HEADER AD

HEADER AD

MAHAKAMA : TUPO TAYARI KUTOA ELIMU YA SHERIA KWA JAMII


Na Jovina Massano, Musoma

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Musoma mkoani Mara imejipanga kuelimisha umma juu ya sheria mbalimbali ikiwa ni moja ya uwajibikaji wao kwa wananchi.

Hayo yameelezwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Musoma Fahamu Mtulya alipokuwa akizungumza hivi karibuni na Mwandishi wa DIMA ONLINE.

Amesema kuwa mahakama hiyo ipo tayari kushirikiana na Tawala za mikoa,Wilaya, Mitaa na Vijiji kuhakikisha wanawafikia wananchi wakiwemo wa vijijini ili kuwapatia elimu ya sheria. 

       Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Musoma Fahamu Mtulya

"Natambua wananchi wengi wapo vijijini na huwa wana vikao mbalimbali sisi kama Mahakama tupo tayari kutoa ushirikiano pindi wanapohitaji ufafanuzi kutoka kwetu kama wataalam wa Sheria, ndio lengo letu la kitaifa linavyotuongoza". Amesema Mtulya.

Ameongeza kuwa wananchi hulipa kodi wakiwemo wa vijijini ambapo mishahara wanayolipwa watumishi inatoka kwao hivyo wana haki ya kunufaika na kodi hizo kwa kuwafikia.

Mwenyekiti wa mtaa wa Mtakuja "A" Kata ya Mwisenge Manispaa ya Musoma Aloyce Masatu Lawi amempongeza Jaji Mfawidhi kwa uamuzi wake wa kushuka  kwenye ngazi ya jamii kwani ndipo migogoro inapoanzia.

      Mwenyekiti wa mtaa wa Mtakuja "A" Kata ya Mwisenge, Aloyce Masatu Lawi

"Kuna migogoro mingi katika jamii zetu, elimu hii ya sheria ni muhimu sana ikishuka katika jami zetu itachangia kuongeza usalama na amani katika maeneo yetu ", Amesema Aloyce.

Naye Peragia Kokuirwa Herman mkazi wa Nyakato kwa saa nane Kata ya Mshikamano yeye ameomba elimu ya sheria iwafikie pia wanawake na watoto kwani ipo sheria inayowalinda lakini wao hawafahamu na kwamba ikitolewa itasaidia kupunguza ukatili uliopo majumbani.
         Peragia Kokuirwa Herman

"Serikali yetu ilipotunga hizi sheria ni kwa ajili ya usalama wa kila mmoja kunapotokea uvunjifu wa amani zitatumika ili kuleta usawa na amani nawaomba wahusika waanze kuelimisha mapema jamii zetu tupate mabadiliko",amesema Peragia.

Kauli hiyo ya Jaji Mfawidhi imekuja baada ya habari iliyoripotiwa katika chombo hiki cha habari ya Januari, 31, 2023 ambapo Agatha Mwita mkazi wa Kyagata Wilaya ya Butiama, aliyeshiriki maonesho ya wiki ya sheria aliomba elimu ya sheria itolewe hadi vijijini.

      Agatha Mwita mkazi wa Kyagata Wilaya ya Butiama

Nukuu ya Mwananchi:

>>> "Nawaomba wahusika wa mahakama zetu hapa nchini kutumia hata vikao vya kata na vijiji kutuelimisha juu ya sheria ili watusaidie sisi wananchi kupata uelewa wa kutosha kuhusu mahakama zetu"amesema Agatha. 

Pia aliomba elimu itolewe kwa wananchi wavijijini juu ya sheria ya ardhi ili kupunguza na kuondoa kabisa migogoro ya ardhi kwa jamii.




No comments