe na wanawake wengi"amesema Ester.
Katibu wa Ngome ya Wanawake ACT Wazalendo mkoa wa Mara, Pendo Kuboja Elaga amempongeza Rais Samia kwa kuondoa zuio hilo na kusema uamuzi huo ni kuonesha kuwa wanawake wameiva kisiasa na kiuongozi.
Amesema wakati chama hicho kimeanzishwa 2014 kikiwa bado ni kichanga kilifanikiwa kuvuna wanawake 800 lakini baada ya kuzuiliwa mikutano ya hadhara mwaka 2016 na kutofanyika kwa zaidi ya miaka 6 mfululizo wanawake walisambalatika ambapo kwa sasa mkoa huo una wanawake 50.
"Baada ya Rais Samia kuingia madarakani kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi kadhaa ya uongozi wake ameondoa zuio la mikutano ya hadhara lililowekwa na mtangulizi wake aliyekuwa Rais Hayati Magufuli.
"Nampongeza Rais kwa kuondoa zuio tumerudi nyuma sana ukizingatia chama chetu kwa wakati huo kilikuwa bado ni kichanga, ile hatua tuliyokuwa nayo ikarudi nyuma, kuzuiliwa kwa mikutano kumetupa hasara kubwa sasa hivi tunaanza moja.
"Sisi Ngome ya wanawake tulianza kuvuna wanachama mwaka 2014 baada ya ACT kuanzishwa hadi mwaka 2015 tulikuwa na zaidi ya wanawake 800 baada ya mikutano kuzuiliwa tumebaki wanawake 50 wengine waliamua kuacha kwakuwa hawakuona umuhimu wakuendelea na chama kwakuwa mikutano ilizuiliwa.
Ameongeza kusema "Mikutano ilisaidia kutuweka pamoja tulijadiliana, tulitafuta wanawake wenzetu kujiunga na chama, kusaidiana katika mambo mbalimbali kuhakikisha wanawake tunasonga mbele katika siasa kwakweli vyama vya upinzani tumeathirika sana"amesema Pendo.
Pendo amesema kuwa Rais Samia kuondoa zuio hilo ameonesha ukomavu wake katika siasa na anaamini wanawake wanaweza kuongoza hivyo amemuomba Rais Samia kusimamia vyema kuhakikisha mikutano ya vyama vya siasa inafanyika kwa haki bila upendeleo wowote.
"Mimi ninaamini kabisa mwanamke anaweza, kinachosababisha waseme wanawake hawawezi ni pale mwanamke anaposhindwa kuyaamini mawazo yake anategemea aongozwe au kuamini mawazo ya mwanaume kuwa ndio mawazo sahihi wakati huwenda mawazo yake yakawa sahihi zaidi.
"Kama Mungu ameweka kipawa ndani yako na ukasimama kwa yale maono ambayo Mungu amekupa utafika mbali, shida inakuja tu pale mwanamke anaposhindwa kusimama yeye kama yeye anashindwa kuamini mimi hapa nilipo nisimame mimi kama mimi na kama kiongozi.
Katibu huyo wa Mkoa amesema Rais Samia anajitahidi kuiongoza nchi " Anajitahidi sana, mapungufu kila mtu anayo hakuna aliyekamilika hapa duniani, mwanamke anaweza pasipo shida akisimama amesimama kweli lakini usimame kwa wito aliokuitia Mungu ukitaka kufanya jambo muombe Mungu akuelekeze sisi wamama tumefanya makubwa na yameenda mbali"amesema.
Pendo amesema anachojivunia katika uongozi wa Rais Samia ni kujiamini kwake katika kuongoza nchi na kupitia uongozi wake umewafungua wanawake wapate kujitambua kuwa wao wanaweza kusimama na kusimamia mambo yakaenda vizuri.
"Kupitia uongozi wake umetujenga sisi wanawake kujitambua kuwa hata sisi wanawake tunaweza kusimama katika hatua fulani na tukafanya mambo yanayoonekana, kujiamini kwake kumefanya na sisi wanawake wenzake tujiamini.
"Ukiwa kwenye nyumba yako lazima ufanye maendeleo ili mji wako upendeze, Rais Samia ni mmiliki wa mji kwa maana ya nchi lazima afanye nchi yake iwe nzuri iwe na maendeleo lazima aangalie upande huu upo vipi aweke sawa"amesema Pendo.
Katibu huyo amesema anaamini Rais Samia kwakuwa ameondoa zuio la mikutano atasimamia vyema kuhakikisha mikutano inaenda vizuri kwa uhuru na haki bila ubaguzi na upendeleo.
"Ninaamini atasimamia vizuri maana wakati mwingine unakuta vyama vya upinzani vinafanya mikutano yao bila huru wanakuwa kama wapo chini ya kizuizi fulani, hili linawafanya watu wanakuwa na uoga wakati wapo kwao hawafanyi mambo kwa haki na Uhuru.
"Kwa vile wote tupo Taifa moja naamini mtanzania halisi hawezi kufanya siasa za kuleta vurugu lazima afanye siasa ambazo zipo, na siasa hizi zinasaidia mahali pale palipoanguka mtu agundue kumbe hapa naenda vibaya acha nirekebishe.
Ameongeza" Kwavile ameruhusu basi atasimamia, atoe maagizo ili watu wanapokuwa kwenye mikutano yao watoe sera zao waeleze wananchi, lengo ni kuijenga Tanzania lakini pia sisi wanasiasa tunaposimama basi tutamke manufaa ya Taifa pasipo kuleta uchonganishi " amesema Pendo.
Naye Mwenyekiti wa Ngome ya ACT Wazalendo Jimbo la Tarime Mjini, Doto Chacha Zakayo Wangwe amesema amefurahishwa kwa kitendo cha Rais Samia kurejesha mikutano kwani mikutano inawapa wanawake ujasiri na ukakamavu kuzungumza mbele ya umati wa watu na inasaidia kuwaondoa uoga.
"Nimefurahishwa sana kwa kitendo cha Rais Samia kurejesha mikutano, tuliathirika sana tulishindwa kuwafikia wanachi, kunadi sera zetu, vyama vya upinzani ndio vinaibua mambo mengi yaliyofichika vinafichua na serikali inafanya marekebisho.
"Mikutano inatupa ukakamavu, kutujengea ujasiri na kuaminiwa na wananchi, akina mama tumejipanga tutagombea nafasi za uongozi naomba wanawake wa ACT tushikamane tutafute wanachama"amesema.
Doto ameupongeza uongozi wa Rais Samia akiwa rais mwanamke wa kwanza nchini Tanzania nakusema kuwa amefanya mambo mengi ya maendeleo kama vile kuimalisha utawala bora wa kidemokrasia.
Pia miradi mbalimbali kujengwa ikiwemo ya barabara, miradi ya maji, vyumba vya madarasa na elimu bila ada hadi kidato cha sita hivyo anamuombea kwa Mungu aendelee kumpa uzima ili aiongoze nchi vizuri.
Post a Comment