WANANCHI WATAKIWA KUSIMAMIA NA KUTUNZA MIRADI ILIYOJENGWA
Na Jovina Massano, Musoma.
VIONGOZI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali ya mkoa wa Mara wamewaomba wananchi kusimamia na kutunza miradi ya maendeleo kwani miradi hiyo imegharimu fedha nyingi.
Ombi hilo limetolewa Februari, 5,2023,wakati wa kusherekea miaka 46 ya kuzaliwa Chama cha Mapinduzi (CCM) yaliyofanyika kimkoa katika Wilaya ya Musoma viwanja vya shule ya msingi Kigera .
Mkuu wa mkoa huo Meja Jenerali Suleiman Mzee amesema katika kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, wananchi wana wajibu wa kusimamia miradi ya maendeleo.
"Hiyo miradi yote ni yenu isimamieni msikubali wizi, ni jukumu letu kuisimamia na nitawachukulia hatua wote wanaotaka kuikwamisha miradi", amesema Suleiman.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Chama cha Mapinduzi, Christopher Mwita Gachuma amewaomba wananchi kuhakikisha wanasimamia na kutunza miradi yote iliyopo katika maeneo yao ili iweze kuwanufaisha sasa na baadae.
Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania ( UWT) Bara, Joyce Ryoba Mang'o amewaomba Viongozi na watendaji wote wanaopewa ridhaa ya kusimamia miradi waisimamie kwani Serikali inajitahidi kuhakikisha wananchi wake wanapata maendeleo.
Pia Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini Joseph Kasheku Msukuma, amewaomba viongozi wa CCM, Mkuu wa mkoa wa Mara na Wakuu wa Wilaya kusimamia na kudhibiti mfumko wa kupanda bei za bidhaa na chakula na kwamba suala hilo sio la Rais.
Mkazi wa Kwangwa Consolata Nyakabwende amemshukuru Joseph Kasheku Msukuma aliyekuwa mgeni katika maadhimisho hayo kuwasisitiza viongozi kusimamia kupanda kwa bei za bidhaa.
Consolata amesema kuwa wao waliamini kuwa Rais Samia ndiye anasababisha maisha kuwa magumu lakini mbunge Msukuma amewafungua upeo.
"Yaani huyu baba ametufungua masikio tulikuwa tunamchukia Rais Samia kuwa analeta tabu kumbe ni watendaji, haya maneno yameingia moyoni mwangu tungekuwa tunayapa mapema tusingemlaumu ametupatia maneno mazuri nimefurahi sana", amesema Consolata.
Kushoto ni MNEC Joseph Msukuma akisalimiana na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara Patrick Chandi, wa pili kushoto ni Katibu wa CCM mkoa wa Mara Langael Akyoo, wa kwanza kulia ni MNEC Joyce Mang'o.
Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Butiama ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Jumanne Sagini, kulia ni MNEC Joyce Mang'o.
Post a Comment