HEADER AD

HEADER AD

PASUA KICHWA TAARIFA YA VIONGOZI, RAID MAUAJI MGODI WA NORTH MARA


>>>Viongozi Watuma barua nchini Kanada wakidai hakuna mauaji, vipigo, mateso vilivyofanyika Mgodi wa North Mara 

>>> Ni baada ya Watanzania kufungua kesi nchini Kanada ya ukiukwaji wa Haki za Binadamu dhidi ya Mgodi

>>>Wataka Vyombo vya Dola kuwachukulia hatua RAID kwa kuandika habari za ukiukwaji haki za Binadamu dhidi ya Mgodi.

>>>> RAID yaweka wazi ripoti yao ya ukiukwaji wa Haki za Binadamu yakiwemo mauaji Mgodini


Na Dinna Maningo, Tarime 

KWA muda mrefu kumekuwepo malalamiko ya baadhi ya wananchi Wilayani Tarime mkoa wa Mara, nchini Tanzania ya ukiukwaji wa Haki za Binadamu unaosababishwa na askari wa jeshi la Polisi Mkoa wa Polisi Tarime Rorya wanaolinda Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa kuwapiga wananchi, kuwajeruhi kwa risasi na wengine kupoteza maisha kwa madai ya kuvamia mgodi.

Pia kumekuwepo na malalamiko ya wananchi kupitia ripoti mbalimbali za ukiukwaji wa haki za binadamu zilizoripotiwa katika vyombo vya habari, Viongozi wa Serikali na Vyama vya kisiasa zikihusisha mauwaji, vipigo, mateso unyanyasaji kwa wananchi wanaoishi kando kando ya mgodi huo wa North Mara.

Ripoti hizo zinawalenga askari wa Jeshi la Polisi wakilalamikiwa kutumia nguvu katika kuimalisha ulinzi na usalama mgodini kwa kuwajeruhi wananchi kwa vipigo na kuwapiga risasi na kupelekea kupata vilema vya maisha na huku wengine kupoteza maisha.

Mashirika mbalimbali ya kutetea haki za Binadamu yamekuwa yakijitokeza kupinga vitendo hivyo na kufanya tafiti mbalimbali kuhusiana na ukiukwaji wa haki za Binadamu kwa wananchi wa vijiji vinavyozunguka mgodi huo huku viongozi wa Serikali ya Tanzania wakifika kusikiliza malalamiko ya wananchi na kuahidi kuyashughulikia.

Wananchi wa maeneo yanayozunguka mgodi wa North Mara wamekuwa wakilalamikia Serikali yao kwa kutokomesha vitendo vya mauaji  vinavyofanywa na baaadhi ya askari wa jeshi la Polisi wanaolinda mgodi.


Kutochukuliwa hatua za uwajibishaji kwa watuhumiwa, baadhi ya Watanzania wamelazimika kufungua kesi ya ukiukwaji wa haki za Binadamu ikihusisha vipigo, mauwaji na mateso.

Wamefungua  kesi ya kisheria katika Mahakama Kuu ya Sheria ya Ontario nchini Kanada dhidi ya kampuni kubwa ya madini ya Barrick Gold yenye makao yake makuu nchini Kanada kwa ukiukwaji wa haki za Binadamu unaofanywa na mgodi wa dhahabu wa  North Mara uliopo nchini Tanzania.

Watanzania wapatao 21 wanadaiwa kufungua kesi wakiulalamikia mgodi wa North Mara kwa vitendo vya mauaji ya kikatili, risasi na mateso wanayodai kufanyiwa na Polisi wanaokuwa wakilinda mgodi huo.

Malalamiko hayo ya Watanzania wanaodai kufanyiwa katika mgodi huo yamepingwa vikali na baadhi ya Viongozi wa Serikali za Vijiji 11 wakiwemo Wenyeviti wa Vijiji, Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Kata.

Viongozi  hao wameandika taarifa iliyotiwa saini zao na kugongwa mihuri inayodaiwa kutumwa Mahakama Kuu ya Ontario ikipinga habari zzilizoripotiwa na RAID Shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake makuu nchini Uingereza linalojihusisha na masuala ya Haki za Binadamu ambalo hufichua vitendo vya ukiukwaji wa haki za Binadamu.

Wenyeviti hao na Watendaji wamepinga ripoti za RAID zinazoeleza ukiukwaji wa haki za binadamu yakiwemo mauwaji yanayotekelezwa na askari wa Jeshi la Polisi wanaolinda mgodi wa North Mara.

Taarifa ya Viongozi ikiutetea mgodi

DIMA Online imefanikiwa kupata nakala ya taarifa ya Viongozi wa Vijiji, 11 vinavyozunguka mgodi huo wakiwemo na Watendaji wa Vijiji na Kata wapatao 22 ikizungumzia madai ya RAID yenye kichwa cha Habari 'TAARIFA ZA VIONGOZI WA VIJIJI 11 VINAVYOZUNGUKA MGODI KUHUSU MADAI YA RAID  TAREHE 13,JULAI 2022'.

Nakala ya taarifa hiyo ilitolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) ambaye pia aliwahi kuwa mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini mwaka 2015-2020, John Heche.

Chombo hiki cha habari kilipata taarifa hiyo wakati akizungumza  na wananchi na kusikiliza kero zao katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Nyamwaga kata ya Nyamwaga wilayani humo na kugusia taarifa hiyo iliyoandikwa na Viongozi wa Vijiji wakikana kutokea Mauaji Mgodi wa North Mara.

                   John Heche

Taarifa hiyo imeambatana na majina, saini na mihuri ya Wenyeviti wa Vijiji 7 Kati ya 11 ambao wote wanaotokana na Chama cha Mapinduzi (CCM) Chama tawala kilichopo madarakani, Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Kata wameeleza kusikitishwa na uchapishaji wa habari mbalimbali unaoendelea na kueleza kuwa ripoti hizo ni za uongo na za kudhalilisha zilizotolewa na taasisi ya RAID.

Viongozi hao katika taarifa hiyo wamesema kuwa wao ni viongozi wakuu wa masuala  ya ulinzi, usalama na maendeleo ya wananchi katika vijiji vyao, kwamba mara kwa mara, RAID huchapisha ripoti kuhusu kile wanachokiita ukiukwaji wa haki za kiibinadamu na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara.

Wametaja moja ya ripoti ni yenye kichwa cha habari Mauaji mapya na mashambulizi katika mgodi wa Barrick Gold Tanzania yavunja madai ya uboreshaji mkubwa wa kampuni', ripoti iliyochapishwa mwezi Machi 2022.

Viongozi hao wamedai kuwa wamefuatilia zaidi na kugundua kuwa RAID iko katika mchakato wa kuchapisha na kutoa ripoti nyingine yenye madai kama hayo. RAID inadai kwamba;

 "Wamefanya misheni mbili za utafiti katika vijiji vyetu mnamo Mei 2022 kuhusu masuala ya mashambulizi toka kwa vyombo vya usalama na kusababisha mauaji.Walipokea ripoti za kuaminika za wakazi wa eneo hilo kwamba kuna watu waliouawa na kushambuliwa na operesheni za vyombo vya usalama kati ya Februari na Julai 2022. 

"Wamezidi kudai kwamba watu wawili waliuawa na angalau wengine kumi kujeruhiwa vibaya baada ya kupigwa, kupigwa risasi na kuteswa. Maafisa wa polisi wanaolinda mgodi mara kwa mara huingia kwenye jamii na kurusha risasi za moto na mabomu ya machozi ovyo, kuvunja mali bila kibali, kuwakamata na kuwapiga wakazi kiholela na kusababisha uharibifu wa mali."Taarifa imeeleza.

Katika taarifa hiyo wamesema hayo ni madai mazito ya ukiukwaji wa masualama ya usalama, kijajusi na haki za binadamu katika nchi ya kidemokrasia kama Tanzania.

"Tunapenda kukumbusha kwamba kwa mujibu wa Ibara za 145 na 146 za Katika ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali za Mitaa ni vyombo vya utoaji haki na walinzi wa amani, usalama na haki za binadamu katika jamii zetu.

"Kama wawakilishi wa jumuiya ya wenyeji kutoka vijiji 11 vinavyozunguka mgodi, tumefanya kazi na mgodi ili kuhakikisha uzingatiaji thabiti wa masuala ya haki za kibinadamu na heshima na jumuia ya watu wa eneo hili.

"Tunaweza kusema kwa majigambo kwamba, Mgodi wa North Mara unazingatia na kudumisha kwa dhati kanuni za haki za binadamu na utu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa serikali za mitaa zinashiriki katika usalama na ulinzi wa shughuli na mali za mgodi" Imeelezwa kwenye Taarifa.

Viongozi hao wamesema kwamba kwa mujibu wa sheria ya NGOs ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa, NGOs zote zinazotaka kushirikisha jamii zinatakiwa kujitambulisha katika serikali za mitaa zinakotaka kufanya kazi.

"Kwa bahati mbaya hakuna hata Kijiji kimoja kati ya vijiji 11 kilichopokea taarifa kama hiyo.Vilevile, kwa kuzingatia unyeti wa taarifa za masuala ya ulinzi na usalama, mateso na mauaji, mashauriani sahihi yalihitajika kufanyika kabla ya kufanya majumuisho.

"Vijiji 11 vimekuwa vikifanya kazi kwa karibu na vyombo vyote vya dola vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama vya serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa, kitaifa ndani ya Tarime na Barrick North Mara Gold Mine bila tatizo lolote. Kwahiyo" Taarifa imeeleza.


Taarifa hiyo inazidi kueleza " Tukiwa viongozi wa jamii katika vijiji vinavyozunguka mgodi tumesikitishwa sana na njia isiyo ya kitaalam ambayo masuala na ukweli hupotoshwa kimakusudi.

"Hatukushirikishwa kutoa maoni na RAID juu ya madai yaliyotolewa wala hatujui RAID ni nani, wala wanamwakilisha nani na wana maslahi ya aina gani. Tunalaani na kuhimiza vikali vyombo vya dola vinavyohusika kuchunguza, na kuchukua hatua zinazohitajika."imeeleza Barua 

Viongozi hao wamesema hawana uhakika kama RAID imesajiliwa kufanya kazi nchini Tanzania na ina mamlaka ya kisheria ya kukusanya, kuchapisha na kusambaza habari kuhusu usalama wa Tanzania bila mashauriano yanayofaa.

Taarifa hiyo ya viongozi ina wasihi Asasi za kiraia na taasisi zingine zozote husika na watu binafsi kufuata taratibu zinazoruhusiwa kisheria katika kufanya tafiti na kushughulikia masuala ya jamii ikiwa ni pamoja na kufanya mashauriano sahihi na mamlaka husika.

"Tunapenda kukumbusha kuwa Rais wa Tanzania amekuwa mstari wa mbele kutafuta wawekezaji wa kukuza uchumi wa Tanzania na Mgodi wa North Mara ni ubia kati ya Barrick na Serikali ya Tanzania kupitia Twiga Minerals Co.Ltd.

"Tunawaomba Barrick kuripoti RAID kwa mamlaka husika kwa hatua zaidi na kuendelea na shughuli za Mgodi ili kunufaisha jamii za eneo laNorth Mara na nchi kwa ujumla.

"Mwisho, Tungependa kukumbusha kwamba, Barrick imekuwa na uwazi wa kushirikisha wadau mbalimbali katika shughuli zake. Viongozi wa vijiji na jamii zinazozunguka North Mara wamekuwa na mazungumzo kadhaa na mgodi katika masuala mbalimbali yenye maslahi kwa pamoja.

Viongozi hao wanaongeza kusema" Kama wawakilishi wa jumuiya ya eneo la North Mara, hatuna nia ya kuficha ikiwa haki za binadamu zinakiukwa na Barrick. Kando ya hayo, vyombo vya Habari, NGOs za ndani na serikali ya Tanzania zote zinafanya kazi na hazijagusia masuala haya wakati wowote .

Wanawasihi RAID iwaache Barrick waendelee na shughuli zake na wasitumie mgodi na jamii maskini zinazozunguka North Mara kwa manufaa binafsi.

Maelezo hayo ya viongozi  yameambatana na majina yao yakiwa na saini zao za mkono na majina mengine yakisainiwa kwa mkono na kugongwa mhuri wa Serikali ya kijiji na mhuri wa Afisa Mtendaji.

Majina ya Wenyeviti wa Vijiji

Viongozi hao ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja  Bunini .J. Bunini aliyesaini na kugonga mhuri wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja, Chacha Michael Babere Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamwaga aliyesaini kwa mkono, Mwita .M.Kirindo Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyangoto aliyesaini kwa mkono na muhuri wa Serikali ya Kijiji cha Nyangoto kugongwa.

Wengine ni Chacha Makuri Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyakunguru aliyesaini kwa mkono na mhuri wa Serikali ya Kijiji cha Nyakunguru kugongwa, John .M.Otunga Mwenyekiti wa Kijiji cha Genkuru aliyetia saini pekee, Mniko Magabe Mwenyekiti wa Kijiji cha Kerende  aliyetia saini pekee pamoja na Stephano Ng'weina Mwenyekiti Kijiji cha Msege aliyetia saini na kugonga mhuri wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Msege.

Maafisa Watendaji wa Vijiji (VEO) 

Maafisa Watendaji wa Vijiji ni Marwa Nyamantage Mtendaji Kijiji cha Nyakunguru aliyetia saini pekee, Zawadi .F. Temba Mtendaji Kijiji cha Nyabichune aliyetia saini pekee, Sumun Samson Mtendaji Kijiji cha Kewanja aliyetia saini na kugonga mhuri wa Mtendaji Kijiji cha Kewanja, Mussa N.Raphael Mtendaji Kijiji cha Komarera aliyesaini na kugonga mhuri wa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Komarera.

Wengine ni Winfrida .E. Mwita Mtendaji Kijiji cha  Mjini Kati aliyetia saini pekee, Mogosi Gasper Ntambe Mtendaji Kijiji cha Kerende aliyetia saini na kigonga mhuri wenye maandishi ya lugha ya kingereza, Gichogo Chacha Nyankena Mtendaji Kijiji cha Genkuru aliyesaini na kugonga mhuri wa Afisa Mtendaji wa Kijiji, John .M. Otunga Mwenyekiti Kijiji cha Genkuru aliyetia saini pekee.

Watendaji wengine wa vijiji ni Mwita M.Mtariro Mtendaji Kijiji cha Msege aliyesaini na kugonga mhuri wa Mtendaji wa Kijiji cha Msege, Faustine .C.Kikerero aliyetia saini pekee, Robert Marwa Makonyo Mtendaji Kijiji cha Nyangoto aliyesaini na kugonga mhuri wa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyangoto na James Magige Wambura Mwenyekiti Kijiji cha Nyamwaga aliyesaini na kugonga mhuri wa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyamwaga.

Watendaji wa Kata (WEO)

Maafisa Watendaji wa Kata ni Happnes .W.Kahalwe Mtendaji kata ya Nyamwaga aliyetia saini pekee,  Venance .B. Karoli Mtendaji Kata ya Kibasuka aliyetia saini pekee, Paulo Masirori Mtendaji Kata ya Kemambo aliyetia saini pekee na Lucus .I. Kichogo Mtendaji Kata ya Nyarokoba aliyetia saini pekee.

Ripoti ya RAID

Shirika la RAID limekuwa likiripoti habari mbalimbali zikihusisha ukiukwaji wa haki za Binadamu unaofanywa na mgodi wa North Mara kutokana na tafiti zilizofanywa na shirika hilo katika mgodi huo.

Kwa mujibu wa Tovuti ya RAID www.naid-uk.org Novembar 23,2022 iliripoti habari ikieleza waathiriwa wa haki za Binadamu wa Tanzania wamefungua kesi ya kwanza kabisa ya kisheria nchini Canada dhidi ya mgodi wa Dhahabu wa Barrick.

Shirika la utetezi wa haki za binadamu RAID linasema kwamba raia 21 wa Tanzania wamefungua kesi ya kisheria dhidi ya kampuni kubwa ya madini ya Barrick Gold ya Canada kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za Binadamu katika mgodi wa dhahabu wa Kampuni hiyo North Mara nchini Tanzania.

Ripoti za RID zinaeleza kuwa ni mara ya kwanza Barrick kukabiliwa na hatua za kisheria nchini Canada kwa ukiukwaji wa haki za Binadamu katika moja ya shughuli zake nje ya nchi.

Ripoti ya RAID inaeleza kwamba wananchi hao waliofungua kesi ni wa Kabila la Wakurya waishio wilaya ya Tarime nchini Tanzania wakilalamikia mauaji ya kikatili, risasi na mateso wanayodai yalifanywa na Polisi waliokuwa wakilinda mgodi huo.


Wananchi hao wanawakilishwa na Makampuni ya kisheria ya Camp Fiorante Matthews Mogerman LLL na Waddell Phillips kesi iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu ya Sheria ya Ontario.

Kesi hiyo inajumuisha matukio matano ya kuteswa, na majeraha mengine matano ya kupigwa kwa risasi na askari polisi wanaolinda mgodi.

RAID iliripoti kwamba mgodi wa North Mara ni miongoni mwa migodi hatari zaidi ya kiviwanda barani Afrika kwa ghasia zinazohusiana na usalama, takribani watu 77 waliuwawa na 304 kujeruhiwa na Polisi wanaohusika na usalama wa mgodi, matukio mengi yamekuwa yakitokea tangu Barrick kumiliki mgodi huo Machi, 2006.

RAID imeripoti kuwa kiini cha vurugu kinatokana na matumizi ya mgodi huo kwa Maafisa wa Polisi wa Tanzania, Mgodi wa North Mara unawalipa vifaa Polisi, unawalisha na kuwahifadhi takribani maafisa 150 wa Polisi kwa utaratibu wa makubaliano yaliyotiwa saini kati ya Kampuni hiyo na Polisi.

Ripoti inaeleza kuwa Polisi wanaolinda mgodi wana bunduki ndogo, na mipini ya mbao pamoja na mabomu ya machozi na mabomu ya sauti ambayo hufyatua kutoka ndani ya mgodi.






No comments