HEADER AD

HEADER AD

UKOSEFU VITABU VYA NUKTA NUNDU MATESO KWA WALIMU, WANAFUNZI


>>>Shule ilisajili wanafunzi wasioona tangu mwaka 2019

>>>Haijawahi kuwa na kitabu chochote cha Nukta Nundu

>>> Walimu wanalazimika kubadilili maandishi kutoka kwenye vitabu vya kawaida kuwa ya Nukta Nundu.

Na Dinna Maningo, Tarime

SHULE ya msingi Magufuli ya Wanafunzi wenye mahitaji maalum iliyopo Kata ya Nyamisangura, katika Halmashauri ya Mji Tarime Mkoani Mara haina vitabu vya Nukta Nundu.

Walimu wanalazimika kubadili maandishi kutoka kwenye vitabu vya kawaida na kuyachapa kuwa maandishi ya nukta nundu kwenye karatasi maalum na kudurufu kwa ajili ya kujifunzia wanafunzi wenye ulemavu wa kuona.

Mekaus Maingu mwenye ulemavu wa viungo ni Katibu wa Shirikisho la (SHIVYAWATA) Vyama vya Watu wenye Ulemavu Halmashauri ya Mji Tarime ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya watu wenye ulemavu katika Halmashauri hiyo, na ni Mwalimu wa shule hiyo akifundisha wanafunzi wasioona darasa la nne.

Katibu huyo Mwl. Mekaus anasema wanalazimika kubadili maandishi ya kawaida kuwa maandishi ya nukta nundu kwakuwa hawana vitabu maalum vya nukta nundu kwa ajili ya wanafunzi wasioona kujifunzia.

      Katibu wa SHIVYAWATA Halmashauri ya Mji Tarime Mekaus Maingu.

Anasema kutokuwepo vitabu vya nukta nundu hujikuta hawaendi na muda unaotakiwa wa ufundishaji kwakuwa muda ambao wangetumia kufundisha wanafunzi wanautumia kunakili maandishi kutoka kwenye vitabu mbalimbali vya kufundishia na kubadili katika maandishi ya nukta nundu.

" Tunafundisha masomo mbalimbali kutoka kwenye vitabu vya Hisabati, Kingereza, Maarifa ya Jamii, Uraia na Maadili, Stadi za Kazi, Afya na Mazingira, Kusoma, Kuhesabu na kuandika ambavyo ni vitabu vinavyotumika pia kwa wanafunzi wasio na mahitaji maalum.

"Muda wa kubadili na kuchapa maandishi yote ya vitabu vyote vya kufundishia kuwa maandishi ya nukta nundu alafu ufundishe hautoshi, unafanya kazi mbili kwa wakati mmoja na unashindwa kukamilisha vipindi kwa wakati, tunajikuta hatuendi na muda unaotakiwa wa kufundisha". anasema Mwl. Mekaus".

Katibu huyo wa Shirisho la Walemavu na Mwalimu wa shule hiyo anaongeza kusema" Wanafunzi wasioona walianza kusajiliwa mwaka 2019 wakati huo wakiwa wanasoma katika shule ya msingi Turwa.

"Hadi sasa hatujawahi kupata kitabu chochote cha nukta nundu zaidi ya kubadili maandishi kutoka kwenye vitabu vya kawaida kuwa ya nukta nundu unayachapa kwenye mashine, unafanya kazi mbili kwa wakati mmoja" anasema.

          Shule ya msingi Magufuli ya Wanafunzi wenye mahitaji maalum

Mwalimu huyo anasema kuwa vitabu vya nukta nundu ni muhimu kwa wanafunzi wasioona kujifunzia kwani vinapokuwepo vinawasaidia wanafunzi kujisomea wawapo darasani na wawapo nyumbani.

"Faida ya vitabu cha nukta nundu ukishafundisha mwanafunzi ana uwezo wa kujisomea, kutokuwepo kwa vitabu kunakwamisha ufundishaji mzuri kwa wanafunzi.

Katibu huyo anasema kuwa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi wenye ulemavu wa kuona wapatao sita wanaosoma katika madarasa mbalimbali ambapo darasa la nne wapo wanafunzi wanne wanaotarajia mwaka huu kufanya mtihani wa kujipima na kwamba ukosefu wa vitabu vya nukta nundu unawakosesha haki ya kujisomea.

          Maandishi ya Nukta nundu

"Tuna walimu watatu wanaofundisha wanafunzi sita wasioona, walimu wanatosheleza kwa hilo naipongeza sana serikali kwa kutuletea walimu wa kutosha kufundisha wasioona.

Anasema sababu ya kuwa na wanafunzi wachache inatokana na uelewa mdogo wa wazazi kutoandikisha watoto shule na kwamba walimu wamekuwa wakijitahidi kuzunguka majumbani kutafuta watoto wenye ulemavu wakiwemo wasioona lakini baadhi ya wazazi huwaficha.

Anasema sababu nyingine ni ukosefu wa fedha za kuwasafirisha watoto kwa kutumia usafiri wa pikipiki kwenda shuleni na kurudi nyumbani hali inayochangia watoto kutopelekwa shule na wengine kuacha shule kwasabu ya wazazi wao kushindwa kumudu nauli za usafiri wa pikipiki.

" Serikali imejenga bweni moja kwa ajili ya wanafunzi wa kike bado halijakamilika ili lianze kutumika, likikamilika watoto wa kike wataishi shuleni maana hata huduma ya chakula serikali inagharamia wazazi hawachangishwi fedha yoyote.

"Tukipata mabweni kwa wanafunzi wa kike na kiume yatasaidia kuondoa visingizio vya wazazi kuwa wanashindwa kuleta watoto kwasababu ya kukosa nauli ya pikipiki kuwaleta shuleni, wapo watoto wanaotoka mbali kufika shuleni nauli ya pikipiki ni 1000-1500 kwenda na kurudi kwa siku moja ni 2000-3000" anasema Mwl Mekaus.

Mashine zinahitajika

Mbali na vitabu vya nukta nundu pia kuna upungufu wa mashine ya kuchapa maandishi ya nukta nundu, walimu na wanafunzi wanalazimika kuchangia mashine moja jambo ambalo linakwamisha juhudi za utendaji wa kazi na fursa ya wanafunzi ya kujifunza kwa muda unaofaa kuchapa maandishi ya nukta nundu.

       Mwanafunzi mwenye ulemavu wa kuona akichapa maandishi ya Nukta Nundu

" Mashine ni moja hiyohiyo wanafunzi waitumie kujifunzia, bado walimu watatu wanatakiwa wachape maandishi ya nukta nundu kila somo analofundisha bado hiyohiyo itumike kuchapa mitihani. Hali hii inarudisha nyuma elimu, tunaiomba serikali yetu itusaidie vitabu na mashine ili elimu izidi kuwa bora" anasema.

Afisa Elimu akataa kuzungumza

Afisa Elimu Msingi katika Halmashauri hiyo John Matiko Kebaha alipoulizwa kuhusu ukosefu wa vitabu hivyo alidai kuwa vitabu vipo licha ya uongozi wa shule kukiri kutokuwepo vitabu  hivyo.

 Pia hakuwa tayari kuzungumza zaidi kuhusu shule hiyo hadi na kumwomba  Mwandishi huyo wa Habari aende ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji  kuomba kibali ndipo azungumze.

" Hivyo Vitabu vipo lakini naomba uende kwa Mkurugenzi akupe kibali kisha uje tuzungumze, kuna Mwandishi wa Habari aliwahi kuripoti habari bila kibali cha Mkurugenzi aliyekuwepo kwa wakati huo ilituletea shida sana naomba uende kwa Mkurugenzi uzungumze nae" anasema Matiko. 

Mkurugenzi akataa kuhojiwa 

Mwandishi wa Habari wa DIMA Online, Februari,2, 2023 alifika ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Tarime Mkoani Mara, Gimbana Ntavyo kupata ufafanuzi wa habari aliyokuwa akiifuatilia.

        Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Tarime Mkoani Mara, Gimbana Ntavyo.

DIMA Online alihitaji kufahamu mafanikio na changamoto za elimu katika shule hiyo lakini hakujibiwa chochote zaidi ya kumtolea maneno makali mwandishi wa habari akimtuhumu kuandika habari ya uongo aliyoiripoti mwezi mmoja uliopita akidai ilikuwa ni habari ya uongo.

Mkurugenzi huyo alikataa kuhojiwa na kumwambia mwandishi huyo ni waganga njaa na mbabaishaji huku akimpiga marufuku kutofika tena ofisini kwake. 

Desemba, 19, 2022, DIMA ONLINE iliripoti habari yenye kichwa cha habari kisemacho TARIME TC YASHINDWA KUTEKELEZA AGIZO LA NAIBU WAZIRI TAMISEMI' habari ambayo ilihusu ujenzi wa vyumba vya madara ambayo imeonekana kumchukiza mkurugenzi huyo.

Nukta nundu ni nini ?

Nukta nundu ni muwasilisho wa herufi kwa njia inayoshikika au kutambulika kwa vidole ambapo herufi na namba au hata noti za muziki na alama za kisayansi zinachorwa kiasi kwamba mtu asiyeona au mwenye uoni hafifu anaweza kutambua na kusoma kama kawaida.

           Maandishi ya Nukta nundu

Mradi wa shule Bora

Shule Bora ni mradi wa Serikali unaofadhiliwa na Serikali ya Uingeleza wenye thamani zaidi ya Tsh.Bilioni 270 wenye lengo la kuendeleza azma ya serikali ya kuboresha elimu nchini Tanzania.

Mradi huo umelenga kutatua changamoto za kielimu hapa nchini ambao umejikita katika vipaumbele vinne muhimu ambavyo ni kujifunzia (Wanafunzi), Kufundishia (Walimu), Elimu jumuishi kwa wanafunzi wa hali zote na uimarishaji wa shule.

      Uzinduzi mradi wa Shule bora

Lengo ni kuhakikisha Elimu ya awali, msingi na sekondari inaboreshwa, mazingira rafiki,usawa wa kijinsia ili wanafunzi wapate elimu bila vikwazo.

Rejea ya Viongozi:

April, 4, 2022, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akiwa kwenye uzinduzi wa mradi wa 'Shule Bora' katika shule ya msimgi Mkoani iliyopo Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani, alisema mradi huo utaongeza ubora wa elimu nchini.

         Uzinduzi mradi wa shule bora

Aliongeza kuwa serikali inaendelea kuangalia suala la miundombinu ya elimu ili kuhakikisha inakuwa bora ambayo inawezesha watoto wote kuitumia bila vikwazo vyovyote hasa wale wenye mahitaji maalum.

Waziri wa Uingereza Vick Ford ni miongoni mwa walioshiriki katika uzinduzi wa mradi wa 'Shule Bora', alisema mradi huo utasaidia zaidi ya watoto Milioni nne kutoka Mikoa 9 nchini Tanzania ambayo ni mkoa wa Tanga, Mara, Pwani, Dodoma, Singida, Kigoma, Katavi, Simiyu na Lukwa ili kuhakikisha watoto wote wanaopaswa kwenda shuleni wanaingia shuleni.

   Waziri wa Uingereza Vick Ford

Vick alisema kuwa mradi huo utafanya kazi katika mfumo wa elimu wa nchini kuwajengea uwezo walimu ili waweze kufundisha vizuri huku akiipongeza serikali ya Tanzania kuruhusu watoto waliokatisha masomo yao kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ujauzito kurudi shuleni.

Waziri huyo wa Uingereza alisema ndoto yake ni kuona ufadhili kutoka nchini humo unaleta matokeo chanya nchini Tanzania, kwa kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum, wenye mazingira magumu na watoto wa kike wanapata elimu bora.

Pamoja na uwepo wa changamoto mbalimbali za kielimu serikali ya Tanzania imekuwa ikijitahidi kuhakikisha elimu inakuwa bora katika ufundishaji na ujifunzaji pamoja na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya elimu ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa huduma ya chakula bure kwa shule zenye mahitaji maalum.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa katika ziara maalum Machi, 7, 2022, katika shule ya Sekondari Benjamin Mkapa alisema kuwa serikali itaendelea kutoa fedha kuhakikisha inajenga mazingira wezeshi kwa watoto wenye mahitaji maalum ili kuwawezesha kupata elimu katika mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia nchini.

      Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan

Rais Samia aliagiza ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kuhakikisha wanaifanyia kazi miongozo ili kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum wanakaa vyema na wanapata fursa zitakazotolewa na serikali katika sekta ya Elimu.

Aliongeza kuwa katika mwaka wa 2020/2021 Serikali imechapa na kusambaza vitabu vya maandishi yaliyokuzwa kwa masomo yote kuanzia darasa la kwanza hadi la saba kwa ajili ya wanafunzi wenye uoni hafifu au wasiona kabisa.

Mkataba wa Kimataifa kuhusu nukta nundu

Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye ulemavu (CRPD) wa mwaka 2006, Nchi ya Tanzania ilisaini mkataba huo Machi, 2007 na kuridhia Novemba, 2009 kukabiliana na ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa dhidi ya watu wenye ulemavu duniani.

Ibara ya 2 ya mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu inataja nukta nundu kama mbinu muhimu kwenye elimu, uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, kupata taarifa na mawasiliano mbalimbali.

Mkataba huo wa Kimataifa unasema kuwa watu wenye ulemavu watapata usaidizi unaohitajika ndani ya mfumo wa elimu, ili kuwawezesha kuelimika vilivyo.

Kuwezesha mafunzo ya maandishi ya nukta nundu, maandishi mbadala na njia za kukuza mawimbi ya sauti na nyinginezo za kuboresha mawasiliano, mbinu kabilifu za ujongeaji, na kuwezesha huduma za makundi rika na ushuri.

Pia kuhakikisha kwamba elimu kwa watu wenye ulemavu hususani watoto wasioona, viziwi, au viziwi wasioona inatolewa kwa lugha, mfumo na njia sadifu za mawasiliano, na katika mazingira yatakayotoa nafasi kubwa ya maendeleo kitaaluma na kijamii.

No comments