HECHE : WANANCHI TARIME HAWATEGESHI WANATUMIA FURSA
>>> Asema kama wananchi ni tegesha basi na mke wa Kikwete ni tegesha
>>>Asema tathmini imekiuka Sheria, haikuwa ya uwazi na ushirikishaji
>>>Aahidi kuitafuta haki ya wananchi ndani na nje ya nchi
Na Dinna Maningo, Tarime
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) ambaye pia aliwahi kuwa mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini mwaka 2015-2020, John Heche amesema kuwa kitendo cha wananchi kutolipwa fidia na wengine kupunjwa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaoshirikiana na Serikali ya Tanzania katika uthamini ni ukiukwaji wa haki za Binadamu.
Amesema kumekuwa na tabia ya Serikali kwa kushirikiana na mgodi kugomesha malipo kwa wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa kwa shughuli za mgodi wakiwemo wa Kijiji cha Komarera Kata ya Nyamwaga kwa madai kuwa nyumba za wananchi na mali zao zilijengwa kwa kuvizia malipo ya mgodi maarufu 'Tegesha'.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Nyamwaga Kata ya Nyamwaga hivi karibuni Februari, 17,2023 ulioandaliwa na Chama hicho, John amesema Wananchi wa Tarime hawategeshi.
Amesema wanachokifanya ni kutumia fursa iliyopo na kwamba kama nyumba na mali zao ni tegesha basi na ardhi ya Salma Kikwete mke wa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoinunua mkoani Lindi kwenye ukanda wa bahari nayo ni tegesha.
"Eti wanawaita watu tegesha kuanzia leo niwaambie hakuna mtu anaitwa tegesha hapa Tarime, watu wanaotegesha ni mgodi ndio wamekuta watu wanaishi, watu wa Tarime wamechungulia fursa wakaona fursa wakawekeza, watu wa Tarime ni wawekezaji, tutawapigania mpaka watalipwa fidia zao.
"Hivi kwa mfano ukiambiwa pale Komarera hakuna Lodge (nyumba ya kulala wageni) na kuna watu wengi wanataka maeneo ya kulala, ukienda kuweka lodge je wewe ni tegesha au umeona fursa ukaenda kuwekeza?.amehoji.
John ameongeza " Pale Lindi kumekuwepo na gesi watu wanaenda kuchimba gesi kuna makampuni makubwa yanayotoka Ulaya yameenda kuchimba gesi , mke wa Kikwete Rais Mstaafu amenunua ardhi kwenye ukanda wa bahari anasubiri wale watu wakija wanunue ardhi yake Kwahiyo ni tegesha au amewekeza ?.
"Mtu wa Tarime wakisikia amenunua kaeneo ka -laki mbili walau apate kamilioni we ni tegesha, mke wa Kikwete yeye sio tegesha? sisi sote ni sawa na hakuna tegesha watu wametumia fursa" amesema.
John amesema kuwa zoezi la uthamini lililofanyika Kijiji cha Komarera kata ya Nyamwaga halikufuata sheria kuanzia Kwenye tathmini na halikuwa la wazi wala shirikishi.
"Ukisoma mwongozo wa uthamini wa namna ya watu kulipwa fidia ukurasa wa 12 unasema kama mtu ana mimea na mazao mti unaozalisha atalipwa asilimia 100,mimea au miti iliyopevuka mtu atalipwa asilimia 60,mimea au miti michanga atalipwa asilimia 30, mimea au miti mikongwe atalipwa asilimia 50, wao wanaandikia watu asilimia 25, asilimia 30, asilimia 40, asilimia 15 wamezitoa kwenye mwongozo gani"amesema John.
Amshukia Mbunge Waitara
John amesema ameshangazwa kwa kitendo cha Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara kutowasemea wananchi wake ambao wamenyimwa haki zao katika malipo ya fidia badala yake anawabagua.
"Ninashangaa eti mtu anaitwa Mbunge ambaye ni mwakilishi wa wananchi sio mwakilishi wa Serikali anasimama anasema kwanza watu hawa wanatoka Keisangura, yeye ambaye amejenga kule Ukonga-Dar es Salaam amezaliwa huku je siku wakitaka kulipa eneo kule Ukonga watakataa eti anatoka Karakatonga?.Mbunge anaenda kufanya Family Day (Siku ya Familia) Mgodini wakati wananchi wake wanalala nje wamebomolewa nyumba, wananchi waliobomolewa wao hawana familia!
" Sio wote wenye ardhi pale Komarera lakini ni ndugu zetu , jamaa zetu kama mgodi umekuja umeona eneo na akalihitaji akalipwa pesa akaja kujenga nyumba mafundi atakaowatumia ni wa hapo kwenu, matofari, mchanga atachukua hapo kwenu.
" Fundi atanunua mboga atamtuma bodaboda apeleke mboga nyumbani pesa hiyo boda atanunua mafuta kwahiyo hakuna sababu ya kuoneana wivu hiyo mali tusipoipata sisu itaondoka kwenda Ulaya na sisi tutabaki na maisha ya tabu" amesema John.
Mjumbe huyo wa Kamati ya CHADEMA amesema Mgodi umekuwa ukitoa matangazo kwa wananchi kuchukua maeneo yao kwa madai ya kuwafanyia tathmini na kuwazuia kuendeleza maeneo hayo lakini huchukua muda mrefu bila kuwalipa kitendo ambacho wananchi wanalazimika kuendeleza maeneo yao.
"Tarehe 28, Mei, 2020 mgodi ulitoa tangazo pale chini (Komarera) ukasema watu wasiendeleze maeneo toka tarehe hiyo wakaja mwaka mwingine tarehe 26,Juni,2021, yaani mtu akute eneo lako apige tangazo mimi nataka kununua eneo lako lakini akwambie hakuna kulima eneo hilo mpaka nije ,hivi huo ujinga upo kwenye nchi gani ?wakati huo watoto wako wanakula nini.
"Wakakaa mwaka mzima bila kufanya uthamini alafu leo wanawaambia watu eti tulipiga picha za setilaiti (Setellite) mwaka 2020 kwahiyo tutatumia picha za Setilaiti, mimi Heche nasema hatutumii malipo ya Setilaiti, tutatumia malipo ya kile mlichokikuta kwa sasa, ndio sheria inavyosema.
Heche amezidi kueleza kwamba " Kuna mtu hapa anaenda kufanya kazi za mgodi, anavaa viatu vya mgodi anakula mgodini anaitwa Rashid anasema wakurya ni wajinga Rashid tutaruka na wewe kama mwewe unavyochukua vifaranga acha kutania watu kwasababu sheria inasema pale unapofanyiwa uthamini unaambiwa mali zako.
"Kama una mti unaambiwa una miti kumi unajibu eee unaangalia kama imeandikwa miti kumi, una mahindi 200 na wewe unaangalia kama kilichoandikwa ndicho chenyewe unakubali, wanathamini vyote kisha wanakupa kopi nao wanabaki na yao juu ya mali zote walizothamini ,siku ya malipo wanakuletea vocha ya malipo ya vitu walivyovikuta unachukia na ile nakala yako ya Tathmini unafananisha hivi walivyonipa ndo vyenyewe? na pesa ndiyo yenyewe ?.
"Lakini mgodi haukufanya hivyo, naambiwa eti mtu mmoja alikuwa anawaambia saini hapa unasaini alafu anaondoka anakwambia utakuta pesa benk sasa utafahamu vipi vitu pesa iliyopo na vitu walivyokuandikia kama vipo sawa? alafu kwanini huyu Rashid asikamatwe kwasababu huo ni ufisadi! kwanini watu wa TAKUKURU hawajamkamata huyo Rashid"amesema John.
Akisoma risala iliyoandaliwa na uongozi wa Kata wa Chama hicho Chacha Mariba Ntora amesema Wananchi wanakabiliwa na manyanyaso, uvunjifu wa haki za Binadamu, na ukiukwaji wa sheria za nchi.
Amesema kuna nyumba zilibomolewa barabara ya Tarime lakini wamekosa mtetezi kwani watu hawakulipwa fidia, wananchi wa Kijiji cha Komarera kunyanyaswa na mgodi kwa kushirikiana na Serikali bila malipo kwa baadhi ya wananchi.
"Tatizo lingine ni wananchi kupewa amri ya kinguvu kupisha maeneo kwa ajili ya ujenzi wa stendi kinyume na haki, kucheleweshwa malipo makusudi upande wa mgodi, watu kunyimwa malipo ya uthamini kwamba wametegesha, ubaguzi wa makazi, kunyimwa nakala za fomu za uthamini.
"Mgodi umekuwa ukifanya vitendo visivyokubalika kisheria kwa kuvamia maeneo ya watu na taasisi mfano kuvamia kanisa Katoriki Kigango cha Nyabikondo na kufanya tathmini bila hidhini ya viongozi wa kanisa, vipigo, udhalilishaji hivyo watu kuvunjiwa heshima, kwani wakazi ambao hawakuridhika na uthamini walipigwa sana" amesema.
Chacha amewataja baadhi ya wananchi waliopata vipigo ni pamoja na Mzee Machungu, Chacha Nyangoko ambapo pia wananchi wengine waliharibiwa mali ikiwemo kubomolewa nyumba zao kinyume na kibali cha Mahakama ,vitendo vya rushwa.
" Pia kuna tatizo la watu kubambikiziwa kesi na Mwenyekiti wa Kijiji cha Komarera, baadhi yao waliobambikizwa kesi ni Msabi Samwel Mseti, Joseph Mwita maarufu Masai, Mwita Sagire, Joseph Pius Mkami, hizi ni takwimu chache za matukio mabaya yanayofanywa na mgodi , uongozi wa CCM na Serikali"amesema Chacha.
John amesema barabara zinazojengwa ni kwa fedha za Benk ya Dunia na zimeelekezwa mtu alipwe fidia kama barabara imepita kwenye eneo lake na kwamba wapo wananchi waliojenga nyumba zao tangu mwaka 1970 na barabara imeanza kujengwa hivi karibuni lakini watu wamebomolewa nyumba bila kulipwa fidia jambo ambalo ni ukiukwaji wa haki za Binadamu.
Katibu wa Chama cha Democrasia na Maendeleo (CHADEMA) Lucus Ngoto amesema kuwa wananchi wamekuwa wakilalamika kubomolewa nyumba zao lakini Serikali haina muda kuwasikiliza na kutatua matatizo yao.
Lucu Ngoto
Amewaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Chama hicho katika kuitafuta haki kwakuwa haki ya mtu yaweza kuchelewa lakini haipotei na haki itapatikana iwapo watashirikiana.
Wananchi kupitia mkutano huo wamemuomba John Heche kuwasemea ili wapate haki zao naye amewaahidi kuwatetea ndani na nje ya nchi kuhakikisha wanapata haki zao.
Mwongozo wa Uthamini wa Fidia
Kwa mujibu wa mwongozo wa uthamini wa fidia wa march, 2016 uliotayarishwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi unasema fidia ni malipo yanayotolewa kwa mtu au taasisi kama mbadala wa mali yake kutokana na kuondolewa kwenye eneo lake lililotwaliwa kwa manufaa ya umma na kupangiwa matumizi mengine tofauti na yale yaliyopo sasa.
Mwongozo unasema swala la fidia katika nchi ni kitu kisichoepukika kulingana na uhitaji mkubwa wa ardhi kwa miradi yenye manufaa ya umma kama vile kwa ajili ya uwekezaji au shughuli yoyote inayofanywa na Serikali au binafsi hasa za maendeleo ya Taifa.
"Mara nyingi na hasa kwa wakati huu ambao ardhi inatambuliwa ni mali na mtaji chini ya sheria za ardhi Na. 4, na 5, panakuwa na ongezeko la mvutano baina ya mamlaka zinazolipa fidia na wananchi wanaolipwa fidia juu ya taratibu za Uthamini na viwango halisi vya thamani za Mali zao zinazotwaliwa kwa mujibu wa sheria.
"Kutokana na ukweli kuwa ni haki ya msingi ya mwananchi (ama mfidiwa au mlipaji ) kuhoji, kuelimishwa, kulalamika na kusikilizwa kuhusu kupatiwa haki yake ya fidia; ni dhairi kwamba kuna changamoto nyingi kuhusu maswala ya fidia na hivyo hatuna budi kufuata misingi na taratibu za uthamini wa fidia katika hatua zote kikamilifu" Mwongozo umeeleza.
Misingi ya Uthamini wa Fidia
Mwongozo unaelekeza kwamba msingi mkuu wa fidia ya haki, kamilifu na inayolipwa kwa wakati ni kiwango cha thamani ya soko (market value) ya ardhi na maendelezo kwa wakati husika.
Fidia ya Haki (Fair compensation): ni ile inayohakikisha taratibu, vigezo na viwango vya ukadiriaji thamani vyenye usawa baina ya wafidiwa wote na kwa pande zote husika (bila kuegemea au kupendelea/kuonea upande wowote) na yenye uhalisia ya viwango vya soko.
Fidia Kamilifu (Full compensation): ni ile ya kutosheleza yenye uhalisia wa viwango vya soko kwa wakati uliopo kwa kuzingatia sheria na misingi ya taaluma ya uthamini.
Fidia inayolipwa kwa wakati (prompt compensation): ni ile inayolipwa ndani ya kipindi cha miezi sita (6) ambayo;
Kwa mujibu wa Sheria; Kifungu cha 13(2) cha kanuni za sheria ya Ardhi Na.4 za mwaka 2001 na Kifungu cha 19(1)–(3) cha kanuni za Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na.5 za mwaka 2001 ni tangu ardhi ilipotwaliwa au milki kubatilishwa.
Lakini, Kwa mujibu wa Taaluma ya Uthamini ni tangu taarifa ya uthamini inapoidhinishwa na Ofisi ya Mthamini Mkuu kwa kigezo kuwa hiyo ndiyo tarehe ya thamani hiyo (valuation date/validity).
Pamoja na kuzingatia bei ya soko, lakini kutokana na kwamba suala la utwaaji linahusisha ‘forced sale’ na siyo suala la ‘willing seller and buyer’ basi sheria imezingatia hilo kwa kulipa fidia inajumuisha posho ambazo ni posho ya upotevu wa makazi, upotevu wa faida, usumbufu, usafiri na gharama za awali katika kupata ardhi.
Hivyo, kifungu Na.3(1) (g) cha Sheria ya Ardhi Na.4 ya 1999 na Kanuni zake pamoja na vifungu Na.(7-11) vya kanuni za Sheria ya Ardhi, 2001 zitawezesha kufikia fidia stahiki.
Uwekaji asilimia (%) za ukuaji katika uthamini wa mazao
Mwongozo unamwelekeza mthamini ajitahidi kuwa mwangalifu katika uwekaji asilimia kwa kuhakikisha asilimia ya ukuaji inayowekwa inawiana na ukubwa wa mmea.Asilimia kuu za ukuaji ni Kama ifuatavyo. Mimea/Miti inayozalisha 100%, Mimea/Miti iliyopevuka 60%, Mimea/Miti michanga 30% na Mimea/Miti mikongwe 50%.
Post a Comment