MNEC MSUKUMA : RC MARA WATUMISHI WAKO NDIO SHIDA WAONDOE
>>>Asema fedha zimeletwa zimekwisha miradi haijakamilika
>>>Amwomba Rais Samia kuwaondoa Wakurugenzi wabovu
>>Aviomba vyombo vinavyotoa taarifa kutopambapamba taarifa
Na Mwandishi Wetu, Musoma
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini Joseph Kasheku Msukuma, amemuomba Mkuu wa mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee na Wakuu wa Wilaya, kutumia madaraka yao vizuri kuwawajibisha watendaji wanaokwamisha miradi ya maendeleo licha ya serikali kutoa fedha nyingi za miradi.
Msukuma ameyasema hayo Februari, 5, 2022 kwenye mkutano wa hadhara wa kuadhimisha miaka 46 ya kuzaliwa kwa chama hicho uliofanyika kimkoa Wilaya ya Musoma.
"Mkuu wa mkoa watumishi wako ndio shida kuna miradi imejengwa hapa lakini haijakamilika na hela zimepigwa, tusaidie wale ambao una uwezo nao waondoe weka hata rokapu.
" Yaani mimi Samia angenipa u DC heeeee wangening'oa meno kama ubunge tu watu hawalali, tumieni madaraka yenu vizuri kuchukua hatua, una wakuu wa Wilaya wazuri wakuletee taarifa miradi ikamilike" amesema Msukuma.
Msukuma amesema Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi kujenga miradi lakini wapo baadhi ya watendaji wanakwamisha juhudi za rais huku akimwomba Rais Samia kuwaondoa wakurugenzi wa Halmashauri wasiokwenda na kasi yake katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
"Hatujawahi kupata rais anayeleta mabilioni ya pesa kama huyu Rais Samia, pale niliko mimi kijijini tumemwaga lami kwenye barabara sasa tusimwangushe fedha zinaletwa lakini utekelezaji unakuwa F.
"RC, mfano tu mdogo unajua mimi sio muoga Mkurugenzi wako wa Tarime Mji (Gimbana Ntavyo) wa ovyo sana na lazima tuseme mimi sio muoga hata kama yupo hapa mimi hamkuniita hapa kuja kupamba mi sipambi.
Msukuma amesema katika Halmashauri ya Mji Tarime zimeletwa fedha za ujenzi wa miradi lakini baadhi ya miradi pesa zimekwisha miradi ikiwa haijakamilika.
" Zimeletwa pesa shule jirani wamejenga Milioni 400 na kitu na chenji imebaki Milioni 9, huku kwake mjini... Mwenyekiti wa Halmashauri Tarime mjini uko wapi? hela mmemaliza na mnataka Milioni 280 sijui zinatoka wapi, alafu mkipiga simu anawatishia haiwezekani" amesema Msukuma.
Mjumbe huyo wa Halmashauri kuu ya CCM amesema Mabilioni ya fedha yanatolewa lakini hayafanyi kazi inavyotakiwa na hivyo watendaji hao kuwa sehemu ya kukiharibia Chama na Serikali na kwamba wanapaswa kutolewa nafasi za ukurugenzi wa Halmashauri.
"Rais Samia hawa ndio wanatuharibia Chama na Serikali watoe watoe ,kwenye Taarifa ya CAG Bwana Kichere kuna Halmashauri ilifanya vibaya ilitoka Mara kwa Getere, tumezungumza haya ndio yanatuangusha Mabilioni bila usimamizi yanatolewa kwenye mfuko yanadondokea chini.
"Hawa watu watoe najua Mh.Rais karibu unatoa mkeka wa Wakurugenzi fyatua hawa ambao wanalalamikiwa utuletee wengine kwani nini bwana!, kama Mkurugenzi hawezi kumuogopa mkuu wa mkoa, hawezi kumuogopa Dc, Mwenyekiti wa Chama ndio usiseme.
Ameongeza" Tumeletewa Rais mwingine tunaemuogopa hapa ni Mkuu wa Mkoa na Dc, Mkurugenzi ni mtu mdogo sana hiki kibuli cha kusema uteuzi wa Rais itafika mahali.....hawa ndio wanatusumbua" amesema.
Pia ameviomba vyombo vinavyompatia taarifa Rais Dkt. Samia kumpa taarifa sahihi na sio kuzipambapamba ambazo baadae Chama cha CCM kinapata shida.
Amesema iwapo kuna jambo limeshindikana kwenye uongozi wa Chama, Madiwani wanalalamika , Rc analalamika basi ni vyema wakaandika malalamiko hayo kwenda uongozi wa juu kwani wakati viongozi wanalalamika wengine wanapamba kwakuwa wanawekewa mafuta kwenye gari zao jambo ambalo halifai.
Post a Comment