HEADER AD

HEADER AD

MAHAKAMA YATOA ELIMU YA SHERIA MTAA WA MTAKUJA


Na Jovina Massano, Musoma.

MAHAKAMA ya Mwanzo Musoma Mjini imewaasa wananchi kutochanganya sheria na tamaduni ili kuepusha migogoro katika familia zao na jamii kwa ujumla.

Rai hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Musoma Mjini Mkoani Mara Bahati John Bwire alipokuwa akitoa elimu ya sheria ya mambo mbalimbali katika mkutano wa Mtaa wa Mtakuja A Kata ya Mwisenge uliowashirikisha wakazi hao wakiwepo viongozi wa Kata na Mtaa huo.

Amesema elimu imejielekeza kwenye migogoro ya ardhi, ndoa,mirathi, jinai na kesi za madai lakini pia kununua haki(rushwa).

     Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Musoma Mjini Bahati John Bwire akitoa  elimu ya Sheria kwa wakazi wa Mtakuja "A" Kata ya Mwisenge.

Ameeleza kuwa watu wengi wanachaganya tamaduni na sheria hasa katika mirathi na ndio maana migogoro mingi katika familia inatokea ambapo sababu ni kutokana na mfumo dume katika baadhi ya makabila hapa nchini.

" Migogoro mingi katika jamii ni ya ardhi hii inatokana jamii kutoelewa umuhimu wa usimamizi wa mali zilizopo wengi hawatoi nafasi kwa mwanamke kuwa mrithi wa mali sio kwa kuondokewa na mume hata mtoto wa kike haruhusiwi kuwa mrithi hii ni kutokana na tamaduni zilizopo lakini katika sheria ni tofauti inaeleza kuwa mrithi ni mtu yeyote katika familia mtenda haki ", amesema Bahati.

Ameongeza kuwa migogoro mingine ni ya ndoa na mirathi na ipo baina ya familia au watu wa karibu yaani majirani kwa majirani na hivyo kutumia njia ya utatuzi kwa kuielimisha jamii na kufanya usuluhishi, njia itakayosaidia amani na utulivu baina ya pande zote.

Mkazi wa Mtakuja "A" Marysiana Makubi ameipongeza Mahakama kuu Kanda ya Musoma kwa kutimiza ahadi yao ya kuelimisha wananchi uelewa wa sheria kupitia Mahakama ya Mwanzo kwani elimu iliyotolewa ina umuhimu mkubwa katika jamii.

         Marysiana Makubi Mkazi wa Mtakuja "A" Kata ya Mwisenge

"Yaani hili somo la sheria limeniingia sana nimefunguliwa masikio naomba mahakama itenge muda wa kutosha kutulisha chakula hiki tunahangaika na kurumbana kumbe njia nyepesi za bila msuguano zipo.

"Ninamuomba Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma asichoke kila kikao cha mtaa wawepo hii itasaidia kuimarisha amani migogoro itaisha tufanye maendeleo katika jamii na nchi yetu", amesema Marysiana.

Nae Mjumbe wa Mtaa wa Mtakuja "A" Amina Nyamhanga amesema amefurahishwa kutolewa somo la udhulumaji haki na kwamba amefahamu njia za kufuata ili kupata haki endapo ameikosa na amewashauri wakazi wa mtaa huu kushiriki kikamilifu katika mikutano inayofanyika mara kwa mara.

  Mjumbe wa Mtaa wa Mtakuja "A" Amina Nyamhanga

Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mtakuja "A" Halima Tangawizi amesema kuwa hakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu mirathi na umiliki wa ardhi.

      Halima Tangawizi Katibu mwenezi CCM Kata ya Mwisenge

Amemshukuru mtoa elimu kwa kuelezea na kuchanganua kwa ufasaha na amewaomba wakazi wa mtaa huo kuhakikisha wanashiriki mikutano ya pindi wanapopata taarifa kwani elimu iliyotolewa ina manufaa kwa familia.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mtakuja A Aloyce Masatu  kuwa ni wakati sasa kwa viongozi wa ngazi za chini kufanya mikutano kisasa ili kuiwezesha jamii kuwa na misingi bora na kushiriki kikamilifu katika kujiletea mabadiliko kiuchumi.



Lakini pia amemshukuru Jaji Wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma kwa kutimiza ahadi ya kushuka kuelimisha jamii hasa ngazi za chini  hii itasaidia kuleta mabadiliko ya chanya ya kimaadili.
                  




No comments