HECHE ASEMA WANANCHI WANATAKA MPAKA GN 235/1968
>>>Asema migogoro ya mpaka imesababisha watu kuuwawa
>>>Ataka Serikali kutafuta wananchi waliopotea
>>>Mhifadhi asema hana taarifa za kupotea
MJUMBE wa Kamati Kuu ya (CHADEMA) ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini 2015-2020, John Heche amesema Vijiji vilivyopo katika kata ya Nyanungu, Gorong'a na Kwihancha wilayani Tarime mkoani Mara, vinakabiliwa na migogoro ya mipaka kati ya vijiji na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) hali ambayo imesababisha kutoweka kwa amani na usalama.
Amesema kuwa migogoro ya mipaka ya vijiji na hifadhi imesababisha baadhi ya wananchi kupigwa risasi, kujeruhiwa, kuuwawa, na wengine kukamatwa na kupotelea ndani ya hifadhi huku wengine wakihofia usalama wao na kukimbilia nchi jirani ya Kenya lakini pia mifugo ya watu kukamatwa na mingine kuuwawa kwa kupigwa risasi wakati ikichunga kwenye eneo ambalo linadaiwa ni la hifadhi.
Heche ameyasema hayo wakati wa mkutano wa hadhara wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) uliofanyika Februari, 17, 2023 katika Kijiji cha Kegonga Kata ya Nyanungu.
Amesema kuwa wakati alipokuwa mbunge alizungukia mipaka hiyo wakiwa na viongozi wa Serikali lakini mwafaka haukupatikana kwakuwa yeye alihitaji mpaka wa mwaka 1968 unaotambuliwa na wananchi ndio utambuliwe jambo ambalo Serikali haikuzingatia.
"Mpaka unaotambulika ni GN Na. 235 wa mwaka 1968 uliotangazwa kwenye gazeti la Serikali, siku tulipokuja na Kigwangala aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii tuliwaonesha mpaka wakataka kuweka alama mahali kusiko tukawaambia weka alama hapa nikatoa gazeti ambalo mwalimu Nyerere alisema mpaka uwe hapa tukasimama na kukatalia pale.
"Walipoona hivyo waliondoka wote na lile jiwe kama alama wakashindwa kuweka pale, sasa hivi nasikia wamelima barabara wamefika pale.
"Hawa wananchi hatuwezi kuwaua kwasababu eti hakuna ardhi, ardhi ipo hawa wananchi wanaishi hapa wanajua mpaka, wanaweza wasijue namba ya GN na wasijue kuisoma lakini wanajua walipogawana mipaka mbuga ilikomea hapa na Serikali ilikomea hapa.
Wananchi wakinyoosha mikono juu ishara ya kukubali Waziri wa Maliasi na Utalii afike Nyanungu kusikiliza kero zao
Amshukia Mwenyekiti CCM, Mbunge Waitara
"Mwenyekiti wa CCM Ngicho ndio anaishi polini kabisa yeye ng'ombe zake hazikamatwi zinachunga ndani ya hifadhi alafu yeye ameshiba anakuja kuwaambia watu kuwa hamuwezi kupamabana na Tembo, ambaye hawezi kupambana na tembo ajifiche uvunguni anayeweza kupamabana na tembo nimekuja sasa nipo nimesimama"amesema Heche.
Heche anazidi kueleza" wamehongwa wanakuja hapa kuwaambia watu kuwa ndizi hazina kazi hivi mtu anawezaje kusema mambo ya kijinga, mkungu wa ndizi ni Tsh. 15,000 ila kwakuwa yeye anachimba dhahabu anapata hela anaona ndizi za wananchi hazina kazi, ndizi zetu zina kazi, Mkuu wa mkoa ndizi zetu zina kazi na tutaendelea kula.
Heche amesema kuwa wakati wa Kampeni Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara aliwaambia wananchi wa Kegonga wasimchague John Heche kwakuwa anatoka koo nyingine ya Wakira jamii ya Wakurya
Heche amesema kwamba Waitara aliwahimiza wananchi wa kata hiyo kumchagua yeye anayetoka kwenye koo yao ya Wairege lakini ameshindwa kuwasaidia wananchi kutatua kero ya mpaka.
"Alikuwa anasema Heche sio mwirege akasema chagueni mwirege wenu wakasema mimi ni nyumba ntobhu wakasema wao ni nyumba iliyoozeshwa kwamba hawawezi kugonga hodi ni moja kwa moja hadi uvunguni kwamba yeye ataingia ikulu moja kwa moja leo mwaka wa tatu tunaelekea shida ndio imeongezeka.
"Wao wanakaa mjini wanaagiza supu ya kongoro wakati wanaua ng'ombe, msiende kuomba supu ya kongoro kwasababu ng'ombe mnaowapiga risasi ndio wanazalisha kongoro, wanatoa nyama na maziwa, sheria na utaratibu wa nchi yetu ng'ombe hapigwi risasi.
Heche amelaani kitendo cha Askari wa hifadhi ya Serengeti aliyeuwawa kwa kuchomwa mshale na kusema kuwa kitendo hicho kinapaswa kulaaniwa na kwamba chanzo cha yote ni mgogoro huo kutotatuliwa kwa njia sahihi na za uwazi.
"Juzi kuna oparesheni imekuja hapa kupiga watu kuwa Askari kauwawa na mimi sifurahii askari kuuwawa ni tendo baya na tendo linalopaswa kulaaniwa kwa askari kuuwawa.
" lakini kama tunavyoona askari kauwawa tunataka kujua hawa vijana wetu 9 ambao wamepotea hawajulikani wapo wapi nani amewachukua ,sheria ya nchi yetu inasema kama mtu amekosea akamatwe apelekwe kituo cha Polisi watu wanapotea kama njugu tunataka tujue hao watu wapo wapi.
"Baadhi ya watu hao waliopotea ni pamoja na Mahenge C Mahenge, Nyabaso Mokoni, Ryoba Makuri, Chacha Mogaya Chacha, Chacha Range Wambura, Mwl. Mista gaini, Mwenyekiti Zakaria, Wambura Bhurwa, tangu Februari, 13, 2023 wamepotea hawajulikani waliko ambao ni wakazi wa Kata ya Gorong'a" amesema Heche.
Heche ashangazwa Diwani wa CCM kukamatwa akitetea wananchi
"Diwani wenu Tiboche alipojaribu kuwatetea akakamatwa na kuwekwa rokapu, lakini mbunge wenu ambaye ndiye mkombozi wa wananchi yeye amekuwa mbunge wa Serikali mwenzake akakamatwa yeye akalala mbele kwasababu analinda tumbo lake akajificha.
"Tunamtaka Waziri wa Maliasili na Utalii aje awasikilize, hili tatizo limekuwa kubwa na siku akija na mimi nitakuwepo ili wananchi wawe na amani kuzungumza.
" Ikishindikana nitakuja hapa waanchi mtajipanga foleni na kusaini kwenye karatasi tutafungua kesi didhi ya Serikali kudai haki zenu maana najua Wenyeviti ni wa CCM, Diwani na mbunge ni wa CCM watawazuia" amesema Heche.
Katibu wa Kamati ya sheria na haki za Binadamu Kanda ya Serengeti CHADEMA, Mrimi Zabroni amesema wananchi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Serengeti wanishi kama wajane kama si wazaliwa wa Nyanungu na hivyo kuitaka Serikali ishughulikie matatizo ya wananchi.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Mara Lucus Ngoto naye akakazia kuhusu mgogoro huo.
"CCM haiwezi kuwaondoa kwenye matatizo yanayowakabili , Diwani wenu alipojaribu kusema wanachi wanaonewa rokapu Chama chake, Serikali hiyohiyo ya kwakwe ikamweka rokapu sasa kama mwakilishi wa wananchi yeye anaishi na wananchi anajua ukweli upo hivi anawaambia wananchi watendewe hivi anawekwa rokapu toa maelezo jieleze fanya hivi je wewe utapona?.
"Yule mwingine (Mbunge Waitara) yeye akasema hamna akajificha, Diwani Tiboche yeye akajitoa mhanga ndani. Mwenyekiti wa Chama chake cha CCM anatoka kwenye Kata hii amefanya nini.
"Namshauri Ngicho kama hawezi kusema matatizo ya watu wa Nyanungu na ana ndugu zake hapa Serikali haimsikilizi, Chama chake akimsikilizi ajiuzuru awe mwananchi wa kawaida atapata heshima kubwa katika jamii"amesema Lucus.
Mwenyekiti wa Jimbo la Tarime Vijijini CHADEMA Mwita Isasi amesema mikutano ilipofungwa walipata mateso " Tumeanza safari ya kuelekea Kanani imepita miaka saba mikutano ilipofungwa tumepata machungu utadhani miaka 20, mikutano imeruhusiwa nawaomba wananchi muwe tayali kutoa kero zenu msiogope Polisi wapo kwa ajili ya kutulinda" amesema Mwita.
Diwani wa Kata ya Mbogi Nyahiri
Magarya amesema wananchi ni wa muhimu wana haki hivyo ni vyema sauti zao sikasikilizwa na kulindwa badala ya jicho kutupiwa tu kwa wanyama wa hifadhiniMhifadhi Serengeti afunguka
DIMA Online imezungumza na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti Izumbe Msindai amesema hana taarifa yoyote ya madai ya watu kupotelea ndani ya hifadhi ya Serengeti.
"Mimi sina taarifa ya watu kupotelea hifadhini na sijapokea malalamiko hayo kwahiyo sijui hao wanaotajwa kupotea wamepotelea wapi, istoshe hakuna askari aliyekwenda Karakatonga wala Nyanungu kukamata wananchi"amesema Izumbe
Ameongeza Tangu litokee tukio la askari wa hifadhi kuuwawa hakuna askari yeyote aliyekwenda kijijini, tumekwenda siku ambayo Mkuu wa Mkoa wa Mara alipokwenda Nyanungu akiwa na Kamati yake ya ulinzi na usalama nilikuwepo mimi na viongozi mbalimbali, hizo risasi zilipigwa lini?.
"Huyo aliyesema watu wamepotea ndiye awathibitishie kuwa wamepotelea wapi na risasi zilipigwa lini na nani maana mimi sina taarifa za watu kupotea au kupigwa risasi"amesema Izumbe.
Rejea ya Mhifadhi Serengeti
>>>Hivi karibuni DIMA Online ikizungumza na Mhifadhi Mkuu wa SENAPA kuhusu tuhuma za mauwaji na mifugo kupigwa risasi alisema kuwa askari wakiwa kwenye majukumu yao wanapokamata ng'ombe wanaoingia hifadhini huvamiwa na makundi ya watu wakiwa na silaha za kijadi hivyo ulazimika kupiga risasi hewani kuwatawanya.
Alisema inapotokea mtu kupigwa risasi au mifugo ni kwa bahati mbaya ambapo hutokea wakati askari wakijihami." Hilo eneo ni la Hifadhi lilitengwa na Serikali kuwa la hifadhi tangu mwaka 1968 na mipaka ikawekwa lakini wananchi wamekuwa hawakubaliani na mipaka hiyo iliyowekwa na Serikali.
"Eneo hilo lilitengwa na Serikali tangu 1968 kuwa hifadhi tafuta GN usome mpaka wa hifadhi imeonesha kila kitu, wanachi tumekuwa tukiwaita hata kwenye vikao hawashiriki ,eneo ambalo wanaling'ang'ania ni eneo ambalo mwekezaji angewekeza hoteli ya kitalii wangenufaika lakini wanaling'ang'ania eneo hilo.
Aliwaomba wanasiasa kuwaambia ukweli wananchi wao kuhusu mipaka ya hifadhi na wasitumie maeneo hayo kuomba kura kwamba wakipewa kura watawasaidia kuyarejesha maeneo hayo kwa wananchi.
Mwanzoni mwa mwezi Februari, 2023 Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee akiwa ameongozana na viongozi mbalimbali wa Kamati ya ulizi na usalama ya mkoa na Wilaya ya Tarime, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Kanal Michael Mtenjele pamoja na Viongozi wa TANAPA akiwemo Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Serengeti (SENAPA) Izumbe Msindai walifika Kijiji cha Kengonga kuzungumza na wananchi.
Viongozi wengine waliohudhulia ni wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mara akiwemo Mwenyekiti wa CCM mkoa huo Patrick Chandi, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime Daud Ngicho.
Katika mkutano huo RC Mzee aliwataka wananchi kutumia eneo la mlima linalopakana na hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) kwa malengo endelevu ya uhifadhi na utalii na kuwataka wananchi kutodanganywa na wanasiasa wanaowapotosha kuwa wataachiwa maeneo ya hifadhi kwasababu tu ya kujinufaisha kisiasa.
Post a Comment