HEADER AD

HEADER AD

WANAFUNZI WENYE ULEMAVU WA KUSIKIA HAWANA MWALIMU WA AWALI,VITABU



 >>>Shule ya Magufuli haina Walimu wa awali, vitabu vya lugha ya alama

>>>Haina Kamusi,Video CD ya Lugha ya alama

>>> hakuna vifaa vya kufundishia masomo ya Sayansi 

Na Dinna Maningo, Tarime

SHULE ya msingi Magufuli ya Wanafunzi wenye mahitaji maalum iliyopo Kata ya Nyamisangura, katika Halmashauri ya Mji Tarime mkoani Mara haina walimu wa kufundisha wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia (Viziwi) darasa la awali hadi la pili, wanafunzi wanafundishwa na walimu wanaofundisha darasa la tatu hadi la saba.

Shule hiyo ina vitabu vya Tanzatoto pekee ambavyo vinatumika kwa watoto wadogo wa darasa la awali hadi darasa la pili, haina vitabu vya lugha ya alama kwa darasa la kwanza hadi la saba.

Pia haina kamusi ya lugha ya alama, Video CD ya lugha ya alama na vifaa vya kufundishia  masomo ya Sayansi kwa lugha ya alama.

Shule ya msingi Magufuli

Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Halmashauri ya Mji Tarime Mekaus Maingu mwenye ulemavu wa viungo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya watu wenye ulemavu katika Halmashauri hiyo na mwalimu wa shule ya msingi Magufuli, amesema shule ina jumla ya wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia 15, ina walimu sita wanaofundisha wanafunzi hao.

       Katibu wa SHIVYAWATA Tarime, Mekaus Maingu

Mekaus amesema shule hiyo iliyopewa jina la Magufuli ilianzishwa mwaka 2020 ambayo bado haijasajiliwa, amesema wanafunzi wenye mahitaji maalum awali kabla ya kujengwa majengo mapya ya shule hiyo wanafunzi wenye mahitaji maalum walikuwa wanasoma katika shule ya msingi Turwa iliyokuwa na kitengo cha Elimu maalum kilichoanzishwa mwaka 2012.

"Shule haina walimu wa elimu ya awali, hakuna vitabu vya lugha ya alama , hakuna kamusi  ya lugha ya alama, kuna kitabu cha Tanzatoto pekee kinachotumika kwa watoto wadogo na hiki kilipatikana kwa juhudi ya shule, kuna mwalimu alienda semina akaja nacho tukadurufu.

       Kitabu cha Tanzatoto

"Shule ina Tv na king'amuzi lakini hakuna Video CD ya lugha ya alama kwa ajili ya watoto kutazama, imekuwa ni changamoto sana hata kwenye usajili".amesema Makaus.

Mwalimu anayefundisha wanafunzi wasiosikia amesema hakuna mwalimu wa darasa la awali hadi la pili " Hayo madarasa huwa yana walimu wao ambao wamesomea ualimu wa elimu ya awali lakini kwakuwa shule haina sisi tunaofundisha madarasa ya juu ndio tunawafundisha.

"Wanahitaji walimu wao wa awali kuwafundisha masomo kama vile afya na mazingira, michezo na sanaa, kuandika, kuhesabu na kusoma.Tangu nimekuja hapa 2019 nimekuta hiyo changamoto ya kutokuwepo walimu wa awali hadi darasa la pili.

"Hatuna Video CD ya lugha ya alama, vifaa vya kufundishia masomo ya Sayansi kwa lugha ya alama kuanzia darasa la tano hadi la saba, mfano lenzi, kifaa cha mfumo wa uzazi na vinginevyo"amesema.



Ameongeza kuwa mwaka jana alihitimu mwanafunzi mmoja darasa la Saba mwenye ulemavu wa kusikia na kwamba ukosefu wa kamusi ya lugha ya alama ni changamoto inayorudisha nyuma elimu kwa wanafunzi wasiosikia.

"Tunatumia kamusi zetu binafsi kufundisha, walimu watatu wanazo, pia hatuna mtaala wa darasa la awali hadi la pili kuhusu lugha ya alama, mtaala wa ufundishaji wa lugha ya alama haupo tunafundisha kwa mazoea kwakuwa tulipita chuoni, vitu ulivyosoma chuoni unakuja ili uvifundishe lakini havipo .

"Mitaala ya kufundishia lugha ya alama iwepo ili kuwajenga watoto katika msingi wa lugha ya alama ili anapoingia darasa la tatu anakuwa ana uelewa mzuri katika lugha ya alama".amesema Mwalimu. 

Katibu huyo wa Shirisho la watu wenye ulemavu amesema ni vyema Serikali ikawa na mtaala rasmi kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum pia kutoa semina kwa walimu wanaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum.

       Baadhi ya wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia wakiwa darasani

Lugha ya alama ni nini

>>>Lugha ya alama ni lugha ya ishara inayotumiwa na jamii ya viziwi katika kufikisha ujumbe unaokusudiwa kwa muhusika.

Lugha hii utumia viungo vya mwili ili iweze kufanya kazi, viungo hivyo ni mikono, vidole, kichwa, macho, kiwiliwili, masikio, mdomo, ulimi na pua.

       Alphabeti ya alama zinatotumiwa kwa walemavu wa kusikia (Viziwi)

Kwa mujibu wa watu wenye uziwi, Kuna lugha ya alama ya asili na lugha inayotumiwa na baadhi ya viziwi katika eneo dogo la jiografia wakati lugha ya alama rasmi ni lugha iliyosanifiwa na inatumiwa na idadi kubwa ya viziwi.

Kiziwi ni mtu yeyote mwenye matatizo ya kusikia au asiyesikia kabisa mwenye matatizo ya kusikia kwa maana ya kusikia kwa shida au usikivu wao ni wa majira (Hard of hearing) ila asiyesikia kabisa ni mtu ambaye hawezi kutafsiri sauti ya kitu au kutambua kitu kwa kusikia.




               Kamusi ya Lugha ya alama 




 


No comments