HEADER AD

HEADER AD

WANANCHI WASEMA SERIKALI INAPOTOSHA MPAKA GN 1968


>>>Wananchi wamwomba Waziri wa Maliasili na Utalii afike kuwasikiliza

>>> Wasema mauwaji yamesababisha hofu na wengine kukimbilia kuishi Kenya


Na Dinna Maningo, Tarime

WANACHI wa Kata ya Nyanungu wilaya ya Tarime mkoa wa Mara wamemuomba Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa afike kijijini wamuoneshe mpaka wanaoutambua wao unaotenganisha vijiji na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA).

Wamesema wao wanataka utambulike mpaka uliowekwa mwaka 1968 wakati wa utawala wa aliyekuwa Rais wa awamu ya kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambao wanaujua na kwamba Serikali imebadili mpaka huo na  badala yake ikaweka mipaka mingine na kusababisha wananchi wakose maeneo ya kilimo na malisho.

Wameyasema hayo kwenye mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) uliofanyika katika Kijiji cha Kegonga katika Kata hiyo Februari, 17, 2023 ambapo viongozi wa Chama  hicho walifika kwa nia ya kusikiliza kero za wananchi.

Nyamhanga mwita amesema amefurahi ujio wa John Heche huku akimuomba apange siku ili wakamuoneshe mpaka wanaoutambua wao uliowekwa na Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere kwa kushirikiana na wananchi mwaka 1968.

Mkazi wa  Kata hiyo Magaigwa Matinyi Kemore amesema kuwa Serikali imebadili mpaka jambo ambalo limekuwa likisababisha mgogoro mkubwa baina ya wananchi na vijiji vinavyozunguka hifadhi.

               Magaigwa Matinyi Kemore

Amesema mgogoro wa mipaka  umepelekea kutokea kwa mauwaji ya mara kwa mara ya wananchi kupigwa risasi na askari wa wanyamapori katika hifadhi hiyo na kukamata mifugo yao na mingine kuuwawa kwa risasi kwa madai kuwa iliingia kwenye eno la hifadhi licha ya wao kutambua maeneo hayo ni ya vijiji huku na askari wa hifadhi akiuwawa kwa kuchomwa mshale.

"Mimi tangu nimezaliwa mwaka 1953 hadi nilivyo sasa shida yangu ni mateso tunayoyapata dhidi ya askari gemu na Serikali iliyopo madarakani , mimi kwa bahati mbaya wazazi wangu awakunipeleka shule mimi nina kiswahili cha kuzaliwa, tangu  mwaka 2000 nimekumbana na shida ya njaa matatizo chungu mbovu kwasabu ya serikali zinazokuwa madarakani.

"Mh. Heche hawa wananchi unaowaona hapa shughuli yao kubwa ni kilimo na ufugaji wana umaskini mkubwa walitolewa mashamba yao, na kunyang'anywa mifugo yao wengine wamepoteza nguvu kazi ya familia zao kwa kuuwawa kwa kupigwa risasi na Serikali kwamba wamevamia maeneo ya hifadhi.

"Serikali haitujali inajali wanyama zaidi kuliko binadamu sisi wana Nyanungu Serikali haitujali wananchi wake kilio chetu kikubwa ni kwa Serikali haituthamini wala kutujali sisi wananchi. "amesema Magaigwa.

Mwita Marwa Mugima amesema kuwa Kata hiyo imekosa amani kutokana na mgogoro wa mipaka ambao umesababisha wananchi kupotelea ndani ya hifadhi pindi wanapokamatwa na askari wa hifadhi na wanapolalamika Serikali haiwasikilizi wala kutatua changamoto hiyo ya mgogoro wa mipaka.

             Mwita Marwa Mugima

"Tukuambie siri John Heche kukosekana kwa amani watu wamepanga kukimbilia nchi jirani ya Kenya wakaishi huko, maana Serikali haitujali na tumekosa amani kwa sababu askari gemu wanakuja kijijini wanaswaga ng'ombe na kuchukua watu kwenye miji, wanasababisha watu wakae kwa hofu wazee vikongwe wanakimbizwa wanajificha Serikali imesababisha watu wakimbilie Kenya kwasababu Nyanungu hakuna amani" amesema Mwita.

Nchagwa Mgaya amesema wamechoka na mayanyaso ya askari wa hifadhi lakini hawana mtu wa kwasaidia na kwamba maeneo yao yamewekwa alama za mipaka na hifadhi.

          Nchagwa Mgaya

"Maeneo yetu wameweka bikoni tutaenda wapi na watoto wetu, mpaka umesogezwa hadi kwenye makazi ya watu ukienda kuchota maji unakamatwa, ukienda kulima unakamatwa, ukichunga mifugo unakamatwa na mifugo yako, hata mtoto akienda kujisaidia ni hivi akamatwe.

" Mimi nimeozesha mabinti watano kwa ng'ombe lakini sina ng'ombe hata wakulimia wote walikamatwa na hifadhi,  ng'ombe zikienda kunywa maji zinakutana na risasi hata usiku silali tumekosa mtu wa kututetea, hivi atatokea kweli mtu wa kututetea ? "Alihoji Nchagwa.

Nchagwa anaongeza kusema " Eti anakuja akiwa kama Serikali (Mkuu wa Mkoa Mara) anakataa eti maswali hayawezi kuulizwa hivi ataongeaje hadi amalize aondoke bila kuulizwa maswali? hivi mtu unawezaje kwenda kweye mji wa mtu uongee vizuri hadi umalize uondoke hujaulizwa ulichokifuata au hili jambo lililonileta nitawasaidia hivi.

"Watu wanakuja hapa wanatudanganya kuwa haya maneno yenu yatasikilizwa, tunashtukia watu wanakuja wanaburuza watu na kuwapeleka hifadhini hatujui wapo hai au wamekufa"amesema Nchagwa.

Paulina Chacha Wambura amesema ana hasira ndani ya moyo wake kwakuwa watoto waliozaliwa ndani ya kata hiyo wameuwawa kwa kupigwa risasi na watu wa hifadhi na wakati wote wanaishi kwa wasiwasi huku akisema kuwa amechoshwa kusikia milio ya risasi kijijini.

           Paulina Chacha Wambura

"Sisi watu wa Kegonga na Serikali ya TANAPA ni sawa na Serikali ya Somaria na Al-shabaab, Serikali haitaki kutuona, ng'ombe zetu zinapanda juu ya mlima zinapigwa risasi zinaburuzwa chini askari gemu wanaondoka nazo kwenda hifadhini.

Paulina anasema kuwa vijana sita wameuwawa kwa kupigwa risasi kama mnyama hadharani wakishuhudia kwa macho hivyo wanamuomba Mungu wa mbinguni juu awasaidie siku moja wapate kiongozi mtetezi kutoka Serikalini.

"Vijana sita wameuwawa hadharani tukishuhudia kwa macho yaani mtu anafukuzwa anapigwa risasi kama mnyama, tunaomba Mungu wa mbinguni atusaidie tupate kiongozi atakayetusaidia kuondokana na Mambo haya, najiuliza nafsini mwangu kwamba Mungu huishie juu mbinguni hii ardhi ni yako milima ni yako.

"Kama kweli Serikali ya Tanzania inayotutangulia inahitaji milima tunayochunga ng'ombe ije ituambie hadharani kwamba tunahitaji hii milima labda kuna dhahabu, mali fulani tunataka kuwaleta wawekezaji ili sisi tunufaike tule kwao, vijana wapo wengi wamenunua pikipiki kwa mikopo  lakini hazina kazi hazina sehemu za kufanya kazi.

"Kama kweli ni Serikali inayotusaidia inayohitaji hoja za wananchi kwanini isitutengenezee barabara hata ya Kwenda huko TANAPA vijana wetu waendeshe pikipiki kupeleka ndizi tukauwauzie  matunda watu wa TANAPA tunazo ndizi, maparachichi wapeleke biashara wapate fedha walipe mikopo.

Ameongeza " Huku Nyanungu tumepakana na mpaka wa Kenya na Tanzania  Serikali wakiungana na Kenya tutapata fedha za kigeni kwasababu tumepakana na hifadhi na nchi ya Kenya lakini tumekuwa kama wakimbizi, tunamuomba Mungu wa mbinguni akamguse John Heche akatutamkie hili jambo la kero.


"Sisi hapa ni wafungwa ni dhidi ya Somaria na al-shabaab, majuzi nilishuhudia kuona bunduki ambayo sijawahi kuiona tangu nizaliwe nina miaka 56 wakafika nyumbani kwangu wakaniambia nisipige yowe nikawaambia baba mimi sipigi yowe wakasema tulia.

"Wakasimama pembeni yangu wakapiga risasi wananchi wakakimbia huku na kule hadi bata wangu 13 zikakimbia zikaogopa baadae zikarudi, maskini nililia nakusema Mungu wangu tusaidie"amesema Paulina.

Josephate Wansato Wambura amesema wananchi wanajua mpaka halisi kwani wakati umewekwa enzi hizo wazee wao walishiriki kama mashuhuda lakini kadri siku zilivyokwenda Serikali imekuwa ikisogeza mipaka hadi kwenye ardhi inayomilikiwa na wananchi.

        Josephate Wansato Wambura

"John Heche watu hawajajitokeza kama inavyotakiwa walipoona magwanda ya Polisi walilala mbele, wengine wametoroka, lakini nyie polisi ninyi ni vijana wetu, baba zetu wengine wadogo zetu muwe mnafanya kazi kama mlivyokula kiapo.

"Nipende kusema hili kama ni uongo mnipige mawe mpaka nife,tuliwahi kukaa hapa mwaka 2015 Mwenyekiti wa CCM Wilaya alipoona mji wake umehesabiwa kuwa ndani ya hifadhi alipiga kelele sana TANAPA wakasogeza nyuma mpaka na mji wake ukawa nje.

"Lakini siku amekuja hapa kuna jambo alisema kwamba sogea mrudi nyuma ili tuweke bikoni, sasa kwakuwa Heche wewe ni mwakilishi wa wananchi tunaomba hili ikiwezekana utuvushe kama jinsi Musa alivyowavusha wana wa Israel kutoka Misri.

" Hata baba wa Taifa wakati anapigania uhuru alipata misukosuko mingi ikiwezekana twende kwa mguu tukuoneshe mpaka tunaoufahamu sio huu wanaotuletea, kuna mipaka wameweka miaka ya 1970-1990 ambayo walikuwa wanakuja kuweka usiku wanapaka rangi kwenye mawe" amesema Josephate.

Je nini kilichozungumzwa na viongozi wa CHADEMA katika mkutano huo? Nini kauli ya Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti? endelea kufuatilia DIMA Online.

          Magaiwa Mwita Kebanga

        Viongozi wa CHADEMA





No comments