SERIKALI ILIVYOWEZESHA MADARASA SABA SHULE YA MAHITAJI MAALUM
>>>Wanafunzi wenye ulemavu wa akili, Wasioona, Wasiosikia walikaa darasa moja
>>>Serikali ikatoa Milioni 140 kujenga madarasa 7 kuwaondolea adha
Na Dinna Maningo, Tarime
UKOSEFU wa vyumba vya madarasa ni moja ya changamoto inayorudisha nyuma taaluma ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, kwakuwa ulazimika kulundikana ndani ya darasa moja hali inayosababisha ugumu katika ufundishaji na kujifunza.
Pia wanafunzi hushindwa kusoma kwa uhuru kutokana na mbanano darasani jambo linalosababisha mazingira ya utoaji na upataji elimu kutofikiwa katika viwango vinavyohitajika vya ubora wa kitaaluma.
Shule ya msingi Magufuli ni shule ya mahitaji maalum iliyopo katika Kata ya Nyamisangura wilaya ya Tarime mkoa wa Mara, ilianzishwa mwaka 2020.
Shule ya msingi Magufuli
Awali kabla ya kujengwa kwa shule hiyo mpya wanafunzi wenye mahitaji maalum walisoma shule ya msingi Turwa iliyokuwa na kitengo cha elimu maalum kilichoanzishwa mwaka 2012 jirani na ilipo shule ya Magufuli.
Wanafunzi wa mahitaji maalum wakiwa wanasoma shule ya msingi Turwa walikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vyumba vya madarasa hali iliyowalazimu wote kukaa Kwenye chumba kimoja licha ya kutofautiana mahitaji.
Mekaus Maingu mwenye ulemavu wa vuungo ni Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) Halmashauri ya Mji Tarime, ni Mwenyekiti wa Kamati ya watu wenye ulemavu katika Halmashauri hiyo na ni Mwalimu wa shule ya msingi Magufuli akifundisha wanafunzi wenye ulemavu wa kuona darasa la nne, anaeleza ukosefu wa vyumba vya madarasa ulivyoleta adha .
"Elimu bora inaendana na majengo kwa maana ya madarasa ya kutosha, ili wanafunzi wasome vizuri na walimu wafundishe vizuri ni muhimu shule kuwa na vyumba vya madarasa vya kutosha, hii inasaidia kupunguza mlundikano wa wanafunzi darasani na kumpa urahisi mwalimu kuweza kufundisha vizuri.
"Wanafunzi walipochangia darasa moja ilileta shida kwasababu walisoma kwa kuchanganyikana humohumo wasioona, wasiosikia na wenye ulemavu wa akili, ilileta ugumu sana kwa walimu, mf. wakati unawafundisha labda wanafunzi wasioona wale wa kundi lingine inabidi wasubiri mmalize ndipo mwalimu wao aingie kuwafundisha.
Anaongeza" Wakati unawafundisha hawa wale wengine wanacheza wanapiga kelele na huwezi kuwazuia maana hawana kazi ya kufanya wanakusubiri umalize uondoke mwalimu wao aje kufundisha, hali hii ilisababisha wanafunzi hao kutopata haki sawa ya kielimu kutokana na mazingira yaliyochangiwa na ukosefu wa vyumba vya madarasa.
"Wanafunzi wakiwa wengi darasani ni vigumu kumfikia kila mmoja hata unapotaka kukagua madaftari wanapokuwa darasani utatumia muda nwingi wakati huohuo unahitaji uwafundishe, wanafunzi wanapokuwa wachache darasani inaleta wepesi katika ufuatiliaji wa mwalimu kwa mwanafunzi pamoja na kujua changamoto zake za kitaaluma tofauti na wanaporundikana.
Katika kuhakikisha wanafunzi wenye ulemavu wanapata haki sawa ya elimu, Serikali ya awamu ya tano iliyoongozwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ikatoa fedha Tsh. Milioni 80 kujenga madarasa manne katika shule hiyo iliyopewa jina la Magufuli ambayo bado haijasajiliwa inatumia usajili wa Turwa shule ya msingi.
Darasa
Pia Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ikaendeleza pale alipoishia mtangulizi wake kwa kuongeza madarasa na ujenzi wa bweni la wasichana ambalo limebaki hatua ya ukamilishaji.
Katibu huyo wa shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu anaipongeza na kuishukuru Serikali kwa kuwaondolea adha walimu na wanafunzi kwani baada ya kujengwa madarasa hayo wanafunzi wanasoma kwa raha na kwa uhuru bila mbanano.
"Tunaishukuru Serikali yetu sikivu kwa kutuondoea changamoto ya vyumba vya madarasa ilitoa fedha Tsh. Milioni 140 fedha kutoka Serikali kuu yakajengwa madarasa 7,tangu mwaka 2020 wanafunzi wanasoma kwenye shule yao, wasioona wana madarasa yao, wasiosikia na weye ulemavu wa akili nao wana madarasa yao.
"Hii imerahisisha hata ufundishaji maana hawachanganyikani na ni rahisi kumpitia kila mwanafunzi, wanafurahia shule maana wapo huru wanasoma bila shida tofauti na walivyokuwa wakichagia darasa moja"anasema Mekaus.
Mwl. Mekaus anasema kuwa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 83 ambao ni wanafunzi wenye ulemavu wa akili, wasioona na wenye ulemavu wa kusikia, ina walimu wapatao 12 kati ya hao walimu wanaofundisha wenye ulemavu wa kusikia ni 6, wanaofundisha wenye ulemavu wa akili ni 3 na walimu 3 wanaofundisha wasioona.
"Mwalimu mmoja anatakiwa kufundisha wanafunzi watano tuna jumla ya wanafunzi 83, idadi ya walimu wote 12 kati ya hao wanawake 6, wanaume 6.
Wenye ulemavu wa akili
Mwl. Mekaus anasema wanafunzi wenye ulemavu wa akili ndio wengi ambao ni 59 kati ya wanafunzi 83 ina walimu 3 na kwamba mbali na upungufu wa walimu hakuna changamoto zingine kwa wanafunzi hao kwakuwa kuna vifaa vya kutosheleza vikiwemo vya kuchezea.
Wenye ulemavu wa kusikia
Mwl. Mekaus anasema hadi sasa shule hiyo ina wanafunzi 18 wenye ulemavu wa kusikia, ina wanafunzi wa darasa la kwanza hadi darasa la 6 na katika mwaka huu wa 2023 ina wanafunzi wanne wa darasa la sita wakike watatu na wa kiume mmoja.
Mwl. Jetruda Kilavo akiwafundisha wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia
Walemavu wasioona
Katibu huyo anasema shule ina jumla ya wanafunzi 6 wenye ulemavu wa kuona anasema kuwa kati ya wanafunzi hao wapo wanafunzi wawili wa darasa la nne.
Hali ya Taaluma
Mwl. Mekaus anasema kuwa kwa mara ya kwanza mwanafunzi kuhitimu darasa la saba ilikuwa mwaka 2017 ambapo alihitimu mwanafunzi mmoja mwenye ulemavu wa akili.
"Wanafunzi wanasoma hatua ya 1-3 baada ya hapo tunawachambua wapo wanaokwenda kwenye mafunzo ya ufundi na wengine kusoma darasa la 1-7 kulingana na uwezo wao, kuna aombao hawawezi kabisa tunawapeleka ufundi.
"Tulianza kuhitimisha darasa la saba mwanafunzi mmoja wa kiume wa ulemavu wa akili aitwae Amos Samwel , mwaka 2021 wanafunzi wawili walienda chuo cha ufundi Mwanza, akiwemo Frank Chacha ambaye ni yatima, wanafunzi wote wanasoma bure Serikali ndio inawalipia ada"anasema.
Anaongeza" Awali kulikuwa hakuna chuo wanafunzi walikuwa wanamaliza darasa la saba wanarudi mitaani, baada ya chuo tumefanikiwa kuwapeleka wanafunzi 3 chuo cha ufundi ambao ni walemavu wa akili.
Anasema kwa upande wa wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia shule imefanikiwa kuhitimisha wanafunzi watatu darasa la saba 2022 kati yao wawili waliendelea na masomo ya elimu ya sekondari katika shule maalum mkoani Arusha.
"Mwanafunzi mmoja hakufikisha alama tulimuomba akariri darasa akakataa mzazi wake anamtafutia chuo cha ufundi, angefaulu serikali ingemsomesha kama ilivyofanya kwa wengine.
Miundombinu
Anasema kuwa Serikali imejitahidi katika ujenzi wa madarasa kwani awali wanafunzi walichangia darasa moja lakini baadae Serikali ilijenga madarasa manne na choo mwaka 2020.
"Mwaka 2022 ikajenga madarasa matatu, hivyo kuwa na madarasa saba, majengo yanakidhi wanafunzi. Pia mwaka 2022 Serikali ikatujengea bweni la wanafunzi wa kike ambalo lipo kwenye hatua ya ukamilishaji lenye vyumba 20 ambalo litabeba wanafunzi 80 kila chumba kitakuwa na vitanda vinne" anasema Makaus.
Bweni la wasichana ambalo bado halijakamilika
Shule hiyo ina umeme ambao unawawezesha wanafunzi kutizama TV ili kujifunza mambo mbalimbali, ina king'amuzi cha kuwawezesha kutizama channeli mbalimbali za ndani na nje ya nchi na inavuna maji ya mvua kwa ajili ya matumizi ya shule.
Vitendea kazi
Katibu huyo wa Walemavu anasema kuwa Serikali imetoa vitabu vingi vya kufundishia na kujifunzia, vifaa vya kupima usikivu, meza, viti, vifa vya kusaidia usikivu, vifaa vya walemavu wa akili.
Baadhi ya vifaa vya walemavu wa kuona, kiti mwendo kimoja cha matumizi ya shule ambapo baadhi ya mashirika kama Angel House na ATFGM Masanga wamesaidia kuwapa viti mwendo baadhi ya wanafunzi.
Chakula
Anasema shule hiyo inatoa chakula kwa wanafunzi kinachogharamiwa na serikali na kwamba ratiba ya chakula ni saa moja asubuhi ambapo hunywa uji wa ulezi, saa sita mchana hula chakula kulingana na ratiba ya siku husika.
"Jumatatu wanakula wali nyama na matunda, Jumanne wali maharage, Jumatano Makande na chai, alhamis wali nyama na matunda , Ijumaa wali mboga za majani na kwamba huduma ya chakula ilianza kutolewa mwaka 2015.
Watumishi
Anasema shule ina jumla ya walimu 12, mlinzi mmoja na mpishi ambao wote wanalipwa na Serikali, wazazi hawachangii chochote.
Changamoto
Kulipo na mafanikio, changamoto hazikosekani, mbali na mafanikio hayo shule hiyo inakabiliwa na changamo kadhaa ikiwemo ya upungufu wa walimu, ofisi ya walimu, jengo la utawala, choo cha walimu, jiko, vitabu kwa ajili ya wanafunzi wasioona na wasiosikia.
Shule ya Magufuli haina vitabu vya Nukta Nundu, walimu wanalazimika kubadilili maandishi kutoka kwenye vitabu vya kawaida vya kufundishia kuwa ya nukta nundu kisha kuyachapa kwenye karatasi maalum kwa ajili ya wasioona kujifunza.
Pia haina vitabu na kamusi za lugha ya alama wala Video CD za lugha ya alama, vifaa vya kufundishia masomo ya Sayansi kwa wanafunzi wa darasa la tano hadi la saba kwa ajili ya wanafunzi wasiosikia.
Wanafunzi wenye ulemavu wa kuona wanalazimika kuchangia mashine moja ya kuchapa na kudurufu maandishi ya Nukta Nundu.
Mwanafunzi mwenye ulemavu wa kuona akitumia mashine kuchapa maandishi ya Nukta Nundu
Pia shule hiyo ya wanafunzi wenye ulemavu haina mtaalam wa tiba matamshi na wa tiba mazoezi.
Mabweni ni muhimu
Ukosefu wa mabweni umesababisha shule hiyo kuwa na idadi ndogo ya wanafunzi kwakuwa baadhi ya wazazi wameshindwa kuwapeleka shule watoto kutokana na kukosa nauli ya usafiri wa pikipiki kuwapeleka shule na kuwarudisha nyumbani kiasi cha Tsh 2000-3000 kwa siku huku baadhi ya wanafunzi wakiacha shule baada ya wazazi kukosa gharama za usafiri.
Mariam Turwa ni mlemavu wa viungo mkazi wa mtaa wa Rebu anasema ukosefu wa gharama za usafiri ni changamoto kubwa inayokwamisha watu wenye ulemavu kupata elimu kwakuwa baadhi ya watoto wanatoka kwenye familia zisizo na uwezo wa kumudu nauli kila siku.
"Watu hatulingani uwezo ndio maana unaona hata vidole vya mikono na miguu vinapishana urefu kwahiyo mtu anafikilia kila siku atatoa wapi pesa za nauli wakati hata chakula cha nyumbani ni shida, serikali isaidie ijenge mabweni kwa wanafunzi wote wa kike na wavulana ili watoto waishi shuleni" amesema Mariam.
Thobias Ghati ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji Tarime ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyamisangura anasema anazifahamu changamoto hizo kwakuwa naye alishafika shuleni hapo akiwa ameongozana na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Kata hiyo kuona maendeleo ya shule na changamoto.
Diwani Thobias anasema kwamba changamoto hizo zinafanyiwa kazi huku akiipongeza Serikali kwa ujenzi wa madarasa pamoja na mafanikio mbalimbali katika kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanapata elimu bora.
Imeelezwa kuwa endapo mabweni yakijengwa na kukamilika itasaidia wanafunzi wengi kujiunga na shule kwakuwa wataishi shuleni wazazi hawatasumbuka gharama za usafiri.
Changamoto hizo zikitatuliwa itasaidia kukuza taaluma ya wanafunzi wenye mahitaji maalum kwani utoaji wa elimu bora ni nguzo muhimu ya maendeleo katika nchi yoyote duniani.
Elimu bora husaidia kupata rasilimali watu wenye maarifa, stadi na mahiri katika nyanja mbalimbali na hivyo kuchangia maendeleo ya nchi.
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekuwa ikijitahidi kutatua changamoto za elimu ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa nchini.
Pia imedhamilia kuhakikisha kwamba elimu inayotolewa nchini inakidhi viwango vya ubora katika nyanja zote muhimu.
Baadhi ya viwango hivyo ni ubora wa mazingira wezeshi ya utoaji elimu yanayozingatia usalama, afya, ustawi wa wanafunzi sambamba na uwepo wa miundombinu bora na yenye utoshelevu na huduma muhimu za kijamii.
Post a Comment